A

A

SALAMU ZANGU KWA RAIS NA KIONGOZI AJAYE WA TAIFA HILI


Salamu  za mwisho kwa Rais wangu
Na Angela Kiwia
NIMEKUWA na utaratibu wa kumuandikia Rais wangu barua  na salamu ambazo huandikwa kupitia ukurasa huu.Nimekuwa nikitumia utaratibu huu kutokana na kutopata fulsa ya kumkaribia na kuonana naye uso kwa macho.Hivyo basi kutokana na fulsa niliyonayo kupitia Kurunzi nimekuwa nikimtumia salam zangu ambazo kwa hakika huwa zinamfikia ipasavyo.
Natambua ya kuwa wapo ambao wamekuwa wakifikisha salamu hizi kwa kuzipindisha na kuweka uchochezi kwa manufaaa yao, lakini kwa vile natambua kwa busara zake ikiwa ni pamoja na kutumia kanuni ya mbayuwayu ya kuchanganya na zake, huwa anawapuuza kutokana na yeye binafsi kuujua ukweli kutokana na kupata fulsa ya kusoma maandiko hayo.
Leo nimeona heri kumalizia salamu zangu kwake kutokana na kuwa salamu za mwisho hasa katika kipindi hiki ambacho ninaamini ya kuwa sitarajii kumtumia salamu nyingine kutokana na kile nitakachokieleza katika salamu hizi.
Mh.Rais wetu, pole sana na majukumu ya kila iitwayo leo, pole kutokana na baadhi ya mambo unalazimika kuyafanya mwenyewe kwa vile wale uliowateua waweze kukusaidia wameamua kuishi maisha ya kutanua na kujifanya kuwa wamesahau majukumu yao huku lawama zikielekezwa kwako kutokana na uteuzi huo.
Pamoja na kukupa pole, naomba nikupongeze kwa kuweza kupata kijana, mchapakazi, anayejitambua katika kutekeleza majukumu yake uliyomkabidhi.Katika kipindi kifupi kilichopita uliweza kuona na kusikia Watanzania wakilalamika kwa kuwa na wasaidizi ambao ni Mawaziri mizigo katika baraza lako la mawaziri.
Pamoja na juhudi zilizofanyika katika kuhakikisha mizigo hiyo inaondoka na kumalizika ambazo zilifanywa na wewe binafsi ikiwa ni pamoja na chama wapo ambao wamebaki na si mizigo tu bali wanyonyaji na wafujaji wa raslimali na fedha za walipa kodi.
Mtukufu Rais, katika baraza lako la mawaziri unao baadhi yao ambao ni wachapakazi na walioweza kujitanabaisha kuwa wanayo nia ya dhati, kutoka uvunguni mwa mioyo yao kuwa wapo tayari kuhakikisha wanasaidiana na Watanzania wenzao nchi yetu inasonga mbele na tunaondokana na unyonywaji unaofanywa na kupe wachache wabinafsi.
Nikupongeze kwa uteuzi wako wa Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Naibu Katibu Mkuu wa CCM,Mwigulu Nchemba.Huyu ameweza kutumia halmashauri yake ya kichwa kutuonyesha ni kwa kiasi gani bado taifa hili linao vijana wazelendo wenye uthubutu wa kusema hapana, imetosha.
Mh.Rais  wapo wanaaona kuwa wanalitendea hila taifa hili bila kipingamizi wala taabu, na wanaamini ya kuwa hiyo ni haki yao, lakini nilichoweza kuona kwa Mwigulu ni pale anapojidhihirisha kuwa wadharimu hao mauti yao yamekaribia.
Nchi hii haiko salama hata kidogo, hali ni tete na kwa bahati mbaya baadhi ya wasaidizi wako hawaoni kwani macho yao yamepigwa upofu kutokana na  kukubali kuwa mizigo na watwana, wasio na uchungu na taifa lao bali wao na familia zao.Wanaona fahari kuwa wazurulaji wazuri wanaoishi maisha ya angani huku ndugu zao wakiwalaani viongozi waliowateua.
Mh Rais sina shaka na uhuru wa kweli, wa pili wa taifa ili katika siku chache zijazo.Uhuru huu utakaoletwa na vijana wa leo na walio tayari kuisemea na kuikomboa nchi yao kama afanyavyo Mwigulu Nchemba.
Hakuna mtu atakayeweza kuzuia mabadiliko hata kama wanayoyataka sasa hawatokuwepo wakati huo.Ninachotambua ni kwamba kukosa hekima kwa baadhi ya wasaidizi wako katika uongozi kunakusababishia lawama zisizo na maana kutokana na kuwa wewe ndiyo mteule wao.

Mh Rais, baadhi ya ndugu zetu wameendelea kuteseka kila kukicha, wakiishi maisha magumu,  lakini wamekuwa wakisikia ya kuwa baadhi ya wateule wako wanaishi maisha ya anasa na kutumia fedha za walala hoi hao katika mambo ya hovyo.
Wagonjwa mahosiptalini wanakufa kwani panadol imekuwa dawa ya kutibu maradhi yote, lakini baadhi ya mawaziri wako wanaishi Marekani na kufanyakazi Tanzania.
Nikushukuru kwa kumteua Mwigulu ambaye ameweza kulionyesha taifa hili mwanga na kudhihirisha ni kwa kiasi gani nchi yetu ilivyo na hazina ya wapambanaji.Hivi karibuni niliweza kumsikia mimi binafsi akiapa kupambana na wafanyabiashara wanaokwepa kodi na kuliibia taifa hili tajiri lenye jina baya nisilolipenda la Masikini.
Niliweza kumsikia jinsi anavyosikitishwa na uwepo wa rasilimali tele kama vile dhahabu , Tanzanite , Gesi , Almasi , Mbuga za Wanyama , Madini ya Urani , Mlima Kilimanjaro , Kahawa , Pamba , Korosho , Bandari , Mito na maziwa pamoja na vitu vingine vingi, lakini  bado vimeshindwa kutoa mwanga wa maendeleo katika Taifa hili kutokana na uzembe wa watu wachache walio tayari kukuangusha katika uongozi wako.
Mwigulu ameniwezesha kufanya mang’amuzi sahihi katika kipindi hiki ambacho nchi yetu inakumbana na changamoto za kila aina huku baadhi ya wanaharakati wa kisiasa wakitumia mwanya huo kuwachonganisha Watanzania na viongozi wao.
Mh Rais wetu, sina uwezo wa kukutishia ila napenda kukufahamisha ya kuwa Mungu hadhiakiwi,bali kila apandacho mtu ndicho avunacho, najua watakuja wapuuzi wanaojipendekeza kwako kisha watakuambia umeona ujinga wa yule mwandishi wa Kurunzi? watasema kwako na kwingineko kuwa nimeandika ujinga, watakebehi na hata kuniita mchochezi kwenye mambo ya msingi.
Nimeyaandika haya baada ya kutafakari kuhusu taifa letu, nchi yetu na hatima yetu na vizazi vyetu.Nimeandika kukukumbusha jinsi baadhi ya wateule wako wasivyo na udhu hata wa kukukaribia.
Watanzania wanalazimishwa kukata tamaa kutokana na baadhi ya wasaidizi wako kuwatelekeza, wanakerwa na viongozi wasiowajali wao wala nchi yao.Nakuomba rais wangu usiwape nafasi warafi na wazandiki ya kuendelea kukuchafua kutokana na mambo yao ya hovyo wanayofanya.
Finitoooooo

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako