A

A

Msomi ashauri muundo wa serikali mbili ulioboreshwa




Wajumbe wa Bunge la Katiba wakipinga jambo ndani ya Bunge juzi wakati Kamati Namba Tatu  na Nne zilipowasilisha ripoti zao  mjini Dodoma.Picha na Salhim  Shao 

Kwa ufupi
  • Ni Profesa wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ushirika na Biashara Moshi, anayesema muundo huo unafaa kwa sharti la kuboreshwa


Dodoma. Profesa Robert Msanga wa Chuo Kikuu kishiriki cha Ushirika na Biashara Moshi (Muccobs) amependekeza muundo wa Muungano wa serikali mbili uendee kutumika isipokuwa uboreshwe.
Akizungumza na gazeti hili jana, Profesa Msanga ambaye pia ni Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, alisema kumekuwapo dhana potofu juu ya
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“Ukijadili aina hii ya Muungano tulionao, ina maana unataka kututoa nje ya Muungano huu ambao umedumu kwa miaka 50. Sisi tunataka tubaki hapa tulipo isipokuwa tuuboreshe,”alisema.
Profesa Msanga alisema kilichoungana siyo nchi, bali watu wa mataifa hayo mawili ambao waliungana kiuchumi, kisiasa na kijamii na kufanya wawe watu wa taifa moja lenye mshikamano.
“Hata ukifananisha Muungano wetu na ndoa ya kidini haina maana wanapoungana mwili na roho ndio hata wakitembea barabarani watakuwa wameshikana. Muungano wetu ni hivyo,” alisema.
Aliongeza kuwa kwa vyovyote vile, muundo wa serikali tatu utaongeza gharama kwa nchi washirika, wakati gharama hizo zinaweza kuepukwa kwa kuondoa tu kero za Muungano wa sasa.
“Serikali  haizalishi inategemea watu na rasilimali na hata muundo wa sasa tunawakamua wananchi wetu maskini. Sasa hiyo Serikali ya tatu chanzo chake cha mapato ni kipi?” alihoji.
“Kwa hiyo kama ni kuungana tayari tuna Muungano wa serikali mbili, tunataka serikali ya tatu ya nini? Tayari tuna ushirikiano tuuboreshe tu.”