A

A

Wapinzani wa Yanga na Azam kutua Dar es salaam leo

Dar es Salaam. Wapinzani wa Yanga timu ya Komorozine de Domoni kutoka Comoro watatua nchini leo tayari kwa mchezo wa Jumamosi wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa.
Yanga imepangwa kuanza na Wacomoro hao katika hatua ya awali ya mashindano hayo makubwa ya klabu barani Afrika. Wakifanikiwa kusonga mbele watavaana na Al Ahly ya Misri. Mchezo huo wa Yanga utachezeshwa na waamuzi kutoka Somalia wakati wenzao wa Azam watachezeshwa na waamuzi kutoka Sudan Jumapili ijayo. Ofisa habari wa Yanga, Baraka Kizuguto alisema jana  kikosi chao kipo Bagamoyo kujiandaa na mchezo huo.
“Bagamoyo ndiyo kambi yetu ya kudumu hadi Ligi na mashindano yote tumalize. Kila kitu kinaenda vizuri, wachezaji wanaanza mazoezi rasmi ya kuwakabili Wakomoro leo (jana), baada ya mapumziko ya siku moja.” alisema
Hata hivyo Yanga itashuka dimbani bila ya mchezaji wao tegemeo Emmanuel Okwi ambaye amezuia kucheza na Kamati ya Maadili na Hadhi ya Wachezaji baada ya usajili wake kuwa na utata na kusubiri ufafanuzi kutoka Shirikisho la Soka duniani (FIFA).
Akizungumzia suala la mshambuliaji huyo Bonifance Wambura alisema “Fifa tulishawakumbusha kuhusu ufafanuzi tulioomba wa Okwi, wametujibu kuwa wameshapata barua yetu na wataifanyia kazi, ni lini sijui, ndiyo tunasubiri mpaka watakapotujibu.” alisema
Azam nao wameingia kambini jana kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Ferroviario De Beira ya Msumbiji katika raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho.
Iwapo timu hiyo yenye maskani yake Chamazi itafanikiwa kuwanyuka Ferroviario na kuvuka hatua hiyo  watamenyana na mshindi kati ya St Michel ya Shelisheli na ASSM Elgeco Plus ya Madagascar.
Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako