A

A

Baba amshitaki mwanaye wa pekee kwa kumwoa mwanamke masikini

 PATNA, India -- MWANAMUME nchini India amemshtaki mwanawe wa pekee wa kiume katika mahakama kwa kumharibia sifa, alipoamua kumuoa mwanamke wa tabaka la chini.

Alisema kwamba kitendo hicho kimemharibia sifa na hadhi yake katika jamii.

Mzee Sidhnath Sharma anataka alipwe rupia 10,000,000 (KSh13,638,900) na mwanawe Sushant Jasu, na anataka mahakama iamuru kwamba kijana huyo asitumie tena jina la familia.

Sharma, ambaye ni wakili kutoka ukoo wa familia ya watu wanaojiweza ya Bhumihar, alisema ndoa aliyofunga mwanawe 
mwishoni mwa mwaka jana ilivunja mwiko ambao umedumishwa kwa miaka 400, kwamba mtu wa familia ya hadhi ya juu hafai kumwoa wa walalahoi.

“Kwa miaka mingi, sheria hii imekubaliwa na kwamba ndoa ni lazima zipangwe na wazazi kwa sababu ya kuwa mtu amuoe wa hadhi yake. Lakini mwanangu pekee ameamua kumaliza utamaduni huu. Sio tu kwamba nimepigwa na butwa, bali pia kitendo chake kimetia doa hadhi yangi katika jamii,” aliambia shirika la Habari la Ufaransa, AFO nyumbani kwake mjini Danapur, viungani mwa jiji la Patna.

Mtindo huo wa kuwagawa watu katika makundi kulingana na hadhi zao, umerithiwa mno nchini India kiasi kwamba umekita mizizi hata miongoni mwa wasomi na watetezi wa haki za binadamu.

Cha kushangaza ni kwamba, unafuatwa hata katika jimbo la Bihar, mojawapo ya maeneo maskini zaidi na yenye idadi kubwa ya watu nchini India.

Itikadi hiyo ndiyo dira hasa ya maisha ya watu wengi wa India, na inaweza kuamua kuhusiana na masuala ya ndoa, elimu, ajira na umiliki wa ardhi, japokuwa sharia za nchi hiyo zinapiga marufuku kuwabagua watu kwa misingi ya hadhi zao.

Watu wanaokwenda kinyume na wazazi wao na kuamua kuoa nje ya matabaka yao, mara kwa mara wamekuwa wakiuawa, katika kinachotajwa kuwa 'mauaji ya kuhifadhi hadhi’ ili wanandoa wasiharibu heshima na sifa za wazazi wao. Sharma aliwasilisha keshi dhidi ya Jasu mwezi uliopita na mahakama mjini Danapur inatarajiwa kuanza kuisikiza kesi hizo kesho Jumamosi.

Benki

Jasu, ambaye ni afisa mkusanyaji mapato katika jimbo la Gujarat, alimwoa mke huyo anayefanya kazi katika benki mjini Danapur mwezi Novemba mwaka jana. Sharma anasema iwapo mwanawe ataendelea kutumia jina la familia kwenye jina lake, ataomba alipwe rupia 10,000 kama ada ya hakimiliki, kila mara atakapotajwa au kusikika akiitwa na mtu.

“Nimeiomba mahakama imwagize anilipe kwa kuniumizahisia zangu, kisaikolojia na pia kwa kuniharibia hadhi yangu katika jamii. Ninataka anilipe gharama yangu yote niliyopata kumfanya awe mtu aliye sasa,” akasema.

Jasu alikataa kuzungumza kuhusu kesi hiyo.


-- via SwahiliHub

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako