Balozi
Seif akiwa pembezoni mwa dirisha ndani ya chumba cha chini ya Bahari
akiangalia samaki na mazingira yake mara baada ya kuuzindua mradi huo
hapo Manta Resort Hoteli Makangale.
Balozi
Seif akiangalia ngazi ya kutokea juu ya chumba cha chini ya Bahari
katika Hoteli ya Manta Resort Makangale Mkoa wa Kaskazini Pemba kwenye
sherehe za uzinduzi wa chumba hicho ikiwa ni muendelezo wa sherehe za
kutimia miaka 50 ya mapinduzi ya Zanzibar.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimpongeza Meneja Mkuu wa
Hoteli ya Manta Resort Bwana Methew Saus kwa kukamilisha ujenzi wa
chumba cha chini ya Bahari kwenye hoteli yake iliyopo Makangale Mkoa wa
Kaskazini Pemba huku Waziri wa Habari Mh. Marouk akifurahia kitendo
hicho.
Kitanda
na mandhari halisi na nzuri iliyomo ndani ya chumba cha chini ya Bahari
katika hoteli ya Manta Resort Makangale Kaskazini Pemba mradi
uliozinduliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif.
Sehemu ya choo katika chumba cha chini ya Bahari kilichopo kwenye Hoteli ya Manta Resort huko Makangale Pemba.
Meneja
Mkuu wa Hoteli ya Manta Resort Bwana Methew Saus Maarufu “ Babu kwa
Nini “akitoa maelezo ya hatua zilizochukuliwa kukamilisha ujenzi wa
chumba cha chini ya Bahari katika Hoteli ya Manta Resort iliyoko
Makangale Mkoa wa Kaskazini Pemba.Kushoto
ya Balozi Seif ni Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi, Waziri wa Habari,
Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk na Naibu wake Mh.
Bihindi Hamad.
Meneja
Mkuu wa Hoteli ya Manta Resort Bwana Methew Saus akionyesha eneo la juu
la chumba cha chini ya bahari ambapo mgeni atapata fursa ya kupunga
upepo pamoja na kuota jua.
Mandhari nzuri ya Hoteli ya Manta Resort ya Makangale Mkoa wa Kaskazini Pemba eneo ambalo kipo chumba cha chini ya Bahari.
Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mradi
mpya wa ujenzi wa Chumba cha chini ya Bahari uliofanywa na Hoteli ya
Manta Resort iliyopo katika Kijiji cha Makangale Mkoa wa Kaskazini Pemba
umeiweka Zanzibar katika ramani mpya ya Dunia katika harakati za
kuimarisha sekta ya Utalii unaobeba nafasi kubwa ya Uchumi katika
Mataifa mengi Ulimwenguni.
Chumba
hicho cha chini ya Bahari kilichopo Makangale ambacho ni cha pekee
Barani Afrika kimeiwezesha Zanzibar kuwa ya tatu kwa kuwa na mradi kama
huo Duniani ikitanguliwa na Nchi za Puerto Riko,Sweden, Kisiwa cha Fiji
na ikifuatiwa na Dubai.
Mradi huo
ulioko katika Matengenezo unatarajiwa kuwa na vyumba takriban 220.
Jengo hilo lenye huduma kamili anazostahiki kuzipata mwanadamu ni pamoja
na chumba cha kulala,huduma za maji safi,Choo, umeme, sehemu ya
Mapumziko, na eneo maalum la juu kwa ajili ya kuotea jua. Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ambae ndiye aliyeweka Nanga ya
Msingi ya mradi huo wa Makangale Miezi 12 iliyopita Tarehe 25/12/2012
akakizindua tena rasmi chumba cha mradi huo kilichoko umbali wa mita Nne
chini ya Bahari.
Uzinduzi
huo uliojumuisha mamia ya Wananchi wa Kijiji cha Makangale pamoja na
majirani zake ulishuhudiwa pia na Viongozi kadhaa wa Serikali, vyama vya
Siasa pamoja na watendaji wa Sekta ya Utalii wakiongozwa na Waziri wa
Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk na Naibu wake
Mh. Bihidndi Hamad.
Akizungumza
mara baada ya kuuzindua Mradi huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif alisema kwamba uwepo wa mradi huo wa chumba cha chini ya
Bahari ni kielelezo muhimu kitakachokuwa kivutio kwa wageni katika
harakati za kukuza utalii hapa Zanzibar.
Balozi
Seif aliupongeza Uongozi wa Hoteli ya Manta Resort ya Makangale kwa
kuamua kuwekeza mradi huo wa kipekee Barani Afrika ambao utaleta
maendeleo makubwa katika Sekta ya Utalii. “ Nimeshuhudia uzuri wa chumba
hichi ambapo yapo mazingira mazuri ya mapumziko na kulala, samaki wa
kuvutia.
Natarajia
wakaazi wanaonguuka eneo hilo watashirikiana vyema na uongozi wa Hoteli
hiyo katika kukilinda chumba hicho kinachotarajiwa kuongeza ushawishi
kwa watalii kutembelea Zanzibar “. Alisisitiza Balozi Seif.
Alielezea
matumaini yake kwamba Uongozi wa Hoteli ya Manta Resort Makangale
utaendelea kutoa huduma bora na za uhakika ili kuongeza idadi ya wageni
na watalii kutembelea Pemba. Katika kuunga mkono jitihada hizo za
wawekezaji alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwapa
mashirikiano ya karibu wawekezaji wa sekta hiyo ili waendeshe shughuli
zao kwa ufanisi mkubwa.
“ Sisi
Viongozi wa Serikali akiwemo Mheshimiwa Rais, Makamu wa Kwanza wa Rais
na mimi mwenyewe tunapofanya ziara nje ya nchi hutumia fursa ya
kuwabembeleza wawekezaji kuwa kuwekeza Nchini mwetu hasa katika sekta ya
utalii na Viwanda.
Bahati
nzuri wanatuitikia na wanakuja na ndio maana leo Zanzibar ina vitega
uchumi vingi vya sekta ya utalii na mfano hai ni huu mradi wa chumba cha
chini ya Bahari hapa Makangale “. Alifafanua Balozi Seif.
Alifahamisha
kwamba pamoja na maendeleo ya ujenzi wa miradi ya uwekezaji katika
sekta ya utalii lakini bado Serikali pamoja na Wananchi wanahitaji
kuendelea kuwa na matumaini ya kuongezeka kwa idadi ya watalii hali
ambayo itasaidia kuongeza mapato ya Taifa.
Hata
hivyo Balozi Seif alitahadharisha kwamba watalii na wageni hao
hawataingia nchini iwapo jamii haitojikita katika kuendeleza amani na
utulivu ndani ya maeneo yao hasa sehemu zenye vitega uchumi hivyo.
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar alisema wananchi hawanabudi kupania kuiweka
nchi katika hali hiyo ya amani na usalama ili wageni hao washawishike
kupenda kuendelea kutembelea Nchini na kuishi bila ya wasi wasi.
“ Tuwe
wanyenyekevu kwa wageni wetu, tuwaonyeshe bashasha za Kizanzibari kama
ilivyo tabia na desturi yetu, tusiwabughudhi wakiwa ufukweni au katika
matembezi yao. Tunataka wafurahie ukaazi wao katika visiwa vyetu vya
karafuu na Viungo “. Alieleza Balozi Seif.
Mapema
Meneja Mkuu wa Hoteli ya Manta Resort Bwana Methew Saus Maarufu “ Babu
kwa Nini “ alisema utafiti wa mradi huo ulifanyika kwa karibu miaka sita
ambapo wataalamu wa kimazingira na mambo ya bahari walilazimika kupima
mwenendo wa maji ya bahari ya eneo hilo ili kuwa na uhaika wa kuanzisha
mradi huo.
Bwana
Methew Saus alisema mazingira ya Kisiwa cha Pemba yamepelekea kuanzishwa
kwa mradi huo wa majaribio wa chumna cha chini ya Bahari uliogharimu
zaidi ya Dola za Kimarekani Laki Tano { U$ 500,000 } sawa na fedha za
Kitanzania Milioni Mia 758,000,000/-.
Meneja
huyo wa Hoteli ya Manta Resort ya Makangale ameipongeza Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Wizara inayosimamia Sekta ya Utalii kwa
ushirikiano iliyompa kuweza kufanikisha mradi huo muhimu kwa maendeleo
ya uchumi wa Zanzibar.
Akimkaribisha
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Waziri wa Habari,
Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk alisema mradi huo kwa
kiasi kikubwa umeanza kuitangaza vyema Zanzibar katika sekta ya utalii
wa Daraja la juu duniani.
Waziri
Mbarouk aliwaasa wananchi na hasa wavuvi wanayoizunguuka hoteli hiyo
kujiepusha na uvuvi pembezoni mwa mradi huo jambo ambalo litaondoa sifa
na mazingira halisi ya kuwepo kwa samaki wanaokizunguuka chumba hicho.
Alikemea
tabia iliyoanza kujichomoza ya baadhi ya wavuvi wa maeneo hayo ya kuvua
kwa kutumia nyavu ndogo nje ya chumba hicho kwani inaweza kumvunja moyo
muwekezaji huyo ambae ameshajitolea kusaidia maendeleo ya Vijiji jirani
na Hoteli hiyo.
Mradi
wa mwanzo wa ujenzi wa vyumba vya chini ya Maji Jules Undersea Lodge
umeanza Nchini Puerto Rica mwaka 1970, Utter In Vasteras Sweden Mwaka
2000, Poseidon Undersea Resort Fiji na Mwengine Crescent Hydropolis
unaendelea kujengwa Nchini Dubai.
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako