Mzee huyo Pascal Mwanjelanje(75) alinusurika kuzikwa akiwa hai
akituhumiwa kumuua mke wa mtoto wake aliyejulikana kwa jina la Salome
Amosi (20).
Kaburi ambalo angezikwa huyo mzee
Mume wa Marehemu, Moses Pascal (27) mkazi wa Uyole Jijini Mbeya
alisema mkewe alifikwa na umauti walipokuwa wameenda kijijini kwao
Shilanga kwa ajili ya kilimo lakini kabla ya kifo cha Mkewe walikuwa
wametoka Hospitali kumtibu mtoto wao majira ya saa Tisa alasiri.
Mwenyekiti wa kijiji cha Shilanga, Romani Tubuke, alisema lilitokea
hivi karibuni majira ya saa 9 alasiri wakati marehemu Salome Amosi (20)
kupoteza maisha akiwa anafua nguo katika mto uliojirani na kijiji hicho.
Mzee mmoja mkazi wa kijiji cha Shilanga Wilaya ya Mbeya Mkoani hapa
amenusurika kuzikwa akiwa hai akituhumiwa kumuua mkwewe kwa ushirikina.
Tukio lilitokea hivi karibuni majira ya saa tisa alasiri ambapo Mzee
huyo Pascal Mwanjelanje(75) alinusurika kuzikwa akiwa hai akituhumiwa
kumuua mke wa mtoto wake aliyejulikana kwa jina la Salome Amosi (20).
kupona kwa mzee huyo kumetokana na kugoma kwenda sehemu lilipochimbwa
kaburi kwa ajili ya mazishi ya marehemu baada ya kushtukia mchezo
mchafu wa vijana waliokuwa wakichimba kaburi.
mzee huyo alishtukia kufuatia tukio la awali lililotokea Novemba 6,
Mwaka huu katika kijiji cha Mshewe Wilayani hapa ambapo watu Sita
akiwemo Mwenyekiti wa kijiji walipandishwa mahakamani wakituhumiwa
kumzika mtu akiwa hai wakimtuhumu kumuua mwanaye kwa ushirikina.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa kijiji cha Shilanga, Romani
Tubuke, alisema lilitokea hivi karibuni majira ya saa 9 alasiri wakati
marehemu Salome Amosi (20) kupoteza maisha akiwa anafua nguo katika mto
uliojirani na kijiji hicho.
Alisema baada ya kupata kwa taarifa za msiba huo familia iliandaa
matanga kama kawaida ambapo siku iliyofuata vijana wa kuchimba kaburi
walianza kuchimba majira ya saa sita mchana ambapo kabla ya kukamilisha
walisitisha zoezi hilo na kisha kuandamana hadi walipowaombolezaji na
kuwasihi wanyamaze.
Alisema baada ya watu wote kukaa kimya ndipo vijana hao walipohoji
sababu ya kifo cha marehemu na kutaka majibu ya kuridhisha ili
wakaendelee na shughuli za machimbo ambapo walianza kumuuliza bibi
aliyemlea marehemu ambaye aliulizwa kama mjukuu wake amewahi kuwa na
tatizo lolote lakini alijibu kuwa mjukuu wake hakuwahi kusumbuliwa na
ugonjwa wowote.
Alisema kutokana na majibu ya bibi huyo vijana hao walimsimamisha pia
Mume wa Marehemu Moses Pascal(27) ambaye alisema yeye binafsi hajui
ugonjwa uliomuua mkewe zaidi ya kuletewa taarifa kuwa amekufa mtoni
akiwa anafua baada ya yeye kuachiwa mtoto nyumbani.
Hata hivyo vijana hao hawakuridhika na majibu hayo na kuamua kumwita
mzee Pascal Mwanjilanji wakitaka aeleze sababu za kifo cha mkwewe lakini
aligoma kuzungumza lolote na walipomwita kusogea eneo la kaburi mzee
huyo hakukubali ndipo vijana hao walipoamua kufukia kaburi kisha kuubeba
kinguvu mwili wa marehemu na kuhamishia katika kijiji cha Nungwe kwa
wazazi wa marehemu ambako walichimba kaburi lingine na kutaka kuzika.
Aliongeza kuwa kabla hayo yote hayajafanyika taarifa zilipelekwa
Jeshi la Polisi ambao walifika eneo la tukio na kuwasihi watulie hadi
Serikali itakapopima mwili wa marehemu ili kubaini ugonjwa
uliomsababishia kifo na kisha kuamua ni upande upi unapaswa kuzika na
siyo kung’ang’aniana mwili wa marehemu.
Baadhi ya ndugu wa marehemu walisema kitendo cha kuhamisha mwili wa
marehemu haukufanywa na wao bali ni vijana waliokuwa wakichimba kaburi
ambao hata wao hawakuhusishwa na ugomvi waliokuwa nao zaidi ya wao
kuamrishwa kuondoka eneo la msiba na kuhamia kwao.
Mzee wa mila wa kijiji cha Dimbwe, Hezron Dimbwe alisema mwenye
jukumu la kuzika ni upande wa wafiwa ambao ni ukoo wa mwanaume aliye
muoa na si vinginevyo hivyo kama serikali itaamua wasizike Familia ya
upande wa marehemu italizimika kulipa fidia kijijini kwa ajili ya
kufukia kaburi.
Naye Mume wa Marehemu, Moses Pascal (27) mkazi wa Uyole Jijini Mbeya
alisema mkewe alifikwa na umauti walipokuwa wameenda kijijini kwao
Shilanga kwa ajili ya kilimo lakini kabla ya kifo cha Mkewe walikuwa
wametoka Hospitali kumtibu mtoto wao majira ya saa Tisa alasiri.
Alisema baada ya kurudi nyumbani mkewe aliaga kwenda mtoni kufua
hivyo alimwachia mtoto abaki naye lakini baada ya muda kidogo akapata
taarifa za kifo chake na kwamba alifanya juhudi za kwenda kumchukua
hivyo hakukua na maongezo yoyote kabla ya kifo.
Akizungumzia kuhusishwa kwa baba yake na kifo hicho alisema ni maneno
ya uzushi kutoka kwa watu na kwamba huenda anahusishwa kutokana na
kubaki peke yake katika ukoo wao kutokana na wenzie wote kufa hivyo
kuhusishwa na ushirikina.
Aliongeza kuwa bado baba yake anahusishwa kufuatia kifo chenye utata
cha mtoto wake wa kwanza ambaye alifariki baada ya kumwagikiwa na maji
ya uvuguvugu jambo ambalo pia baadhi ya watu walimtuhumu baba yake mzazi
kuwa ni mshirikina.
Aidha hadi tunaingia mtamboni Mwili wa marehemu ulikuwa upo katika
chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa ajili
uchunguzi ili kubaini sababu ya kifo cha marehemu ili baada ya kupata
majibu pande zote mbili zielezwe na kufafanuliwa na kukabidhiwa kwa
taratibu za mazishi.
Na Mbeya yetu




No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako