Na Mwandishi,
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe anatarajiwa kufanya mabadiliko ya baraza lake kivuli la mawaziri.
Katika mabadiliko hayo, Mbowe anatarajiwa kuingiza sura mpya, kuhamisha baadhi wizara, wengine kubaki kwenye nafasi zao huku akiwatoa baadhi yao.
Kwa mujibu vyanzo mbalimbali ndani ya kambi hiyo, Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), anatarajiwa kulitangaza baraza hilo wakati wowote.
Baraza kivuli alilolitangaza Februari 5, 2016 bungeni jijini Dodoma lilikuwa na wizara 18 likijumuisha vyama washirika wa Ukawa vyenye wabunge; NCCR-Mageuzi, Chadema na CUF.
CUF kwa sasa imegawanyika katika pande mbili; upande unaomuunga mkono Profesa Ibrahim Lipumba, mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na upande wa katibu mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.
Baada ya kuzitenganisha wizara hizo sasa zimekuwa nne. Kilimo inajitegemea kama ilivyo Mifugo na Uvuvi huku ya Nishati na Madini nayo ikigawanyika kuwa Wizara ya Madini na nyingine ya Nishati.
Kanuni ya 15(2) ya Bunge inampa mamlaka kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuteua wabunge wa chama chake au wabunge wa kambi ya upinzani ambao watakuwa wasemaji wakuu wa kambi ya upinzani kwa wizara za Serikali zilizopo.
Mwandishi wetu alipomtafuta Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai (Chadema) kujua undani wa taarifa hizo, hakukana wala kukubali zaidi ya kueleza atafutwe baadaye, lakini hakupatikana tena.
Alipoulizwa kuhusu taarifa za mabadiliko hayo, katibu wa wabunge wa Chadema ambaye pia ni mbunge wa Momba, David Silinde alisema, “Ni kweli lakini atakayetangaza ni KUB (Kiongozi wa Upinzani Bungeni) ili kujua nani kaenda wapi na nani kabaki wapi.”
Katika mabadiliko hayo, inatazamiwa kuwa mbunge wa Kaliua (CUF), Magdalena Sakaya ambaye kwenye baraza la awali alikuwa waziri kivuli wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ataondolewa kwa kuwa yupo upande wa Profesa Lipumba na tayari alikwisha kutengwa ndani ya Ukawa.
Pia, mabadiliko hayo yanatokana na nafasi zingine kuwa wazi baada ya waliokuwa wakizishikilia mathalan, Dk Godwin Mollel kuhamia CCM na sasa ni mbunge wa chama tawala kutokea Siha.
Pia mabadiliko hayo yatatokana na CUF upande wa Profesa Lipumba kuwavua uanachama baadhi ya wabunge wa viti maalumu na hivyo kupoteza sifa za ubunge.
Kutokana na hali hiyo, Riziki Shahali aliyevuliwa ubunge na kambi hiyo na wenzake saba hawatakuwamo. Maftah Abdallah Nachuma (Mtwara Mjini) ambaye pia anatajwa kuwa upande wa Lipumba huenda pia akaachwa.
Baraza la sasa ambalo linatarajiwa kufanyiwa marekebisho na mawaziri pamoja na manaibu wao ni; Ofisi ya Rais, Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora (Jaffar Michael) na manaibu; Joseph Nkundi na Ruth Mollel.
Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira (Ally Saleh) na naibu wake, Pauline Gekul; Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Walemavu (Esther Bulaya) na manaibu; Yusuph Makame na Maftah Abdallah.
Pia, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi alikuwa Sakaya na Dk Emmaculate Sware; Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ni James Mbatia na naibu Willy Qambalo.
Nyingine ni Wizara ya Fedha na Mipango, Halima Mdee na naibu waziri, David Silinde huku Wizara ya Nishati na Madini akiwa John Mnyika na naibu wake John Heche.
Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu na naibu wake Abdalla Mtolela, Mambo ya Nje, Mchungaji Peter Msigwa na naibu wake, Riziki Shahali.
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Juma Omari na naibu ni Mwita Waitara; Wizara ya Mambo ya Ndani, Godbless Lema na naibu wake ni Masoud Abdalla.
Nyingine ni Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wilfred Lwakatare na naibu wake, Salum Mgoso; Wizara ya Maliasili na Utalii, Esther Matiko na naibu ni Cecilia Pareso.
Waziri kivuli wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Anthony Komu na naibu wake, Cecil Mwambe; Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Susan Lyimo na naibu wake ni Dk Ali Suleiman Yusuph; Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto alikuwa Dk Godwin Mollel ambaye alihamia CCM na naibu wake ni Zubeda Sakul.
Nyingine ni Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Joseph Mbilinyi maarufu ‘Sugu’ na naibu wake, Devotha Minja huku Wizara ya Maji na Umwagiliaji akiwa ni Hamidu Bobali na naibu akiwa Peter Lijualikali.
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako