A

A

MAGUFULI AKABIDHIWA RIPOTI, KIFUATACHO CCM NI KUSAFISHA SAFISHA NA KUIMARISHA CHAMA

Tume ya kuhakiki mali za Chama Cha Mapinduzi (CCM), iliyoundwa na Rais John Magufuli, imebaini madudu ukiwamo utapeli na usimamizi mbaya wa mali hizo.

Kamati hiyo iliyoundwa na Rais Magufuli kukagua mali za chama hicho, imefanya kazi hiyo kwa miezi mitano ambapo imekusanya taarifa, kuhakiki na kuchambua taarifa na nyaraka zenye maelezo kuhusu idadi, aina na hali ya mali zinazomilikiwa na kusimamiwa na chama hicho.

Akikabidhi ripoti hiyo kwa Rais John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Dk. Bashiru Ally, amesema tume yake pia ilibaini usimamizi mbovu wa mali za chama.

Akielezea namna tume hiyo ilivyofanya kazi, Dk. Bashiru amesema pamoja na mambo mengine, tume iliangalia vyanzo vya udhaifu wa mifumo na taratibu za usimamizi wa mali, imekusanya ushauri mbalimbali na kutoa mapendekezo ya mikakati na ushauri wa kusimamia mali za chama.

Katika ripoti hiyo, Dk. Bashiru ameeleza tume imebaini uwepo wa upotevu mkubwa wa mali za chama uliosababishwa na mikataba mibovu, ubadhirifu, wizi, usimamizi mbaya wa mali, utapeli na ukosefu wa maadili katika uendeshaji wa miradi ya chama.

“Uhakiki huo umefanyika kwa kutembelea maeneo yenye mali za chama, kuwahoji watu mbalimbali wakiwamo viongozi waliohusishwa na mali zilizokuwa zikihakikiwa, upitiaji wa nyaraka na kufuatilia uhalisia katika ofisi za mamlaka husika, kufanya uchambuzi wa taarifa na kutoa mapendekezo,” amesema.

Kwa upande wake Rais Magufuli ameipongeza tume hiyo kwa kazi kubwa iliyoifanya na amesema ripoti hiyo itawasilishwa katika vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM kwa ajili ya kufanyiwa uamuzi.


“Nilipokuwa nateua tume hii, nilikuwa najua ugumu wa kazi, nilikuwa najua kuwa mtapata shida kwenda kuwahoji watu licha ya kwamba niliwapa uhuru wa kumhoji mtu yeyote na mmefanya kazi nzuri sana, kilichobaki sasa ni kuifanyia kazi” amesema Rais Magufuli.

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako