Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman akipiga kura leo kwenye ukumbi wa Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma kupitisha Sura na Ibara za Rasimu ya Katiba inayopendekezwa. |
Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Yahya Kassim Issa akiomba mwongozo leo Bungeni kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel Sitta kuhusu kitendo cha Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman kuja kupiga kura na kukataa baadhi ya Ibara za Rasimu ya Katiba inayopendekezwa wakati alijitoa kwenye Kamati ya Uandishi ambapo alitakiwa awepo akitetea maslahi ya Zanzibar, jambo ambalo limewachanganya baadhi ya wajumbe. |
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
BUNGE MAALUM
Fax No. +255 026 2323116
Barua pepe: info@bungemaalum.go.tz
Ofisi ya Bunge Maalum,
S.L.P. 901,
DODOMA.
14 Julai, 2014
UKWELI KUHUSU AG WA ZANZIBAR MHE. OTHMAN MASOUD OTHMAN KUAMBATANA NA ULINZI KATIKA MAENEO YA BUNGE MAALUM.
Kumekuwa na Taarifa potofu zinazosambazwa na baadhi ya watu katika mitandao ya kijamii ya kuwa “Mwanasheria Mkuu Zanzibar Othman Masoud Othman amekamatwa baada ya kupiga kura ya hapana Bungeni leo”
Tunapenda kuutarifu Umma wa Watanzania kuwa, taarifa hizo sio sahihi na ni porojo zenye kutaka kuleta hisia potofu kwa wananchi kuhusu kiongozi huyo.
Ukweli wa Jambo hili ni kuwa Mhe. Othman Masoud Othman ametekeleza haki yake ya
Kidemokrasia ya kupigia kura Rasimu ya Katiba inayopendekeza katika Bunge Maalum leo. Ambapo katika kura alizopiga, ameweza kuzikubali baadhi Ibara na kuzikataa ibara nyingine katika rasimu ya Katiba inayopendekezwa.
Pengine hatua hiyo ya kuzikataa baadhi ya Ibara, haikuwafurahisha baadhi ya Wajumbe na hivyo kuleta majibishano ndani ya Bunge Maalum wakilalamikia uamuzi wake huo.
Kutokana na hofu hiyo ya baadhi ya Wajumbe kuanza kupinga uamuzi wake huo ndani ya Bunge, Ofisi ya Bunge Maalum kama ilivyokawaida kwa kila mjumbe, imeweza kumpatia Ulinzi Maalum wakati akitoka Bungeni hadi alipoondoka katika viwanja vya Bunge ili asiweze kubugudhiwa kwa namna yoyote ile kutokana na uamuzi wake huo.
Suala hili limechukuliwa kipropaganda na kuanza kueneza uongo katika mitandao ya kijamii kuwa Mhe. Othman amekamatwa baada ya kupiga kura ya hapana.
Tunapenda kuwahakikishia Watanzania wote kuwa Mhe. Othman hajakamatwa bali alipewa ulinzi katika Maeneo ya Bunge Maalum jambo ambalo hufanyika kwa kila mjumbe ambaye kwa namna moja ama nyingine itaonekana kuna dalili za kubugudhiwa katika Maeneo ya Bunge kutokana na uamuzi au kitendo alichofanya. Na kutokana na hali ilivyo, ulinzi wake umeimarishwa pia mahali alipo kwa hivi sasa mpaka atakapomaliza kazi yake hapa Dodoma.
Kanuni za Bunge Maalum zimempa madaraka Katibu wa Bunge Maalum kusimamia masuala yote ya Ulinzi na Usalama kwa Wajumbe na Maeneo yote ya Bunge Maalum.
Imetolewa na Idara ya Habari
Ofisi ya Bunge Maalum
Dodoma
1 Oktoba, 2014
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman akisindikizwa kutoka ndani ya ukumbi wa Bunge Maalum leo mjini Dodoma na Askari Polisi.
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman (mwenye Kaunda
suti ya kijivu) akisindikizwa kutoka nje ya viwanja vya Bunge Maalum la
Katiba leo mjini Dodoma na Askari Polisi mara baada ya kushutumiwa na
baadhi ya Wajumbe wa Zanzibar.
- Picha zote: Benedict Liwenga/Tanzania Government Blog, Dodoma
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako