A

A

Nape Nnauye katika ziara ya kutoa mafunzo kwa viongozi wa CCM Uingereza

Nape Nnauye katika ziara ya kutoa mafunzo kwa viongozi wa CCM Uingereza

  • Ahimiza CCM UINGEREZA iwe chachu ya mabadiliko ya kiutendaji na kuleta fikra mpya na mbadala nyumbani kwa watanzania kujikomboa kiuchumi.
  • Asema Chama kinaendelea na juhudi za kutatua kero na matatizo ya wananchi; wafanyakazi, Vijana na Wakulima na kuigusa jamii moja kwa moja.
  • Aunga Mkono CCM UINGEREZA Kufanya juhudi za kufufua Jumuiya ya Watanzania.
  • Ampongeza Mwenyekiti mpya CCM UK Kwa kuchaguliwa kwake na kwamba wana Imani na uongozi Mpya.
Katibu wa NEC; Itikadi na Uenezi CCM TAIFA Ndugu Nape Nnauye akifurahia jambo na Mwenyekiti Mpya CCM – UINGEREZA Ndugu Kapinga Kangoma mwenye kofia, kushoto ni Makamu Mwenyekiti CCM - UINGEREZA Ndugu Sukwa Said Sukwa kulia kabisa ni Kaimu Katibu CCM - UINGEREZA Ndugu Leybab Mdegela, Katika semina ya mafunzo jijini London.

Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM TAIFA Ndugu Nape Nnauye amezungumza na kutoa mafunzo kwa Viongozi wa chama cha mapinduzi Tawi la Uingereza Jumamosi tarehe 06.09.2014 katika ziara yake nchini humo iliyokuwa maalum kwa ajili hiyo. Pia Ndugu Nape amempongeza Mwenyekiti Mpya kwa kuchaguliwa kwake na kushukuru kuona uchaguzi ulifanyika salama na akatoa salamu toka kwa KATIBU MKUU TAIFA Ndugu Abdulrahaman Kinana na kuwa CCM TAIFA wana Imani na uongozi mpya hapa Uingereza na wako tayari kuwapa ushirikiano unaostahili.

Akimkaribisha kuzungumza na Viongozi wa Tawi na
Mashina CCM UK; Mwenyekiti Mpya wa CCM UK Ndugu Kapinga Kangoma alimshukuru Ndugu Nape kwa moyo aliounyesha wa kujitoa ili kuimarisha chama hapa UK kwa manufaa ya wana CCM na Watanzania Ughaibuni kwa ujumla na kuahidi kuendelea kufikia watanzania wengi Zaidi hapa UK kujiunga na chama na pia kufufua Jumuiya ya Watanzania hapa Uingereza ambayo itaweza kutuunganisha kwa pamoja kama Watanzania na kuwa chachu ya mabadiliko yenye mawazo mapya kwa chama na serikali.

Awali Katibu Itikadi na Uenezi CCM UK Ndugu Abraham Sangiwa aliwachangamsha Viongozi hao kwa salamu ya Mshikamano na Mnato ambayo CCM UK Huitumia katika kuimarisha umoja wao na moja kwa moja kumpa Ndugu Nape chamgamoto zinazowakabili katika Tawi kwa upande wa mawasiliano kati ya Tawi na makao makuu na namna ya kujiendesha kuwa kikwazo huku michango, dira na mawazo yenye manufaa kwa chama na watanzania kwa ujumla yakishia kwenye makaratasi bila kupata majibu au ushirikiano wa karibu katika kupeana mawazo tofauti na mapya, Hapa Uingereza tuna wana CCM na watanzania wengi wenye ujuzi katika Nyanja mbalimbali waliopata uzoefu wa kamataifa na hasa katika nchi hizi za magharibi hivyo wanaweza kuwa msaada mkubwa katika kuleta mabadiliko ya uwajibikaji na uendeshaji katika sekta tofauti ili kumkwamua Mtanzania kiuchumi na kuleta maendeleo.

Katika Mafunzo hayo Ndugu Nape alianza kwa kutoa ufafanuzi kuhusu historia na wajibu wa uwepo wa matawi ya CCM nje ya nchi. Ndugu Nape aliwakumbusha Viongozi wa CCM UK kuwa matawi hayo yalikuwapo tangu kipindi cha TANU mpaka kuzaliwa kwa CCM mpaka mwaka 1992 ambapo yalifungwa baada ya kuanzishwa kwa vyama vingi jambo ambalo wamekuja kuliona halikuwa uamuzi sahihi kwani matawi haya pamoja na mengine katika taasisi mbalimbali kama vyuoni, mashuleni, maofisini nk ndiyo yalikuwa yakisaidia kuzalisha viongozi bora na chama kupata mawazo tofauti hivyo kuongeza ufanisi katika kutekeleza sera zake kwa manufaa ya wananchi.

Matawi haya yamerejeshwa ili kuweza kwenda na mahitaji ya wakati wa karne hii hivyo ni vyema kila mwenye mapenzi na chama cha mapinduzi popote alipo apate fursa ya kushiriki kikamilifu katika kuleta mabadiliko, kukosoa pale mnapoona mapungufu ndani ya chama panapobidi kufanya hivyo na kuwa chanzo cha kupata mawazo mapya kutokana na exposure wanayopata huko walipo yenye manufaa kwa mwananchi wa kawaida Tanzania kujikomboa kiuchumi jambo ambalo naona mmeanza kulifanya. Kupitia humu ndimo tutakapotoa wanachama wenye misimamo imara na hata kuwa tanuru la viongozi wa sasa na siyo baadaye kwa kuwaandaa na kuwapika waive kisiasa na Imani ya chama.

Ukombozi wa kupata uhuru umeshakamilika sasa ni wakati wa kupigana vita kujikomboa kiuchumi na kuondokana na Viongozi wabovu wanaoturudisha nyuma katika vita hii; walipa kodi wanaotakiwa kulipa kodi Tanzania ni milioni kumi nne lakini wanaolipa kodi ni milioni moja na nusu hivi tu hii si sawa hivyo kisaidieni chama chenu kiweze kuja na mifumo itakayoziba hii mianya ya kukwepa kodi, kuweka viwango vinavyolipika kwa kupanua wigo wa vyanzo vya mapato na pia kudhibiti matumizi ya mapato yanayopatikana. Kuhusu suala la misamaha ya kodi Ndugu Nape amesema ni wakati umefika sasa kwa kila mmoja anayewekeza au kunufaika na rasilimali za Tanzania kutoa mchango wake sawia.

Pambaneni kuwaumbua wala rushwa katika maeneo yanayowagusa kama kupitisha mizigo bandarini, viwanja vya ndege nk hili litakisaidia chama kuweka mikakati ya kupambana na tatizo hili kwa kupata mawazo mapya yanayowagusa wadau wa huduma hiyo wakiwemo wafanyabiashara.

Sisi ndiyo wenye duka hivyo kazi ya kusemea na kusimamia serikali na balozi zetu kutekeleza sera zetu za diplomasia na za kiuchumi sawasawa ni yetu wote hivyo badala ya kusubiri watu wengine watukosowe ni vyema mkatusaidia tukatambua utendaji wa balozi zetu kama unaendana na kile tunachokusudia wakifanye na kama sivyo basi tumuulize aliyewateuwa kulikoni kuhusu viongozi hawa! Tusikubali kuhujumiwa kwani tutakaokuja kupata mshikemshike ni sisi wenye duka na si muuzaji tuliyemuweka na wananchi watakiadhibu chama chako! Hivyo tunaomba matawi haya ya nje yatusaidie kafanya kazi hii ya kuangalia mienendo ya balozi zetu!! Na kutushauri.

Akijibu swali toka idara ya itikadi na uenezi CCM UK Kama lilivyodokezewa na Katibu wa Idara hiyo nchini Uingereza Ndugu Abraham Sangiwa kuhusu miundombinu ya mawasiliano na mfumo wa kujiendesha na kupeana taarifa; Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM TAIFA Ndugu Nape Nnauye alikubali kuwa hiyo ni changamoto kwani mfumo uliopo sasa si rafiki na unahitaji marekebisho yatakayoleta uwajibikaji na namna ya kuyaendesha matawi ya nje. Ndugu Nape aliendelea kuelezea kuhusu changamoto nyingine ikiwemo mitazamo hasi na mingine isiyokuwa ya kweli kuhusu matawi haya nje ya nchi hivyo elimu inahitajika kuwaellimisha wanachama kuhusu matawi yetu ya nje.

Changamoto nyingine ni matumaini yasiyo sahihi na makubwa kuliko hali halisi toka kwa baadhi ya matawi ya nje hivyo kujikuta wanachama na viongozi wakiishia kulaumu zaidi kuliko kujenga hoja zenye mashiko na manufaa kwao, wanachama na watanzania kwa ujumla, upendeleo mnaoupata kutokana na exposure na elimu zenu utumieni vizuri na mjione ni sawa na wanachama wengine wa chama chetu nyumbani na popote pale duniani.

Upungufu wa mafunzo kwa makada na wanachama nje ya nchi ni tatizo kubwa ambalo itabidi idara yangu kwa kushirikiana na uongozi wa tawi na Ndugu Sangiwa wa idara yenu ya uenezi CCM UK tupange namna ya kufanya mafunzo na kanuni ya namna kujiendesha kwa kutumia mtandao Zaidi na kubuni miundombinu itakayosaidia uendeshaji wa matawi haya.

Kutokana na uzoefu wa tawi la CCM UK ambalo ndilo tawi la kwanza kuundwa tena nje ya nchi miaka saba sasa ni muda mrefu hivyo mnajua matatizo mnayokabiliana nayo tuleteeni mapendekezo ya kanuni na taratibu ambazo mnadhani zikitekelezwa zitasaidia kwa kiwango kikubwa namna ya kujiendesha na kuwa sehemu ya mabadiliko chanya ambayo chama chenu kinayahitaji sana.

Kuhusu uwajibikaji wa viongozi wa serikali katika kutekeleza sera za chama; tumeamua kuwa wakali na kuwawajibisha mawaziri na viongozi mizigo wa ngazi mbalimbali kutokana na tuhuma za rushwa na utendaji mbovu ama wa moja kwa moja au wasaidizi wake kushindwa kusimamia kikamilifu majukumu yake ya kiuongozi aliyopewa; hivyo nanyi msisite kusemea pale mnapoona kiongozi tuliyempa dhamana anahujumu sera za chama chetu. Tukibeba mizoga nzi hawataisha kutufuata hivyo ni wakati wa kutupa mizoga pembeni na ili tuweze kusonga mbele hivyo ni vyema kuendelea kuchora mstari kati ya mafisadi na chama chetu hivyo Kiongozi yeyote mwenye uchafu huu tusijihusishe naye katika shughuli za chama chetu na mstari huu sasa unafanya kazi. Hatuwezi kuendelea kubeba viongozi wanaotoboa toboa boti letu majini tunawatosa wazame wenyewe chama kinasonga mbele kikiwa safi.

Kuhusu wagombea Urais kutangaza nia Ndugu Nape amesema kutangaza nia nia sahihi ila kuanza kampeni za kuungwa mkono kabla ya wakati wake ni kinyume na taratibu za chama na hakuna kiongozi au mwanachama aliye juu Zaidi ya chama chenyewe hivyo kiongozi yeyote anayedhani ana umaarufu kupita chama anajidanganya. Chama huandaa sera na ilani kisha hutafuta mgombea mwenye sifa na vigezo ambavyo tumeviweka pia mwenye uwezo na afya njema kuweza kuhimili vishindo katika kutekeleza sera za chama chetu na si vinginevyo.

Viongozi wenye kutamani sana kwenda ikulu na kugawa pesa makanisani na misikitini mlango wa nyuma kwa visingizio vya harambee, wanakigawa chama hivyo ni vyema wakadhibitiwa kuweka nidhamu ndani ya chama na chama kujitenga na vitendo vyao.

Watanzania wanahitaji mabadiliko wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM hivyo hatutakubali kusimamisha mgombea mwenye harufu ya rushwa au utajiri usio na maelezo ya kujitosheleza aliupataje au mwenye historia chafu yenye konakona za kuunga unga na kashfa za ufisadi.

Akijibu swali toka kwa mjumbe shina Reading Bi. Francia Chengula ambaye aliuliza ni kwa nini watanzania walioko nje hawaruhisiwi kupiga kura huko walipo na vyema suala hili likaingia kwenye katiba pamoja na suala zima la Uraia Pacha. Akijibu swali hilo Ndugu Nape alisema suala la Uraia pacha limepotoshwa hivyo wanadiaspora mna wajibu wa kulisemea kiundani ili wananchi na viongozi wetu waone umuhimu wake, kuhusu watanzania nje ya kushiriki katika chaguzi Ndugu alisema hilo linawezekana isipokuwa ni suala ambalo linahitaji utafiti na utaratibu ambao hautaleta mgawanyiko wa Taifa letu.

Pia michango mbalimbali ilitolewa na Viongozi wa CCM UK katika kukabiliana na kuboresha huduma na uwajibikaji katika sekta mbalimbali kuanzia na afya, sheria za usalama barabarani ili kupunguza wimbi la ajali nchini, namna ya kuboresha kilimo na uvuvi wenye soko la uhakika, mikataba ya kimataifa yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wanachi kwa kushirikisha watanzania wasomi wanaoishi nchi hizi za magharibi wenye uzoefu na exposure ya ku-deal na mataifa ya magharibi na kwingineko ili kupata mikataba bora.

Semina hii pia ilihusisha mambo mengine ya kichama yenye manufaa ya kukinufaisha na kukijenga chama kuwa imara zaidi

IMETOLEWA NA ABRAHAM SANGIWA – KATIBU IDARA YA ITIKADI NA UENEZI CHAMA CHA MAPINDUZI TAWI LA UINGEREZA

10.09.2014



Nape akiteta jambo katika mafunzo yaliyofanyika jijini London hivi karibuni kwa Viongozi wa Chama cha Mapinduzi Nchini Uingereza.



Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM – Uingereza Ndugu Abraham Sangiwa akitoa yake machache katika mafunzo yaliyofanyika London nchini Uingeeza.



Nape akiendelea kupiga Darasa



Viongozi wa Tawi na mashina katika picha ya pamoja mgeni rasmi Ndugu Nape Nnauye.





Nape Nnauye katikati, kulia ni Ndugu Hussein Chan”ga toka Reading na Sukwa Said Sukwa Makamu Mwenyekiti CCM UK toka Northampton.



Waenezi Katika Picha ya Pamoja – Katibu wa NEC; Itikadi na Uenezi CCM TAIFA Nape Nnauye na Katibu Itikadi na Uenezi Chama cha Mapinduzi nchini Uingereza Ndugu Abraham Sangiwa.



Londoners na Nape Nnauye.



Viongozi Tawi na mashina ya CCM - UINGEREZA wakisikiliza kwa makini Mafunzo toka kwa Katibu wa NEC; CCM TAIFA ITIKADI NA UENEZI NDUGU NAPE NNAUYE jijini LONDON.

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako