HOSPITALI ya Chuo cha Kimataifa cha
Matibabu na Teknolojia (IMTU)
kinachohusishwa na utupaji wa viungo vya
binadamu mithili ya takataka, Imefungiwa kwa muda usiojulikana baada ya
kugundulika kutokidhi viwango na maadili ya utoaji huduma za hospitali nchini.
Manispaa ya Kinondoni kwa kushirikiana na
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imechukua jukumu la kuifungia hospitali hiyo
baada ya kufanya ukaguzi wa kushitukiza na kubaini uwepo wa mapungufu kadhaa.
Mapungufu yaliyobainika kuwepo katika
hospitali hiyo ni pamoja na kutokuwa na wauguzi wa kutosha, kutokuwa na vifaa
vya kutosha ikiwemo kifaa cha kuchomea taka ngumu, kuchanganya dawa
zilizokwisha muda na ambazo hazijaisha muda wake na pia wauguzi kufanya kazi
ambazo si za kwao.
Akizungumza wakati wa kufunga hospitali
hiyo, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Dk Gunini Kamba alisema, hospitali hiyo
inastahili kufungiwa kutokana na kutokidhi viwango hivyo.
“Baada ya kufanya ukaguzi wa kushitukiza
tumebaini kuwepo kwa mapungufu haya, kwa hiyo tunaifungia hospitali hii mpaka
pale watakaporekebisha,” alisema Dk Kamba.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa
hospitali hiyo, Profesa Yassin Mgonda alikiri kuwepo kwa mapungufu hayo ambayo aliahidi
kuyafanyia kazi. Hata hivyo, Profesa Mgonda aliiomba Manispaa na Wizara ya Afya
kuangalia adhabu hiyo waliyoitoa.
Baadhi ya wagonjwa waliokuwa hospitalini
hapo wakipata huduma walishtushwa na kusikitishwa na kitendo hicho, lakini walikipongeza
na kutaka kuwa endelevu.
Mmoja kati ya wagonjwa hao
aliyejitambulisha kwa jina la Neema Kiwalo alisema, ukaguzi huo unatakiwa kuwa
endelevu ili kuendelea kufichua madudu yaliyopo katika hospitali mbalimbali
nchini.
Aidha, Msemaji Mkuu wa Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja alisema, endapo hospitali hiyo watatimiza masharti
waliyopewa na Mganga Mkuu wa Manispaa wao kama wizara watafanya ukaguzi kuona
kama wamekamilisha.
Alisema ikiwa watakuwa wamerekebisha
kasoro hizo zilizopelekea kufungiwa hospitali hiyo itaruhusiwa kutoa huduma
zake kama kawaida.
Hospitali hiyo imefungiwa wakati kukiwa
kuna sakata linalolihusisha chuo chake, kinachodaiwa kutupa viungo vya binadamu
jalalani.
Katika sakata hilo lililovuta hisia za
watu na kuzua mjadala mitaani, katika vyombo vya habari na kwenye mitandao ya
kijamii, watu wanane wakiwemo madaktari wa IMTU, walikamatwa na Polisi kwa mahojiano
wakituhumiwa kuhusika katika utupaji viungo vya binadamu jalalani.
Serikali wakati ikiendelea kuchunguza
tukio hilo ikiwemo kuunda tume nyingine ya watu 15 chini ya Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii, kujiridhisha kabla ya hatua kuchukuliwa iliyopewa siku saba
kukamilisha kazi yake, tume hiyo imeundwa kukiwa na tume nyingine iliyoundwa na
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Tume iliyoundwa na Kamanda wa Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imejielekeza kuja na majibu kadhaa, ikiwa ni pamoja
na kufahamu idadi kamili ya watu wenye viungo hivyo.
Ikiwa na watu saba akiwemo Mkemia Mkuu wa
Serikali, Tume hiyo itakuja na majibu yanayofafanua viungo hivyo ni vya muda
gani na zilitumika kemikali gani kuvikausha. Pia, jopo hilo litabaini kama ipo
sheria na ni ipi inavunjwa.
Wataalamu hao wanalenga kubaini, pia kama
upo uzembe katika kulinda viungo vya binadamu na vinapatikanaje kwa ajili ya mazoezi.
Kwa mujibu wa Polisi, mifuko ipatayo 85 yenye vichwa, miguu, mikono, moyo, mapafu, vifua na mifupa ya aina mbalimbali ya binadamu, ilikutwa maeneo ya bonde la Mbweni Mpiji eneo la Bunju jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako