Ikiwa kata ya Tandala wilayani Makete mkoani Njombe ni
miongoni mwa maeneo yanayosubiriwa kwa hamu kuwa na umeme wa gridi ya
taifa, hivi karibuni wananchi wa kata hiyo wamembana mbunge wao
aliyekuwa akipita eneo hilo na kumlalamikia kuhusu kutowaka kwa umeme.
Tukio
hili limejiri hivi karibuni ambapo mbunge wa jimbo la Makete ambaye pia
ni Waziri wa nchi ofisi ya makamu wa raisi anayeshughulikia mazingira
Dkt Binilith Mahenge alikuwa akipita akitokea Dodoma kwa ajili ya
kukabidhi sola katika shule ya sekondari Ikuwo, alikumbana na dhahama
hiyo ambapo wananchi walisimamisha gari lake na kumtaka kuwasaidia kujua
kulikoni umeme bado hauwaki katika kata hiyo licha ya nguzo na kila
kitu kuwa tayari
"Mheshimiwa
sisi tunashangaa mpaka sasa hakuna dalili za umeme kuwaka, nguzo
zimefika kama unavyoona lakini umeme hauwaki, kila siku tunaambiwa mara
tujiandikishe, mara vifaa havijaja, mara tusubiri kwanza na hela
tushalipa, sasa tunajiuliza kwa nini mliharakisha kuleta umeme toka
makete wilayani mpaka hapa kama mlikuwa hamna haraka ya kutuwashia?"
alisikika Mwananchi mmoja akisema
Dkt.
Mahenge amewatuliza wananchi hao kwa kuwaambia kuwa anasikitishwa na
hali hiyo, huku akiwahakikishia kuwa umeme huo utawaka mara moja kama
serikali ilivyokusudia
"Ndugu
zangu wananchi naomba niwahakikishie mimi ni mbunge wenu, mmenituma
kuwatumikia, nawahakikishia hili jambo litakwisha, nalikomalia hadi
mwisho maana si lengo la serikali kuwa ninyi mpate tabu, umeme utawaka"
amesema Dkt Mahenge
Kufuatia
hali hiyo Waziri Mahenge amelazimika kuwasiliana na ofisi ya Tanesco
wilaya ya Makete kujua sababu za wao kutowasha umeme katika kata ya
Tandala ambapo alijibiwa na Meneja wa shirika hilo wilaya Bw. Zebedayo
Gadau kuwa wananchi hawajachangia fedha kwa ajili ya wao kuunganishiwa
umeme (Tsh. 175,000/=) na ndiyo maana wapo kimya
Bw.
Gadau amesema umeme upo na transfoma zilizopo katani hapo zina umeme na
kilichobaki ni kuunganisha kwenda kwa wananchi na hawawezi kufanya
hivyo kama wananchi hawajalipia
Hali
hiyo ilimfanya Dkt Mahenge kuomba kukutana na wananchi wa Tandala,
Meneja Tanesco wilaya pamoja na yeye ili kujua utata uko wapi kwa kuwa
maelezo ya meneja na wananchi hao yalikuwa tofauti ambapo ilibainika
kuwepo kwa uzembe fulani katika ofisi ya Tanesco makete
Katika
kikao hicho wananchi wamedai kuwa waliambiwa na Tanesco wafanye "wire
ring" kwenye nyumba zao na shirika hilo lingekuja kukagua kabla ya
kuwaunganishia umeme jambo ambalo walilifanya lakini baadaye waliwaambia
wasilipe gharama za kuunganishiwa umeme kwanza mpaka watakapotaarifiwa
"Hilo
halijafanyika mheshimiwa mbunge, mpaka sasa tunasubiri, sasa nashangaa
tunavyoambiwa hatujalipia, je tutalipiaje ilihali tuliambiwa na tanesco
tusubiri mapaka waje kutuambia, na hadi leo hii wapo kimya?" amesema
mwananchi
Kikao
hicho kilimuamuru meneja huyo kuwaruhusu wananchi waje kulipia gharama
za kuunganishiwa umeme ambapo agizo hilo lilipokelewa kwa furaha na
wananchi hao
Hadi sasa wananchi wanaendelea kumiminika kwenye ofisi za Tanesco wilaya kulipia gharama hizo