Ulinzi kaitka eneo la baa palikotokea mlipuko (picha: Arusha255 blog) |
Jana Jumapili, Aprili 13, 2014 ulitokea mlipuko wa kinachodhaniwa kuwa bomu la kurushwa kwa mkono katika baa maarufu kwa maonesho ya mechi za mpira wa miguu wa Ulaya, ijulikananyo kama Arusha Night Park au Matako baa iliyopo maeneo ya Mianzini, mkoani Arusha na kujeruhi zaidi ya watu 20 wengi wao wakiwa wateja waliojazana kushuhudia mechi za soka.
Majeruhi walikimbizwa hospitali za Mt Meru na Dr Mohamed kwa matibabu ya haraka, na hakuna taarifa rasmi ya mtu aliyepoteza maisha ingawa baadhi ya walionusurika wanashuhudia kuwepo watu waliokatika miguu.
Taarifa ya awali kutoka Jeshi la Polisi inaeleza kuwa bomu hilo ni la kutengenezwa kienyeji baada ya kukuta vipande vya vyuma na misumari eneo la mlipuko. Aidha taarifa zaidi zinaeleza kuwa bomu hilo lilirushwa na mtu anayeendelea kusakwa na Jeshi la Polisi likiwa kwenye mfuko wa plastiki kuelekea katikati ya mashabiki hao.