Wanafunzi wa Kidato cha Nne, watafanya mitihani miwili ya Taifa mwaka
huu, baada ya kuongezwa mtihani wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), ambao
utatumika kuwapima walivyojiandaa na Mtihani wa Taifa wa Kumaliza Elimu
ya Sekondari.
Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari, Paulina Mkonongo,
alitangaza utaratibu huo jana na kufafanua kwamba lengo ni kubaini
wanaohitaji msaada kabla ya mtihani wa mwisho, ili kuboresha taaluma
darasani.
Kwa mujibu wa Paulina, mtihani huo wa BRN, utafanyika kwa
masomo machache lakini yanayosomwa na wanafunzi wote ambayo ni
Baiolojia, Hisabati, Kiswahili na Kiingereza.
Paulina alisema mtihani
huo wa majaribio, tayari umeanza kuandaliwa na utasambazwa kwa maofisa
Elimu nchini ifikapo Mei 10 mwaka huu, na barua kuhusu kufanyika kwa
mtihani huo imeshatumwa kwa makatibu tawala wote, ili kuanza maandalizi.
Matokeo
ya mtihani huo, yanatarajiwa kutumika kubaini mada ngumu kwa
wanafunzi, wanaohitaji msaada na kuwapa walimu mwanga kuhusu wapi
wanafunzi hao wanahitaji msaada na lengo ni kuongeza ufaulu kwa
wanafunzi.
Tayari tangu mwaka jana mikoa 12 ilianza kushiriki katika
programu iliyohusisha mafunzo kwa walimu 4,064 wa masomo husika, na
mikoa 13 iliyosalia itashiriki programu hiyo mwaka huu.
Mafunzo ya
walimu wa mikoa hiyo 13 kwa mujibu wa Paulina, yatafanyika Juni 2014 na
programu ya mafunzo rekebishi kwa wanafunzi wenye upungufu, itaanza
Julai mwaka huu kulingana na matokeo ya mtihani watakaofanya.
“Tutatoa
mtihani wa majaribio kwa wanafunzi wa kidato cha nne, ili kubaini
maeneo yenye wanafunzi wanaohitaji msaada zaidi na kutoa utaratibu wa
mafunzo rekebishi na mafunzo kazini, ili kuwajengea uwezo walimu wa
kuwasaidia wanafunzi walioko kwenye hatari ya kutofanya vema,” alisema
Paulina.
Hata hivyo, Paulina alisema katika utekelezaji utoaji wa
mtihani huo, wanakabiliwa na changamoto ya kuwapatia mafunzo wakuu wa
shule zisizo za serikali, kuchapisha kitabu cha mwongozo na ziara za
wasimamizi wa elimu katika ngazi mbalimbali kutoa ushauri.
Tayari
walimu wakuu 3,001 wa shule za Serikali wamepatiwa mafunzo na Taasisi ya
Uongozi wa Elimu Bagamoyo (ADEM) katika maeneo yaliyoainishwa, huku
kitabu hicho cha mwongozo kikiwekwa kwenye tovuti ya Wizara.
Paulina
alisema mikakati endelevu iliyopo, inalenga kuendeleza mafunzo ya walimu
kazini, ili kuwajengea uwezo kulingana na wakati na mahitaji ya
mitaala.
Mbali na mafunzo hayo, pia wanalenga kuwajengea walimu tabia
ya kutunga mitihani bora ya kupima mchakato wa ufundishaji, kubaini
wanafunzi wanaohitaji kusaidiwa zaidi, kubaini mada ngumu na kutoa
mafunzo rekebishi kwa wanafunzi.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la
Mitihani Tanzania (NECTA), Dk Charles Msonde, alisema vitabu rekebishi
vitaonesha wanafunzi waliofanya vizuri katika kila swali, waliojibu
vibaya na swali lilikuwa likitaka nini.
Vitabu hivyo vitasaidia
walimu na wanafunzi kubaini makosa mbalimbali yanayofanywa na watahiniwa
wakati wa kujibu maswali na kutumia mbinu bora za kujibu maswali.
“Mwisho
wa vitabu hivyo, kuna mada zilizofanywa vizuri na vibaya na jinsi ya
kusaidia walimu wahakikishe wanafunzi wanafaulu mada hizo,” alisema.
Vitabu
hivyo kwa shule za msingi vimetolewa vya masomo ya Kiswahili, Hisabati,
Kiingereza, Sayansi na Maarifa ya Jamii kwa ajili ya mtihani wa
kumaliza elimu ya msingi mwaka 2012 na 2013.
Kwa sekondari,
vimetolewa kwa masomo ya Hisabati, Uraia, Historia, Jiografia,
Kiswahili, Kiingereza, Baiolojia, Kemia na Fizikia kwa mwaka huo.
Dk
Msonde alisema Baraza pia limepewa jukumu la kupanga shule katika
makundi ya ubora wa ufaulu, ili kuongeza kiwango cha ufaulu katika shule
za msingi na sekondari, na kuwajengea walimu na wanafunzi hali ya
ushindani na kujitambua kama shule imepanda au imeshuka.
Makundi ya
ufaulu yatapangwa kwa kutumia rangi za kijani kwa shule zenye ufaulu wa
juu, njano kwa zenye ufaulu wa kati na nyekundu kwa shule zenye ufaulu
wa chini kwa shule za msingi na sekondari.