PIPI 60
za madawa ya kulevya aina ya heroine yanayokadiriwa kuwa na thamani ya
shilingi milioni 60 yanadaiwa kukamatwa ndani ya Gereza la Keko jijni
Dar es Salaam baada ya mtu mmoja kuingia nayo akiwa ameyameza.
Kwa
mujibu wa chanzo, mtu mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Mashujaa Udugu
Matata, aliingia gerezani humo Machi 21, mwaka huu akitokea kusomewa
shitaka la kukutwa na madawa ya kulevya katika Mahakama ya Kisutu jijini
Dar es Salaam.
Inadaiwa
Matata alikamatwa na polisi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere, Machi 17, mwaka huu, saa 8.25 usiku akitokea nchini
Brazil.
Baada
ya kukamatwa alitoa pipi 102 za madawa hayo. Alipofikishwa gerezani
hapo, inasemekana mtuhumiwa huyo hakuwa na hali nzuri kiafya, jambo
lililofanya awekwe chumba cha mahabusu wagonjwa ili aweze kufuatiliwa
kwa karibu na madaktari.
“Kesho
yake asubuhi kuna mfungwa alikwenda kufanya usafi katika chumba hicho,
wakati anachukua takataka, akaitwa na Matata na kumuomba achukue mzigo
uliofungwa kwenye karatasi ambao ulikuwa unanuka kinyesi, akamweleza
ampelekee mahabusu mwenzake anayeitwa Abbas Gede,” kilisema chanzo
chetu.
Inasemekana Gede ni rafiki wa Matata ambaye naye ana kesi ya ‘unga’ na kwamba awali waliwahi kuishi pamoja Brazil.
Kutokana
na sheria kutoruhusu mfungwa kuonana na mahabusu, alilazimika kumpatia
mahabusu mwingine ili aufikishe mzigo huo, lakini badala ya kuufikisha,
mahabusu huyo aliambiwa na rafiki zake kuwa unga huo ni wa mamilioni ya
shilingi, hivyo asubiri awape ndugu zake wakija kumpelekea chakula.
Hata
hivyo, akiwa katika harakati za kutaka kuwapa ndugu zake, askari wa
magereza walimkamata na alipoulizwa alikoyatoa, alimtaja Matata na hivyo
kufanikisha kukamatwa kwa wote waliohusika na mzigo huo.
Mkuu
wa gereza hilo, Sena Shida amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na
kusema kuwa watu wote waliohusika wataadhibiwa. “Kwa upande wake, Matata
ataadhibiwa mara atakapopata nafuu kulingana na sheria ya mwaka 1967,
huo unga tumeuchoma moto,” alisema Shida.
Naye
Kamanda wa Kikosi cha Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulevya
Tanzania, SACP Godfrey Nzowa alipoulizwa alikiri kukamatwa kwa Matata na
kwamba alitoa pipi 102.
Awali
walijua kuwa zimeisha hata hivyo, Nzowa alisema alimwagiza mkuu huyo
kuyapeleka madawa hayo ofisini kwake, akashangaa kusikia yalichomwa.
Aidha, alisema aliwasiliana na mkuu huyo wa gareza ambaye alikiri
kutokea kwa tukio hilo ingawa hakuweza kutoa ripoti kituo cha polisi
kama ilivyo taratibu.
Taarifa
zilizopatikana ndani ya jeshi la polisi zinadai kuwa, Matata aliwahi
kukamatwa mwala 2007 kwa tuhuma ya kusafirisha madawa ya kulevya na
kufikishwa mahakamani na alikuwa chini ya uangalizi wa jeshi hilo na
wakati huo alikuwa hajabadili jina, aliitwa Abdallah Mauri Kaikai.
Kamishina
Mkuu wa Jeshi la Magereza Tanzania, John Minja aliwahi kuufumua uongozi
wa Gereza la Keko kutokana na tuhuma za kuwepo biashara ya madawa ya
kulevya ndani ya gereza hilo.