Tendega akizungumza na wanahabari
Akizungumza na wanahabari nje ya iliyokuwa kambi ya Chadema mjini Iringa ya CK Lodge, Tendega alianza kwa kumshukuru Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na viongozi wengine wote walioshiriki kampeni za chama hicho.
Huku baadhi ya wafuasi wa chama hicho wakiangua kilio alisema; “Ninawashukuru makamanda wenzangu na wanaharakati waliokuwa wanapigania haki Kalenga, wafuasi na wanachama wa Chadema wote, nawapa pole na hongera kwa kuanza na kumaliza uchaguzi huu uliokuwa na dosari nyingi,” alisema.
Alisema maapambano ya ukombozi yana changamoto nyingi na kwamba huo ni mwanzo wa safari ya mabadiliko makubwa nchini, pale walipokesea mbele ya safari watajipanga upya.
Benson Kigaila
Kigaila akisisitiza kuyakataa matokeo
Katika mkutano huo na wanahabaari, Mkurugenzi wa Oparesheni wa Chadema, Benson Kigaila alisema Chadema haiyakubali matokeo hayo japokuwa haitakakata rufaa mahakamani kuyapinga.
Alisema daftari la wapiga kura lililotumika katika uchaguzi huo sio la mwaka 2010 bali ni lile walilolilalamikia awali kufanyiwa marekebisho mwaka huu.
“Kuna wapiga kura wengi waliondolewa katika daftari hilo lakini wengine wengi wapya waliingizwa, tunao ushahidi tuliouwasilisha kwenye kikao tulichofanya na Tume ya Taifa ya Uchaguzi,” alisema.
Alisema “ni mwendawazimu pekee ndiye anayeweza kusema kwamba uchaguzi huu wa Kalenga ulikuwa huru na wa haki, vinginevyo haki ya watanzania inaendelea kuporwa kwa njia ya masunduku ya kura.”
Alisema yako mambo ya kisheria yaliyojitokeza wakati wa zoezi la upigaji kura ambayo watataka ufafanuzi wake kutoka kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa.
“Kuna gari na watu wetu hawajulikani walipo mpaka sasa, kuna wafuasi wetu walikamatwa wakapigwa na kuteswa baada ya kukamatwa na watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa CCM, tunataka kujua wahusika wamechukuliwa hatua gani kwasababu wanafahamika,” alisema.
Alisema yeye na baadhi yaa viongozi wa chama hicho hawataondoka mjini Iringa mpaka watakapopata majibu ya mambo wanayolalamikia.
Jimbo la Chalinze
Kigaila alisema wakimaliza kushughulikia changamoto zote zilizojitokeza wakati wa uchaguzi huo, mapambano yao watayaelekeza katika uchaguzi mdogo jimbo la Chalinze.
“Kule Chalinze kampeni zimekwishaanza; tukitoka Iringa breki yetu ni Chalinze; tutapita kijiji kwa kijiji kuwaeleza watanzania umuhimu wa kuichagua Chadema,” alisema.
Alisema katika kampeni hiyo wimbo wao mkubwa utakuwa ni fursa sawa kwa watanzania wote ili kuondokana na tabia inayojengekea ya watoto kurithi nafasi za uongozi za wazazi wao.
“Wote tuna haki sawa, Chadema tunataka kuona wakulima, walimu na watu wengine wa kawaida wanapata fursa katika nchi hii badala ya kuendelea kutoa madaraka kwa watoto wa wakubwa,” alisema