Huku hali ya taharuki ikiendelea
kutanda mjini Mombasa pwani ya Kenya ambapo magaidi walivamia kanisa
siku ya Jumapili na kuwapiga risasi waumini, mmoja wa waathiriwa wa
shambulizi hilo amefikishwa Nairobi mwa matibabu maalum.Shirika la madaktari la AMREF, limemleta Nairobi Mtoto Cyprian Osinya aliye na miezi kumi kutoka Mombasa kwa matibabu maalum ya upasuaji wa kichwa baada ya madaktari kugundua kuwa risasi imekwama katika ubongo wake.
Mamake aliyekuwa anamkinga kutoka kwa magaidi waliovamia kanisa hilo siku ya Jumapili ,alifariki kanisani humo baada ya kupigwa risasi. Inaarifiwa risasi aliyomuingia kichwani Cyprian ilitoka kifuani kwa mamake na kuishia katika ubongo wa mtoto huyo.
Mamake Cyprian, alikuwa miongoni mwa watu sita waliouawa katika shambulizi hilo, baada ya washukiwa watatu wa ugaidi kulivamia kanisa la Joy in Jesus katika mtaa wa Likoni na kuanza kuwafyatulia waumini risasi kiholela.
Cyprian atafanyiwa upasuaji maalum katika hospitali kuu ya Kenyatta mjini Nairobi.
BBC