Abdallah anayechukua shahada ya Mawasiliano ya Habari na Teknolojia
(ICT) aliibuka mshindi wa kuchora nembo hiyo ya Ukumbi wa Kimataifa wa
Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) kati ya washiriki 272.
“Ninaamini
kuwa katika shindano hili la kubuni nembo ya jengo hili la kimataifa
mimi nilikuwa wa mwisho kutuma kwani nilituma saa 1:45 usiku wa siku ya
deadline (siku ya mwisho),” anasema Abdallah.
Nikiwa mmoja wa waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa nembo hiyo ya
jengo hilo la kimataifa wiki mbili zilizopita uliofanywa na Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, nilipata nafasi
ya kuzungumza na kijana huyo. Kijana huyo ambaye mara zote ni mcheshi
na akitaniana na ndugu pamoja na wanafunzi wenzake huku akionesha furaha
ya kuwa mshindi, anasema kuwa ushindi wake ni wa familia na kampuni
yake yenye wenzake watatu.
Abdallah ni kitinda mimba akiwa na pacha wake, Hannat, katika familia
ya mama Lulua Chandoma na baba Said Chandoma wenyeji wa Pemba katika
mji wa Zanzibar. Abdallah anasema alipata ushindani mkubwa katika
uchoraji wa nembo hiyo kutoka kwa marafiki zake huku akiungwa mkono na
wazazi wake.
Anabainisha kuwa katika shindano hilo aliweza kujinyakulia Sh milioni
tano na cheti maalumu, zawadi ambazo alisema anazipeleka katika kampuni
ikiwa ni moja ya hamasa kuongeza juhudi katika shughuli zake. Abdallah
anasema akiwa mdogo alipenda kuchora michoro mbalimbali lakini alipofika
kidato cha sita alianza kuchora picha kwa kutumia utaalamu wa kompyuta
ujulikanao kama Photoshop.
Anasema lakini alipofika chuo kikuu akiungana na wenzake wawili ambao
alisoma nao awali, waliamua kuanzisha kampuni na kutengeneza nembo,
‘banners’, mabango na stika mbalimbali huku wakiendelea na masomo.
Anasema mwaka huu walianza kutengeneza kwa kutumia utaalamu wa kwenye
kompyuta wa Illustrator ambao anakiri kuwa yote wanafanya kwa kipaji na
utundu kwani hawafundishwi popote shuleni.
“Uchoraji huu nimeufanya tangu mtoto na nimekuwa kila mara
nikijifunza mwenyewe, hivyo kwa kushirikiana na wenzangu mwaka jana
tuliamua kuanzisha kampuni yetu wenyewe,”anasema. Anawataja wenzake
katika kampuni yao iitwayo Alpha Arts akimaanisha kuwa sanaa wanayofanya
kwanza, ni Owen Patrik (23) wanayesoma naye IFM na Edwin Mmuni (23)
anayesoma chuo cha Arusha.
Akizungumzia jinsi wanavyofanya kazi huku mmoja akiwa Arusha anasema
mara nyingi hutumia simu kwa kupiga na wakati mwingine hutumia utaalamu
wa kujadili pamoja kwa simu kwa wakati mmoja (Conference Call). Anasema
kwa sasa wanamalizia usajili wa kampuni hiyo ambayo wamempa kazi
Mwanasheria kusimamia usajili kutokana na kuwa wao wako vyuoni huku
wakiendelea na kazi wanazopata kwenye kampuni yao.
Abdallah anasema wanatarajia ifikapo Aprili mwaka huu watazindua
rasmi kampuni yao pamoja na tovuti itakayoonesha kazi zao zote
walizowahi kufanya. Kushiriki Shindano la Nembo Abdallah anasema siku
tatu kabla ya kufikia tarehe ya mwisho ya shindano ndipo mmoja wa
marafiki zao aliwataarifu kuwepo wa shindano hilo na kuwataka kujaribu.
Anasema wote walipatwa na shauku ya kufanya hivyo lakini kutokana na
siku hiyo kuwa na kazi nyingine katika kampuni yao ambazo zilishalipiwa
na wateja zilitakiwa kuchukuliwa siku hiyo. Kutokana na hali hiyo,
kulitokea ubishani mkubwa baina yao ambapo wapo waliotaka kumalizia kazi
waliolipwa kwani ubunifu wa nembo ni kubahatisha tu huku yeye akiwataka
kufanya zote.
Mwisho yeye akikazania jambo lililowafanya wenzake kujitoa wakati
wameshaanza ubunifu wa awali kwa pamoja hivyo yeye akaamua kuendelea na
ubunifu wa nembo hiyo. Anasema wakati mwisho wa kupeleka nembo hizo za
ushindani ikiwa Desemba 31 mwaka jana, yeye siku ya Desemba 30 ndipo
alipofika na kuliona jengo lenyewe ambalo awali alikuwa halifahamu.
“Baada ya kuliona kwani awali nilitengeneza nembo yenye sura ya Baba
wa Taifa nikaamua kulibadilisha na kuweka picha ya jengo kama unavyoona
na kutengeneza mandhari ya Jiji la Dar es Salaam kwa kuweka mnazi na
alama ya bahari,” anasema. Alisisitiza kuwa alitengeneza akiwa na
madhumuni ya kujaribu tu kwani aliamini zipo kampuni kubwa
zitakazoshiriki hivyo yeye kuwa vigumu kushinda ikiwa ni mara yake ya
kwanza kushiriki katika shindano kama hilo.
Abdallah anasema akiwa na wenzake walituma mara 10 nembo hiyo baada
ya kukamilika siku hiyohiyo ya mwisho kuanzia saa 10 jioni hadi saa 1:45
usiku ilipokubali kwenda. “Siku hiyo, mtandao ulikuwa ukisumbua sana
kutokana na kuwa ni mwisho wa mwaka hivyo tulijaribu kutuma lakini
ilikuwa imekataa na mara nyingine nilikuwa nakata tamaa kabisa lakini
ilipofika muda huo ikakubali,”anasema.
Abdallah anasema kuwa baada ya kushinda shindano hilo amepata mwamko
na yuko tayari kushiriki mashindano yoyote yanayokuja mbele yake. Huku
akiwataka vijana wenzake kuwa tayari kujaribu na siyo kuogopa na kudhani
kuna watu maalum watashiriki masuala mbalimbali.
Anasema hata siku moja hakuwahi kutegemea kazi ya mikono yake
kutumika katika jengo kub- wa kama hilo ambalo linatambulika ndani na
nje ya nchi huku likibeba heshima ya jina la Baba wa Taifa. Anasema yeye
na pacha wake ni watoto wa mwisho kati ya saba wa baba na mama
Chandoma, wa kike wanne na wa kiume watatu.
Anasema familia hiyo inaishi Boko jijini Dar es Salaam huku pacha
wake akimaliza Diploma ya masuala ya Masoko na kufanya kazi katika
Kampuni ya Samsung. Anasema amesoma Shule ya Msingi Mwenge huku Kidato
cha kwanza hadi cha nne akisoma Shule ya Sekondari ya Dar es Salaam.
Anasema baadaye kidato cha tano na sita alisoma Sekondari ya Makongo
na kuchukua masomo ya HGE (Historia, Jiografia na Uchumi) kisha baadaye
kujiunga na IFM. Akimzungumzia Abdallah, mama yake mzazi Lulua Chandoma
anasema tangu akiwa mtoto mwanawe huyo alipenda kuchora mara kwa mara
kiasi ambacho kuta zote za nyumba na geti zilijaa michoro tofauti ya
ubunifu.
Anasema familia imepata furaha ya ajabu na kumtaka ajiendeleze zaidi
na wao kuendelea kumpa ushirikiano kwani katika shindano hilo alipeleka
nembo mbili na baba yake alimchagulia ile aliyoshinda. Naye Meneja wa
Ukumbi huo, Deus Kulwa anataja sifa za nembo iliyoshinda kuwa ni na
alama ya jengo lenyewe, rangi ya dhahabu inayoonesha hadhi ya jengo hilo
kuwa ni dhahabu.
Pili ni rangi ya bluu inayoonesha jengo lipo Pwani karibu na bahari,
anga ya dunia na mnazi ambao ni alama ya zao la Pwani. Akizungumza kwa
niaba ya Kampuni yao, Mmuni anasema suala hilo ni la kujivunia na
itatumika kutangaza kampuni hiyo ya vijana wadogo ambao wamethubutu kwa
nia ya kujiajiri.
Akizungumza wakati wa kuzindua nembo hiyo, Membe alisema kupitia
kituo hicho Serikali imejiandaa kuleta ulimwengu Tanzania na nembo hiyo
iwe chachu ya Watanzania wote kutumia kituo hicho kwa mikutano
mbalimbali, sherehe na hata zile za kijamii kama harusi.
“Ni vema Watanzania wote kuleta mikutano ya taasisi, kampuni za
kimataifa na hata sherehe mbalimbali ili kumuenzi Baba wa Taifa kwa
kutumia kituo hicho ambacho ni kitega uchumi cha Serikali,” anasema
Membe. Naye Mkurugenzi Mwendeshaji wa AICC, Elishilia Kaaya anasema
katika mchakato wa kupata nembo hiyo ilishirikisha Watanzania kwa
kutumia vyombo vya habari ambapo walishiriki Watanzania 272
waliowasilisha nembo za ubunifu 352.
Alisema nembo iliyoshinda ilionesha sura na mandhari ya kituo kilipo
huku wakiwa na mikakati ya kujenga vituo vingine kama hivyo Zanzibar na
Iringa ambacho kitawezesha ukanda wa Kusini kuwa na utalii wa mikutano.
Alisema kituo hicho kimekabidhiwa rasmi kwa uongozi wa Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) ili kukisimamia na uongozi huo
umedhamiria kituo hicho kutofunikwa na kivuli cha AICC kwa kukipatia
nembo yake stahili.
Kituo hicho kilizinduliwa Machi mwaka jana na Rais wa Jamhuri ya Watu
wa China, Xi Jinping, alipokuwa katika ziara yake ya kiserikali ya siku
mbili nchini. Jengo hilo limejengwa na Serikali China, ujenzi wake
umegharimu dola za Marekani milioni 29.7 (Sh bilioni 47.5) likiwa na
uwezo kuhodhi Mikutano minne kwa mara moja, yenye idadi ya watu 1,600.
Kituo hicho cha mikutano kipo kitalu namba 10 katika makutano ya
barabara za Garden na Shaaban Robert kikiwa kimejengwa na Serikali ya
Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya China. Kazi za kituo hicho ni
kuendesha mikutano, kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana nchini
kupitia mikutano na kuangalia na kutunza majengo ya kituo hiki.
Katika kuendesha mikutano, kituo kina jumla ya kumbi 16 ambapo ukumbi
mkubwa kabisa una uwezo wa kuchukua hadi watu 1,003; kumbi za ukubwa wa
kati zenye uwezo kuchukua kati ya watu 150 mpaka watu 300, na kumbi
zingine ndogo 11 zenye uwezo wa kuchukua hadi watu 50 kila moja.
Pia Kituo kina kumbi kwa ajili ya sherehe mbalimbali kama harusi na
shughuli za burudani likiwepo eneo la juu la wazi na Lobby tatu ambazo
hutumika kwa ajili ya Mchapalo na wakati mwingine kwa ajili ya maonesho.
Kumbi zote za mikutano katika Kituo cha JNICC zimefungwa vifaa
mbalimbali vya kisasa vinavyosaidia kuwezesha mikutano kwenda vizuri.
Chanzo Habari Leo
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako