A

A

Serikali Yakanusha kuhusu Habari za Gazeti la DAILY MAIL La Uingereza Kuhusu Ujangili.

SERIKALI imekanusha taarifa zilizochapishwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari nchini kuhusu hali halisi ya vita dhidi ya ujangili ambazo chanzo chake ni gazeti la Daily Mail on Sunday la Uingereza na kuziita za uzushi, uongo na upotoshaji wa hali ya juu.

Taarifa hizo zilidai kuwa nyara karibu zote zinazotoka nchini zilikamatwa nje ya nchi badala ya ndani, jambo ambalo Serikali imesema si za kweli na ukweli ni kwamba nyara nyingi zimekamatwa nchini zikiwa kwenye harakati za kusafirishwa nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa
habari, Dar es Salaam jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema Daily Mail iliandika makala hayo bila kuwa na chanzo cha uhakika na kusisitiza kuwa Serikali ina nia thabiti na ya dhati kuhakikisha inashinda vita dhidi ya ujangili.

“Taarifa zilizochapishwa kwenye makala hayo zimejaa uongo, uzushi na upotoshaji wa hali ya juu kuhusu hali halisi ya vita dhidi ya ujangili nchini. Napenda kuwahakikishia Watanzania wote kuwa Serikali ina nia thabiti ya kuhakikisha inashinda vita hii ya ujangili,” alisema na kuongeza: “Operesheni Tokomeza bado inaendelea na itaendelea kufikia hata wanaojiita wababe wa ujangili,” alisema.

Katika kuhakikisha taarifa za Daily Mail hazikufuata misingi ya kiuandishi kwa kupata chanzo chenye uhakika, Waziri Nyalandu alitoa takwimu zinazoonesha kuwa nyara karibu zote zilikamatwa nchini.

Alisema katika miaka mitatu kuanzia 2010 hadi mwaka jana, jumla ya kilo 19,943 sawa na tani 20 za meno ya tembo zilikamatwa nchini, ambapo watuhumiwa 322 walikamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Aidha, tani 12.2 zilikamatwa mwaka jana pekee na watuhumiwa 145 walitiwa mbaroni akiwamo raia wa nchi hiyo (Uingereza) aliyefahamika kwa jina la Robert Dewar Twist ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Trans-African Logistics Limited ya Dar es Salaam, aliyekamatwa Agosti mwaka jana akiwa na nyara za Serikali na madini vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya dola 911,500 (sawa na Sh bilioni 1.4).

Wengine ni raia wa China ambao ni Huang Qui, Chen Jin Han na Xufu Jie ambao walikamatwa Novemba 2 mwaka jana wakiwa na kilo 1,885 za meno ya tembo yenye thamani ya zaidi ya dola 3,600,000 ( sawa na Sh bilioni 5.8).

Alitaja watuhumiwa wengine waliokamatwa na nyara hizo kuwa ni Watanzania, Muhamedi Suleiman Musa na wenzake watano waliokamatwa Novemba 13, mwaka jana wakiwa na kilo 2,915 za meno hayo yenye thamani ya dola milioni 4.9 (sawa na Sh bilioni 7.9) ambapo watuhumiwa wote kesi zao ziko mahakamani.

Waziri Nyalandu alisema kwa kipindi cha mwaka 2010 hadi mwaka jana, tani 15.6 za meno ya tembo zilikamatwa nje ya nchi ikilinganishwa na tani 19.9 zilizokamatwa ndani ya nchi na kuhoji juu ya taarifa za kizushi na uongo za Daily Mail na kutaka wananchi na wadau kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na ujangili.

Hata hivyo Waziri Nyalandu alikiri kuwa vita dhidi ya ujangili ni kali na kukiri kuwapo mtandao mkubwa wa siri kutoka nje ya nchi, hasa mataifa ambayo ni masoko makubwa ya meno ya tembo, lakini akahakikishia wananchi kuwa Serikali inaendeleza mapambano kwa lengo la kubaini mtandao huo hatari na kuuvunja.

“Serikali kwa kushirikiana na wadau tumejipanga kushinda vita dhidi ya ujangili na tunaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano,” alisema Waziri Nyalandu.

Taarifa za gazeti hilo la Daily Mail zimekuja siku chache kabla ya kufanyika kwa mkutano maalumu uliotishwa na mwana wa Mfalme wa Uingereza, Prince Charles, jijini London mwezi huu, utakaozungumzia jinsi ya kuokoa wanyama walio hatarini kutoweka kwa sababu za ujangili na Rais Jakaya Kikwete ndiye anatarajiwa kuongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo.

Gazeti la Mwananchi jana lilikariri taarifa za Daily Mail zikidai kuwa Tanzania inatajwa kuwa kinara wa ujangili kwa kuua zaidi ya tembo 11,000 kwa mwaka, huku Rais Kikwete akielezewa kufumbia macho uhalifu huo.

Taarifa zilizidi kumchafua Rais Kikwete zikidai kuwa ana urafiki na wafanyabiashara wa meno hayo na kuhusisha pia wafadhili wa CCM katika biashara hiyo.

Pia taarifa hiyo iliwahusisha ndugu wa karibu wa Rais ikidai wana marafiki wakubwa, na pia kuwaingiza majaji, waendesha mashitaka na polisi kwamba wamekuwa wakirubuniwa kirahisi.

Source: Habari Leo 
Kusoma habari zilizoandikwa na Daily Mail ingia hapa>>HAPA

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako