Algeria imeanza siku tatu za maombolezi ya kitaifa
kufuatia kuuawa kwa watu sabini na saba kwenye ajali iliyohusiha ndege
moja ya Kijeshi Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.
Abiria mmoja alinusurika ajali hiyo iliyohusisha ndege aina
ya Hercules C-130 iliyoanguka katika eneo la milima ya Oum al-Bouaghi,
ikiwa njiani kuelekea mji wa Constantine.
Ripoti zinasema hali mbaya ya anga ilisababisha ajali hiyo ya ndege.
Rais wa nchi hiyo Abdelaziz Bouteflika amewasifu wanajeshi waliopoteza maisha yao na kuwataja kama wafia dini wa taifa hilo.
Wengi wa abiria sabini na nane waliokuwa ndani ya ndege hiyo ni maafisa wa kijeshi na familia zao.
Mwanajeshi aliyenusurika, anaripotiwa kuendelea kupokea
matibabu katika hospitali moja mjini Constantine kufuatia majeraha ya
kichwa.
Wizara ya Ulinzi imesema kuwa imeunda tume maalum kuchunguza
ajali hiyo na kuwa Ahmed Gaid Salah, ambaye ni mkuu wa majeshi nba naibu
waziri wa Ulinzi atazuru eneo la ajali hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari,
wizara ya ulinzi imesema kuwa hali mbaya ya anga iliyohusisha kimbunga
na mvua kubwa ya barafu ilisababisha ajali hiyo.
Runinga ya taifa ilionyesha picha za ajali hiyo.
Awali maafisa wa Ulinzi na shirika hilo la habari liliripoti
kuwa watu 103 walikuwa ndani ya ndege hiyo lakini idadi hiyo ilipunguzwa
hadi watu sabini na nane.
BBC
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako