A

A

Tuwe na stara na kufikiria jamii na waathirika kabla ya kuweka picha online


Naandika hivi si kwa kuwa wavuti.com ni kamilifu ama inafanya vizuri kuliko nyinginezo, ila ni kutokana na kukosea katika machapisho yaliyotangulia, kukosolewa na kushauriwa ndiko kumenisababisha niwe na uthubutu wa kuomba sisi wenye blogu na tovuti za kusambaza taarifa na matukio mbalimbali.

Ninasihi ndugu zangu, tuwe na stara kwa wale tunaoonesha picha zao hadharani.

Tujiweke katika nafasi zao kisha tujiulize endapo yangekuwa yametupata sisi wenyewe, tungependa tutendeweje.

Tujiweke katika nafasi za watu wao wa karibu na kuona kama ndivyo ambavyo tungependa ndugu, jamaa na rafiki zetu 
watendewe.

Tuchukue hadhari zaidi hasa kwa watoto ama wasiojiweza kwa namna yoyote ikiwa ni ya ulemavu ama kutokujitambua kutokana na mkasa uliowapata kwa wakati huo.

Kama nilivyosema awali, hapa wavuti.com kila leo naendelea kujifunza kutokana na maoni na ushauri watu, lakini pia binafsi ninafahamu fika ilivyo vigumu kufanya maamuzi ya ama kuweka au kutokuweka picha za watu mfano, marehemu au waliopatwa na ajali na hivyo kuwapa simanzi zaidi wahusika ama wanaomfahamu mhusika, lakini kwa wakati uo huo unalazimika kuziweka ili kuwasaidia kupata taarifa na kuweza kutambua ndugu, jamaa na marafiki wanaotaka kufahamu ikiwa aliyekumbwa na mkasa ni ndugu yao ama la na hatua gani wachukue baada ya taarifa hizo.

Si jambo rahisi. Ila naomba turejeshe kwenye kujali utu na ubinadamu. Pale inapobidi, tuombe ridhaa za wahusika. Tusisubiri kuburutwa mahakamani ama kujengewa uhasama kwa kuwa 'insensitive' ndipo tujirekebishe.

Kilichonisabisha kuandika habari hii ni kutokana na picha nilizoziona zimechapishwa kwenye blogu fulani (bofya hapa kuziona kama bado zipo) hasa picha ya kwanza. Nadhani ingewezekana kuacha kutoa baadhi ya picha ama kuficha baadhi ya maeneo ya mwili kabla ya kuzichapisha hadharani. Siwafahamu wahusika wa kwenye picha hizo, ila nimepatwa na simanzi kwa kuziona.