Nasibu Abdul 'Diamond Platnumz'.
JINA lake lipo juu mno, pengine kuliko msanii mwingine yeyote kati ya
vijana wanaotingisha anga ya muziki wa kizazi kipya kwa sasa. Siyo jambo
la busara hata kidogo, kubeza uwezo wake katika kumiliki jukwaa, jinsi
anavyojituma na zaidi, tungo zake zinazoendelea ‘kubamba’ kila kukicha,
ingawa zina ujumbe unaofanana, kuhusu mapenzi!
Hapa ninamzungumzia Nasibu Abdul maarufu kwa mashabiki kama Diamond,
yule kijana aliyeibuka akitokea mitaa ya Tandale, jijini Dar es Salaam,
ambaye sasa anakula kuku kwa mrija katika maeneo ambayo miaka mitano
nyuma ilikuwa ni sawa na kumdhihaki mtu aguse mbingu!
Wakati flani nilipata kuandika habari zake, muda ambao rafiki yangu Said
Mdoe alikuwa akimtumia katika baadhi ya maonyesho yake, akimchanganya
na Mzee Yusuf wa Jahazi Modern Taarab. Kutokana na ugeni wake katika
fani, nilipata taabu sana kulijua jina lake, kila siku nilikuwa
nikiuliza, anaitwa nani vile?!!
Hivi sasa habari imegeuka, dogo anatisha na sidhani kama Mdoe anaweza
tena kumpandisha katika jukwaa, sijui! Binafsi sijawahi kukutana na
supastaa huyu, si kikazi wala bahati mbaya. Ninamsikia kama wengi
wanavyomsikia, ingawa tofauti yetu ni kwamba mimi sina mzuka naye!
Nimekuwa nikipata simu na sms nyingi katika safu hii, zikimlalamikia,
kwamba anaringa na kujisikia. Kama nilivyosema awali, sijawahi kukutana
naye, sijawahi kuzungumza naye na sitaki dhambi ya kumjaribu mtu. Kwamba
nijaribu kulazimisha nafasi ya kukutana naye ili nithibitishe madai
dhidi yake, naona nitakuwa sitendi haki.
Lakini nimejikuta nikilazimika kusema naye baada ya baadhi ya waandishi
wenzangu, nao kujiunga na mashabiki juu ya lawama za nyodo za Diamond.
Eti sasa hapokei simu zao, hajibu sms zao, hata kama zitakuwa ni kwa
ajili ya kuzungumzia kazi zake mwenyewe.
Wanapojaribu kuniambia kuhusu jinsi alivyokuwa anahangaika kuwatafuta
wakati ule akipanda mlima, sishangai kwa sababu ninayo orodha ndefu ya
wasanii wa aina hiyo. Baadhi yao walikaa kwenye maboksi nje ya ofisi,
wakisubiri tumalize kazi ili tufanye nao mahojiano, na walipiga simu
kila mara kuulizia kuhusu kutoka kwa habari zao.
Lakini hata walipofanikiwa, heshima iliendelea kuwepo. Ingawa sasa
hawawezi kukaa tena kusubiri kwenye maboksi, lakini angalau walipiga
simu kusalimia na mara zote walikuwa wepesi kupokea tulipowapigia na
kama walikuwa bize, hawakusita kueleza.
Tunao wasanii wa aina hiyo, hadi leo tuko nao pamoja wakiendeleza
harakati, bila kujali wana mafanikio kiasi gani. Diamond ni kijana
mdogo, aliyepata mafanikio ghafla. Ingawa mwenyewe amekuwa akielezea
jinsi alivyosota, akitaka tuamini kwamba amehangaika sana, lakini kwa
umri wake, nadhani haelewi nini hasa maana ya msoto.
Kama leo anawadharau waandishi, kwa maana labda sisi tunaoandika
magazetini, ambao tulitumia muda mwingi kumpamba ili atoke, huenda pia
hivi sasa anaweza kuwa anamdharau mama ntilie, aliyekuwa akimkopesha
ukoko wakati ule. Na ni jambo la kutegemea pia kwamba, huenda
anawadharau washkaji aliokuwa akishinda nao ghetto!
Nimshauri tu kuwa kelele dhidi yake zimekuwa nyingi, na bahati mbaya
zingine zinatoka kwa baadhi ya mashabiki wake. Maringo, kujisikia na
kujisifu ni hulka ya mtu, haizuiliki, lakini unapojaribu kutaka kuwa mtu
wa watu, ni vyema kuepuka baadhi ya tabia kwa manufaa yako na wadau
wako.
Nimkumbushe tu kuwa wapo wasanii ambao walianza kuwika tokea kuanza kwa
game na bado hadi leo wako levo za juu, lakini ushirikiano wao kwa
wanahabari, mashabiki na wadau ni wa hali ya juu!.
Credit:GPL
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako