A

A

Heka Heka za Uchaguzi huko CUF,Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad Avuta Fomu

Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akikabidhiwa fomu ya kugombea nafasi ya mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa, kutoka kwa Katibu wa tawi lake la Kidatu 'A' Mtoni, Bakar Hamad Ali. Aliijaza fomu hiyo na kuirejesha papo hapo.Picha na Salmin Said-Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amewataka wanachama wa chama hicho kufuata taratibu wakati wanapotaka kugombea nafasi za uongozi ndani ya chama.
Amesema si halali kwa mwanachama yoyote kupelekewa fomu ya kugombea nyumbani au ofisini kwake, na badala yake anatakiwa kuchukua fomu hiyo katika tawi lake au kumtuma mwakilishi wake kufanya hivyo.
Mhe. Maalim Seif ametoa kauli hiyo katika tawi lake la Kidatu ‘A’ Mtoni, baada ya kuchukua fomu ya kugombea ujumbe wa mkutano mkuu Taifa.
Amesema ameamua kuchukua fomu hiyo katika tawi hilo, ili kudhihirisha ukomavu wa demokrasia ndani ya chama hicho, na kwamba hila mwanachama ana haki ya kuchukua fomu na kugombea nafasi yoyote anayoitaka ndani ya chama.
Amesema chama kitahakikisha kuwa chaguzi ndani ya chama zitakuwa za uwazi, huru na haki, na hakuna atakayependelewa wala kuonewa   katika chaguzi hizo.
Amefafanua kuwa katika kuhakikisha hilo linatendeka, chaguzi za Wilaya zitasimamiwa na wajumbe kutoka nje ya Wilaya husika, na ikiwezekana baadhi ya wasimamizi watatoka Tanzania Bara.

Jumla ya viongozi 20 kutoka Wilaya ya Magharibi wanatarajiwa kuchaguliwa kuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu Taifa, kupitia mkutano mkuu wa Wilaya unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni, baada ya kukamilika kwa changuzi ngazi za majimbo.

Maalim Seif amechukua fomu hiyo ambayo aliijaza na kuirejesha papo hapo mnamo majira ya saa 6.00 mchana, ambapo alikabidhiwa na katibu wa tawi hilo nd. Bakar Hamad Ali.

Katika hatua nyengine, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amekemea tabia ya makundi na mitandao ndani ya chama, na kwamba makundi hayo hayakubaliki ndani ya chama hicho.

Amesema chama kinaweza kufuta uchaguzi wa ngazi yoyote ya chama iwapo kitabaini kuwepo kwa kampeni chafu, ikiwa ni pamoja na uwepo wa mitandao, makundi, pamoja kampeni chafu dhidi ya wagombea wengine.

Ameongeza kuwa mwanachama pia anayo haki ya kukata rufaa ikiwa hakuridhishwa na zoezi la uchaguzi, na kwamba rufaa yake itasikilizwa na kutolewa maamuzi yanayofaa kwa mujibu wa taratibu za chama.

Nae Mwenyekiti wa Tawi la Kidatu ‘A’ Mtoni bw. Ali Juma, amesema nafasi za uongozi ndani ya chama hicho ziko wazi, na kila mwanachama ana haki ya kuomba nafasi yoyote ya uongozi.

Amesema kitu cha msingi ni kufuata taratibu zilizowekwa, ambazo zinatoa fursa ya demokrasia ndani ya chama hicho.
 Na 
Hassan Hamad
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako