A

A

EU yatoa bilioni 9.76 kwa ajili ya uchaguzi nchini

Umoja wa Ulaya umetoa Sh.bilioni 9.76 kwa ajili ya uchaguzi nchini kupitia mpango wa DEP, unaofadhiliwa wahisani mbalimbali na kusimamiwa na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa  (UNDP).
 
Taarifa iliyotolewa na Afisa habari wa Umoja huo,  Susanne Mbise, ilisema kesho,  mkuu wa EU nchini, Balozi Filiberto Sebregondi na mratibu wa UN pamoja na mwakilishi wa UNDP nchini, Alberic Kacou watasaini na kuzindua rasmi ushirikiano wa EU-UNDP.
 
“Katika msaada huo wa kusaini kwenye uchaguzi wa Tanzania, Programu ya Uwezeshaji Demokrasia (DEP), shughuli hiyo itahudhuria na mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva,” ilisema taarifa hiyo.
 
Taarifa hiyo iliongeza kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha pamoja na wanachama wa kamati ya taifa ya Uendeshaji ya DEP na wawakilishi wa taasisi maalum za uchaguzi watashuhudia hafla hiyo.
 
“Wengine watakaokuwepo kesho katika ofisi zetu za EU ni  mashirika ya kiraia yanayoshiriki katika uchunguzi wa ndani, usimamizi wa upigaji kura na elimu ya uraia,” ilisema.
 
Tanzania itafanya uchaguzi wake mkuu wa madiwani, wabunge na Rais mwaka ujao, mara baada ya kupatikana kwa Katiba Mpya ambayo huenda ikaruhusu uwepo wa serikali tatu, Tanganyika, Zanzibar na Muungano wa Jamhuri ya Tanzania.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI