A

A

Chadema Maji ya Shingo,Katibu CHADEMA asimamishwa uongozi

Kamati ya utendaji ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi, imemsimamisha Katibu wake, Jordan Membe, kwa madai ya kwenda kinyume na katiba ya Chama.

Habari kutoka wilayani humo zilizothibitishwa na uongozi wa chama hicho, ngazi ya wilaya na ile ya mkoa, zinaeleza Membe amesimamishwa kutokana na

kukiuka maadili ya uongozi, ikiwa ni pamoja na kujihusisha na masuala ya kuleta na
kusababisha vurugu ndani ya chama.

Baadhi ya wajumbe waliohudhuria kikao hicho, kilichofanyika makao makuu ya ofisi ya chama hicho, wilayani Nachingwea, ambao hawakupenda majina yao kuandikwa kwenye vyombo vya habari kwa madai sio wasemaji wa Chama, wameeleza kuwa Membe anadaiwa kusambaza waraka unaopinga kuondolewa kwa aliyekuwa Naibu Katibu mkuu, Zitto Zuberi Kabwe na wenzake.

Walisema kikao hicho kilichokuwa chini ya  mwenyekiti wa chama Wilaya ya Nachingwea, Hassani Likolovera na mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Mtwara, Kassimu Ahamadi Bingwe, zinaeleza kuwa Kamati imeamua kumsimamisha uongozi katibu wake kwa kukiuka kwa baadhi ya vifungu vilivyopo ndani ya katiba ya chama chao.

Aidha, wajumbe hao, walidai katika kikao hicho, kilikuwa na mvutano mkubwa, kwani wajumbe tisa kati ya 13 waliokuwepo katika kikao hicho, walipinga kitendo cha kusimamishwa Membe, huku wanne waliobaki wakipendekeza asimamishwe.

Pia,walisema wajumbe tisa walipinga hatua hiyo kwa madai hawajaona kasoro katika utendaji wake wa kutimiza majukumu yake ya kukitumikia chama hicho: “Baadhi yetu wamepinga hatua hiyo, lakini wenzetu walisema asimamishwe, hivyo hali ndio ipo hivyo,” alieleza mjumbe mmoja aliyehudhuria kikao hicho.

Katibu huyo alitafutwa lakini hakupatikana kuzungumzia suala hilo.

via Matukio blog