Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe akifurahia jambo na Mnadhimu
Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu (kulia) walipohudhuria
kikao cha Bunge, mjini Dodoma jana. Picha na Emmanuel Herman.
Dar es Saalam na Dodoma. Wakati
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe akitaka waziri anayehusika na
kusimamia Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC) achukuliwe hatua
kutokana na zabuni yenye harufu ya rushwa, imebainika kuwa hukumu
iliyotolewa na Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma (PPAA), imesema
kampuni iliyoshinda zabuni hiyo ilishiriki kuandaa nyaraka za zabuni.
Hukumu hiyo, ni ile inayohusu kampuni ya zabuni za kuandaa vifaa vya
uchaguzi vya kielektroniki, ambayo Nec iliipa kampuni za M/S Jazzmatrix
Cooperation na M/S Invu IT Solution, tenda hiyo iliyokuwa na thamani ya
Sh126 bilioni.
Hukumu hiyo ya PPAA imefikiwa baada ya kampuni za M/S Morpho na M/S IRIS
Corporation Technology kukata rufaa kupinga uamuzi wa NEC.
Akizungumza bungeni jana, Zitto alisema kuwa kampuni iliyoshinda zabuni
hiyo, gharama yake kwa kutoa huduma hiyo ilikuwa juu ilihali kuna
kampuni nyingine zilizokuwa na bei ya chini pamoja na sifa za kufanya
kazi hiyo.
Zitto alisema hayo wakati wa kuchangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala iliyowasilishwa na Kaimu Mwenyekiti
wa kamati hiyo, Gosbert Blandess.
Akijibu hoja za zabuni hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera
Uratibu na Bunge) William Lukuvi alisema kuwa, PPAA ilibaini kuwa
mchakato wa utoaji wa tenda hiyo ulikuwa na upungufu mkubwa na ndiyo
maana ilibatilisha tenda hiyo na kuamuru mchakato wa kumpata mzabuni
urudiwe.
“Hivi vifaa siyo vya kupigia kura, ni vya uandikishaji, mchakato wa
kumpata mzabuni ndiyo uliobainika kuwa na tatizo, tume ya uchaguzi
itachunguza kujua chanzo cha tatizo na ikibidi ichukue hatua,” alisema
Lukuvi.
Mapema akitoa maelezo yake, Zitto alisema kuwa “Serikali itoe taarifa
ndani ya Bunge, nini kilichotokea na ni moja ya pendekezo ambalo
ninataka kamati ichukue ili wafanyie azimio ili waziri anayehusika na
uchaguzi aje alitolee ufafanuzi nini kimetokea na hatua gani
zimechukuliwa,” alisema Zitto.
Alisema wanafahamu mfumo huo uliowahi kutumika katika nchi za Malawi, Kenya na Ghana, umeleta matatizo kwenye nchi hizo.
Alitaka waziri anayehusika kuwajibika kwa kuleta taarifa bungeni ili wabunge waijadili na kuona nini kilichotokea.
Alisema ni vizuri katika mchakato wa jambo kama hilo, wadau wote ambao
ni pamoja na vyama vya siasa washirikishwe katika hatua ya tathmini ili
kuweza kujenga kuaminiana na kuleta mfumo mzuri.
Katika hatua nyingine, Godbless Lema ambaye ni mbunge wa Arusha Mjini, ametaka majina ya watu walioficha fedha nje yatajwe.
Wakati Lema akisema hayo, Zitto alisema kuwa Serikali ieleza Bunge
sababu za ucheleweshaji wa ripoti ya utoroshwaji wa fedha nje ya nchi.
Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), alisema tatizo siyo sheria za kimataifa bali ni utayari
wa Serikali kulifanya jambo hilo kwisha. Alisema kwa sababu tayari kuna
kampeni ya kimataifa ya kutaka kudhibiti utoroshwaji wa fedha na kwamba
kuna mikataba mbalimbali.
Alisema kuna mikataba kwa ajili ya kupeana taarifa na Afrika zimesaini ambazo ni Ghana, Afrika Kusini na Nigeria.
“Utapataje taarifa wakati hujasaini convection (mkataba) kama huu, topic
sasa ni mabilioni ya fedha za Uswisi lakini ni zaidi ya mabilioni ya
Uswisi,” alisema.
“Uswisi Sh319 bilioni, Genes kisiwa kimoja nchini Uingereza kina zaidi
ya trilioni moja za Watanzania na ukikaa mtajadili na Watanzania na
wanapenda vitu vyepesi vyepesi.”
“Na Watanzania watakwambia taja majina taja majina, majina hayatasaidia,
kwa sababu suala zima ni la mfumo kwa hiyo tunahitaji Serikali iweze
kueleza namna gani itaingia mikataba hii ya kimataifa,” alisema Zitto.
Akijibu hoja za Zitto, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Fredrick Werema,
alisema maneno ambayo aliyasema Zitto hayafanani na mwenendo wake wala
kauli alizozitoa mbele ya kamati iliyoundwa na Serikali kuchunguza
sakata hilo.
“Leo anataka tuangalie mfumo badala ya majina nakumbuka katika Bunge la
Tisa, mimi nilikuwa nasema tuangalie mfumo lakini Zitto akasema umefika
wakati wa yeye kutoa dukuduku lake atoe taarifa zake na nyaraka
alizonazo ili watu hao washughulikiwe,”alisema
“Sasa leo tofauti kutokana na kauli ya Mheshimiwa Zitto Kabwe, Bunge
lilitoa hadidu rejea kuchunguza na kubaini majina ya Watanzania
wanaodaiwa kuwa na fedha nje kinyume cha sheria,”alisema.
Alitaja hadidu nyingine za rejea kuwa ni kuchunguza kama fedha hizo ni
haramu, kutambua benki ambako fedha hizo zipo na kuandaa mashtaka na
kuishauri Serikali.
Alisema Februari 26 kamati ilikutana na Zitto katika ofisi zake zilizomo
ndani ya Bunge na akawaambia kuwa anazo taarifa na nyaraka lakini
akatoa masharti mawili.
Moja ya masharti Zitto alitaka kuhakikishiwa na Bunge kuwa hakuna mtu atakayemsonga baada ya kutoa taarifa.
Alisema pia Zitto alitaka Werema aje kiapo kwamba ikigundulika kama si kweli awe huru.
Alisema Machi 23 Zitto akaenda JKT Tanga, lakini kamati ilipoenda Tanga
kumfuata walishauriana kuwa amalize mafunzo na kwamba wakutane Dar
lakini hakufanya hivyo. Alisema walikutana tena bungeni Mjini Dodoma na
kudai kuwa anakwenda Afrika Kusini na hivyo kushindwa kuhojiwa.
Hata hivyo, Mei walikutana katika Viwanja vya Bunge, alipohojiwa
aliondoka katika mahojiano kwa madai kuwa ana hoja muhimu kwa masilahi
ya taifa bungeni na kuahidi angerejea lakini hakufanya hivyo.
Alisema alipotafutwa, alisema yuko Dar es Salaam na kwamba hana nafasi alikuwa anajiandaa kuisaidia timu ya Taifa (Taifa Stars).
Alisema Juni walichukua maelezo ya Zitto chini ya kiapo ambapo alisema
hakuwa na jina wala akaunti ya Mtanzania yeyote aliyeficha fedha nje ya
nchi. “Zitto Kabwe ni mzito… na hili la Zitto tutashughulika nalo
kisheria kwasababu huwezi kusema uongo bungeni na katika kamati halafu
ukaenda hivi hivi,” alisema.
Aliomba kuongezwa muda wa miezi sita ili kukamilisha kazi hiyo.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako