A

A

Wafungwa 1,475 huru, makongamano yatawala

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emanuel Nchimbi
 
Jana Tanzania iliadhimisha miaka 52 ya Uhuru wake huku Rais Jakaya Kikwete akiwapa msamaha wafungwa 1,475, na kuamuru wafungwa wote kupunguziwa asilimia moja chini ya sita ya adhabu zao.
Aidha maadhimisho hayo yaliambatana na makongamano na mikutano ya kisiasa na kutathmini yaliyofanyika katika kipindi hicho.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari jana na kusainiwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emanuel Nchimbi,  msamaha huo unawahusu wafungwa wenye magonjwa ya Ukimwi, Kifua Kikuu (TB), saratani, ambao wako katika hatua ya mwisho na  wazee wenye umri wa miaka 70 na zaidi.

Wengine ni wafungwa wanawake wajawazito  walioingia na watoto wanaonyonyesha na wasionyonyesha,  pamoja na  wenye ulemavu wa mwili na akili.

Taarifa hiyo  ilieleza kuwa, msamaha huo hauwahusu wafungwa waliohukumiwa kunyongwa, waliohukumiwa adhabu ya kifo na kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha gerezani pamoja  wanaotumikia kifungo cha makosa ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Wafungwa wengine wasiohusika na  msamaha huo ni wale wanaotumikia kifungo cha makosa ya kupokea au kutoa rushwa, makosa ya unyang`anyi wa kutumia silaha, makosa ya risasi au silaha, wafungwa wenye kosa la kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

 Wengine ni  wafungwa wanaotumikia kifungo hicho chini ya kifungu cha sheria ya huduma kwa jamii ya 2002, wafungwa  waliowahi kutoroka au kujaribu kutoroka gerezani na wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao.

Jijini Dar es Salaam Rais Kikwete alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo  yaliyoambatana na upigaji mizinga 21 huku ndege tatu za kivita zikiruka angani kutoka Kusini kuelekea Kaskazini..

Tukio hilo liliwafurahisha wengi hasa pale ndege moja ilipokuwa ikiruka juu kwenye usawa wa uwanja huo huku ikijizungusha na kwenda mbele kwa mwendo wa kasi.

 Maadhimisho hayo, pia yaliambatana na gwaride maalumu la mwendo wa pole pole na wa haraka kutoka kwa vikosi vya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Magereza, Polisi na lile la Kujenga taifa, ambalo liliwagusa mamia ya wananchi waliofika katika viwanja vya Uhuru kwa ajili ya tukio hilo hasa pale vikosi vya wanawake vilipokuwa vikionyesha umahiri wake wa kucheza gwaride.

Walikuwapo pia wanafunzi 1,990 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, ambao walionyesha umahiri wao wa kucheza michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutengeneza maumbo ya mawimbi yanavyotua kuonyesha changamoto ambazo taifa lilipitia hadi kupatikana kwa uhuru.

Michezo mingine iliyochezwa na wanafunzi hao ambao walikuwa wamevalia sare mbalimbali ikiwamo ile iliyokuwa na rangi ya bendera ya taifa, hata kuwafanya wengi  waliohudhuria maadhimisho hayo kushangilia ni pamoja na kuunda sura za marais Kikwete na Dk. Shein, kila mmoja akiwa katika moja ya pembe ya bendra ya taifa.

Viongozi wengine waliohudhuria ni Makamu wa Rais, Dk. Gharib Bilal; Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; Rais wa Zanzibar, Dk. Mohamed Shein na Makamu wa Pili wa rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.

Wengine ni Jaji Mkuu, Othman Chande; Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omari Kungu; Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Abeid Aman Karume; Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela; Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa Taifa wa  CUF ,  Prof. Ibrahim Lipumba.

 Rais  Kikwete aliwataka Watanzania kuyaenzi yote yaliyolifikisha taifa la Tanzania hadi hapo lilipo, kwa amani.

KONGAMANO LA BAVICHA

Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), limesema halitakubali kuona viongozi wa kitaifa wanadhalilishwa na kudhihakiwa na kikundi cha mamluki waliopandikizwa kuharibu mikutano ya katibu mkuu wa chama hicho, Dk. willibrod Slaa.
Limesema italinda kwa nguvu zote mikutano hiyo na kukabiliana na mamluki wanaopandikizwa ili kushawishi polisi kupiga marufuku mikutano ya chadema kwa kuwa ina sura ya vurugu.

 Mwenyekiti wa Bavicha taifa, John Heche, alitoa msimamo huo jana, ulioungwa mkono na viongozi wengine na wajumbe wa kamati kuu, katika kongamano la kutafakari miaka 52 ya uhuru na mustakabali wa taifa kimaendeleo.

Alisema vijana watailinda Chadema na viongozi wao na kamwe hawatakubali kutishwa kwani yanayojitokeza sasa hayana taswira njema kwa chama bali yanafanywa na waliobainika kuwa wasaliti na kutimuliwa.

Naye Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, alisema ni lazima chama kikubali mabadiliko na chama chochote kisichokubali hayo kina lengo la madaraka na ni vigumu kuweka kuongoza nchi ifikapo 2015.

Naye Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, alisema kamwe vijana wasiruhusu akili ndogo kutoa wala akili kubwa kwa kukataa kutumia kisiasa na badala yake kusukumwa na changamoto zinazolikabili Taifa kwa sasa kubwa ikiwa ni kuporwa kwa rasilimali.

Alisema adui wa wakati Tanzania ina pata uhuru alikuwa ni ukoloni ila kwa sasa ni adui rushwa, ufisadi na wizi wa mali ya umma, hivyo zinahitajika mbinu mpya kukabiliana naye.

 “Tulitaraji miaka 52 ya uhuru kuwa na taifa la umoja na usawa ila imekuwa tofauti,hivyo ni lazima kujua adui wa kweli ambaye ni CCM na kijana yoyote asikubali kufanya kabla ya kutoa mchangao utakaokumbukwa na vizazi vijavyo,” alisema Msigwa.

Kwa upande wake, Mnadhimu Mkuu wa kambi ya upinzani Bungeni, Tundu Lissu, akiwasilisha mada ya miaka 52 ya Uhuru na umilikaji wa rasilimali zake, alisema ni lazima kung’oa na kuondoa uchafu ndani ya chama kinachojiandaa kushinda dola na kwa maamuzi ya Kamati Kuu (CC) ni katika kusafisaha waliomamluki.

Alisema Tanzania ni ya tatu kwa utajiri wa dhahabu lakini kwa kipindi cha miaka 10 kinachoishia 2011 mauzo ya madini hayo pekee ni dola billioni 12 za kimarekani ,huku kukiwa na utajiri wa wanyamapori wanatumika kwenye utalii na uwindaji lakini biashara hiyo inamalizikia Ulaya na wageni wanapofika nchini huja na fedha za juisi na maji.

Alisema migogoro ya wakulima na wafugaji ina shika kasi nchini baada ya wafugaji kuporwa maeneo yao na kuwa hifadhi za taifa bila kuwapa mbadala.
 Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, akiwasilisha mada ya wajibu wa vijana katika ukombozi wa pili wa Tanzania na katiba mpya, alisema katiba ijayo itamke kuwa rasimali za nchi ni za watanzanai wote hivyo wananchi wanaotoka maeneo ya rasilimali zao wanufaike wa kwanza ikiwa ni pamoja na kupewa taarifa kamili.

KONGAMANO LA UDOM

Vijana nchini wametakiwa kuachana na tabia ya kuwa watumwa wa majina ya vyama vya siasa na kushindwa kutafakari mstakabali wa Taifa.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mbunge wa Kasulu Mjini(NCCR-mageuzi), Moses Manchali wakati akiwasilisha mada ya Vijana katika harakatiza kisiasa na maendeleo ya Taifa kwenye mdahalo wa miaka 52 ya Uhuru uliofanyika katika  Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Alisema vijana wamekuwa watumwa wa vyama na tatizo hilo limekuwa likiwafanya vijana kushindwa kuikwamua nchi katika tatizo lilopo.

“Tunapoadhimisha miaka 52 ya Uhuru wa nchi yetu ni vema sasa vijana tukatafakari na kubadilika upya,” alisema Manchali.

Rais wa Jopo la Wanataaluma Udom (Udomasa), Profesa Kalafunja Osaki, alisema Vijana wengi wameharibikiwa na utandawazi na kujikuta wakifanya mambo mabaya badala ya kufanya mambo ya maendeleo  ya Taifa.

“Dira ya nchi itoke kwa wananchi wenyewe, sasa vijana watachangia nini katika hiyo dira au mmekaa tu na kupoteza muda wenu kwenye mitandao ya kijamii…kwanini umoja wa vijana wa CCM na vyama vingine kwanini hawana nguvu sasa tunahitaji kubadilika,” alisema Profesa Osaki.

Naye Mhadhiri Msaidizi wa Udom, Stella Faustine, alisema vijana wameharibiwa na mambo ya utandawazi na kubweteka badala ya kujituma kwa maendeleo ya nchi na kutambua wajibu wao.

Mwakilishi wa Umoja wa Wanafunzi wa Udom (Udoso), James Martine, alisema vijana wanatakiwa kujitambua na kujitokeza katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.

DK. SLAA
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Willibrod Slaa, ameibua hoja mpya kwa kuitaka serikali ya CCM iwaeleze wananchi mapato ya fedha zilizopatikana tangu Tanganyika ilipopata huru mwaka 1961 ili waweze kupambanua kama zimetumika vizuri au kifisafi.

Alisema hayo wakati akizungumza na wakazi  wa kijiji cha Janda kilichopo jimbo la Manyovu wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma  jana.

Alisema wakati Watanzania wanasherehekea miaka 52 ya Uhuru, serikali inapaswa kueleza mchanganuo wa mapato yaliyopataika ili wananchi wabainishe kama zimetumika kuwaletea maendeleo au zimewanufaisha watu wachache wakiwamo mafisadi.

Hivi sasa matumizi ndani ya serikali ni makubwa kuliko mapato,nachotaka wananchi tuungane tuhoji chenji yetu ipo wapi,wasitugeuze wendawazimu,” alisema huku akishangiliwa na mamia ya wananchi.

Alisema kumekuwa na matumizi makubwa ya fedha serikali hali ambayo imekuwa ikipelekea wananchi kuchangishwa kwa ajili ya kuchangia miradi ya maendeleo ambayo kama serikali ingekuwa na matumizi mazuri wananchi wasingechangishwa.

Dk.Slaa alisema umefika wakati kwa wananchi kuhakikisha kunakuwa na serikali itakayopiga vita masuala ya ufisadi tofauti na sasa mafisadi wanaonekana kutembea kifua mbele bila kuchukuliwa hatua za kisheria.

Alisema wakati wa utawala wa Rais wa awamu ya kwanza Mwalimu Julius Nyerere alipinga vita ufisadi na rushwa na kiongozi akibainika kufanya vitendo hivyo anachukuliwa hatua hapo tofauti na ilivyo sasa.

PROFESA LIPUMBA
Mwenyekiti wa CUF, Prof. Lipumba, akizungumza katika maadhimisho hayo, aliitaka serikali kujenga mazingira ya kuwapatia vijana ajira ili kuleta maana halisi ya kuwaenzi vijana kupitia kaulimbiu kwenye maadhimisho hayo ambayo kaulimbiu yake ni “vijana ni nguzo ya rasilimali watu: tuwaamini, tuwawezeshe  na tuwatumie kwa manufaa ya taifa letu”. Imeandikwa na Elizabethh Zaya, Isaya Kisimbilu, Salome Kitomari, Thobias Mwanakatwe na Agusta Njoji.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako