THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za
Rambirambi Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Abdulrahaman
Kinana kuomboleza kifo cha Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Emmanuel Mteming’ombe
kilichotokea usiku wa kuamkia tarehe 19 Desemba, 2013 katika Hospitali ya Rufaa
ya Mkoa wa Iringa alikokuwa amelazwa kwa matibabu akisumbuliwa na ugonjwa wa
pumu na figo.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na
kuhuzunishwa sana na taarifa za kifo cha Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa
Iringa, Emmanuel Mteming’ombe kilichotokea tarehe 19 Desemba, 2013 katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kutokana na ugonjwa wa pumu na figo”,
amesema Rais Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi.
Rais Kikwete amesema
alimfahamu Marehemu Mteming’ombe, enzi za uhai wake, kama Kada Hodari,
Mwaminifu na Mchapakazi wa Chama Cha Mapinduzi ambaye alipikwa vilivyo na Chama
tangu alipokuwa na wadhifa wa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha
Mapinduzi (UVCCM) katika Chuo cha
Utabibu Songea, hadi alipoteuliwa kuwa Katibu wa CCM Mkoa wa Ruvuma kabla ya
kuhamishiwa katika Mkoa wa Iringa ambako mauti yamemkuta.
“Kwa hakika kifo cha Emmanuel Mteming’ombe
kimeacha simanzi na huzuni kubwa kwa Wana-CCM, na kimesababisha pengo kubwa
katika Chama chetu lisiloweza kuzibika kwa urahisi siyo tu katika Mkoa wa
Iringa aliokuwa akiutumikia, bali Taifa kwa ujumla kwa vile mchango wake kwa
CCM ulikuwa ndiyo kwanza unahitajika zaidi ili kukiimarisha na kukiendeleza zaidi
Chama, na kusukuma gurudumu la maendeleo kwa kasi zaidi katika nchi yetu”, ameongeza kusema Rais Kikwete.
“Kutokana na msiba huu mkubwa, ninakutumia wewe
Katibu Mkuu wa CCM, ndugu Abdulrahaman Kinana Salamu za Rambirambi kutoka dhati
ya moyo wangu kwa kumpoteza Kada muhimu katika Chama. Aidha natoa pole kwa Wana-CCM wote wa Mkoa wa
Iringa na kwa kweli Wana-CCM kote nchini kwa kuondokewa na Kada mwenzao”.
Vilevile Rais Kikwete
amemuomba Katibu Mkuu wa CCM kumfikishia Salamu zake za Rambirambi na pole
nyingi kwa familia ya Marehemu Emmanuel Mteming’ombe kwa kumpoteza Kiongozi na
Mhimili muhimu wa familia, huku akisisitiza kuwa yuko pamoja nao katika kipindi
hiki kigumu cha majonzi na maombolezo.
Aidha Rais Kikwete
amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala
Pema Peponi Roho ya Marehemu Emmanuel Mteming’ombe, na anamuomba Mola awape
wanafamilia, ndugu na jamaa za Marehemu nguvu na moyo wa uvumilivu ili waweze
kuhimili machungu ya kuondokewa na mpendwa wao.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako