A

A

Prof. Kamuzora ateuliwa bodi ya kimataifa ya CTA


Kamati ya mabalozi toka nchi za Afrika, Karibiani, Pasifiki na Ulaya imemteua Mtanzania, Prof. Faustin Kamuzora (pichani), kuwa mjumbe wa bodi ya Kituo cha ufundi cha kilimo na maendeleo vijijini (CTA).
 Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa CTA, Bw. Michael Hailu, uteuzi huo ni wa miaka mitano kuanzia Novemba 7, 2013 hadi Novemba 6, 2018. Prof. Kamuzora pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Utawala na Fedha.

Bodi ya CTA inaundwa na wajumbe sita, watatu kutoka Afrika, Caribbean na Pacific na watatu wengine kutoka Umoja wa Ulaya. Prof. Kamuzora atawakilisha ukanda wa mashariki wa Afrika katika bodi hiyo.

Mkurugenzi wa Mawasiliano, Chuo Kikuu Mzumbe, Bi. Rainfrida Ngatunga alisema katika taarifa yake jana kuwa uteuzi wa Prof. Kamuzora ni sifa kwa chuo hicho, Tanzania na Afrika kwa ujumla.

“Tunampongeza kwa uteuzi wake…hii imeiletea sifa Mzumbe na kuifanya Tanzania in’gare katika anga za kimataifa zaidi,” alisema katika taarifa yake.
Bi.Ngatunga amemwelezea  Prof.Kamuzora kuwa ni mchapa kazi mzuri mwenye uzoefu wa kutosha na ndiyo maana anapata mafanikio makubwa.
CTA yenye makao makuu yake Wageningen, Netherlands, ni moja ya taasisi zilizoundwa ili kutekeleza makubaliano ya ushirikiano kati ya nchi za Afrika, Caribbean na Pacific kwa upande mmoja na nchi za umoja wa ulaya kwa upande mwingine.
Mkataba huo ulisainiwa Cotonou June 23, 2000 na kurekebishwa tena June 25, 2005, Luxembourg na June 22, 2010,Ouagadougou.
CTA inalenga kuimarisha sera na kujenga uwezo wa taasisi wa nchi za ACP zinazojihusisha na kilimo na maendeleo vijijini.

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako