A

A

Mtanzania linasema Rais Kikwete anatarajiwa kupangua Baraza la Mawaziri


IMEELEZWA kuwa Rais Jakaya Kikwete wakati wowote kuanzia Desemba 15, mwaka huu atafanya mabadiliko makubwa ya Baraza lake la Mawaziri.

Hatua ya kwanza ya mabadiliko hayo imeanza kwa kumteua Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Asha-Rose Migiro kuwa Mbunge wa Viti Maalumu na kwamba huo ni mkakati wa kumkabidhi mama huyo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi inayoshikiliwa na Dk. Shukuru Kawambwa.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani, zimeeleza kuwa hatua hiyo ya rais imekuja kufuatia uwepo wa shinikizo la ndani na nje ya 
chama chake la kuwataka baadhi ya mawaziri wake kujiuzulu kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Imeelezwa kuwa Wizara ya Elimu inaonekana kusuasua na mtu pekee anayetajwa kuimudu wizara hiyo kwa sasa ni Dk. Migiro ambaye pia alishawahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Baadhi ya mawaziri ambao wamekuwa wakipatiwa shinikizo la kujiuzulu ni pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Kawambwa na Naibu wake, Philip Mulugo, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, Naibu wake, Adam Malima pamoja na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe.

Kinana amekuwa akiwaandama mawaziri hao, huku akishinikiza kuwashughulikia ndani ya Kamati Kuu ya chama hicho kwa kile alichodai wanakiangusha chama chao kwa kushindwa kutatua kero za wananchi ambao wanazidi kupoteza imani na CCM.

Kutokana na dhana hiyo, imeonekana wazi kumshtua Rais Kikwete katika kuonesha dalili za kufanya mabadiliko ya baraza hilo la mawaziri, ili kuweka sawa upepo wa kisiasa ndani ya chama chake.

Hali kama hiyo ilitokea pia Mei mwaka jana, ambapo Rais Kikwete aliwateua wabunge watatu wapya ambao ni James Mbatia, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. William Mgimwa na Naibu wake, Janeth Mbene.

Taarifa za uhakika zimebainisha kuwa mabadiliko ya mawaziri yatafanyika mara baada ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM kukutana mjini Dodoma wiki ijayo.

via gazeti la MTANZANIA

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako