Mkaguzi wa hesabu katika Shirika la COASCO, Sabas Mlengela (54), amekutwa amekufa maji ndani ya mto, mjini hapa.
Walioshuhudia wamesema tukio hilo lilitokea jana asubuhi ambapo mwili wa mkaguzi huyo ulikutwa ukielea kwenye maji.
"Tulipofika
katika eneo hili tuliona sikio la mtu ndani ya maji na baadaye
tukabaini kuwa mtu amekufa akiwa na baiskeli yake na simu yake ilikutwa
nje," alisema shuhuda mmoja.
Alisema simu hiyo ndiyo iliyotumika kuwapigia ndugu zake kuwajulisha tukio hilo.
Aliongeza
kuwa kifo hicho kina utata huenda kilisababishwa na utelezi uliomfanya
atumbukie kwenye daraja au watu wabaya walimsukuma.
"Kwa
kweli tunashindwa kuelewa nini hasa chanzo cha kifo hiki, nadhani
marehemu atakuwa ameuawa na kutupiwa kwenye maji na watu wabaya kwani
haiwezekani mwili uwe majini halafu simu yake isiwe majini, na hawa
waliomuua nadhani siyo vibaka kutakuwa na fitina fulani tu," alieleza
shuhuda mwingine alijitambulisha kwa jina moja la John.
Kaimu
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga, ACP Kihenya Kihenya,
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mwili wa marehemu
ulikutwa umezama kwenye mto huo pamoja na baiskeli yake, ingawa simu
yake na kalamu vilikuwa vimeanguka pembeni mwa mto huo huku mwili wake
ukiwa hauna majeraha yoyote.
Kamanda
Kihenya alisema kwa mujibu wa maelezo ya ndugu wa marehemu, siku moja
kabla ya tukio walikuwa pamoja na Sabas kwenye kikao cha kuvunja kamati,
aliondoka saa 3 usiku na hakuonekana mpaka walipopata taarifa za
kukutwa akiwa amekufa.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako