KIPA Ivo Philip Mapunda, amesaini Mkataba wa kujiunga na klabu ya Simba SC ya Dar es Salaam,akitokea Gor Mahia ya Kenya.Ivo amesaini Simba SC, baada ya kung’ara akiwa na kikosi cha Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge mwaka huu
Ivo aliiongoza Kilimanjaro Stars kufika Nusu Fainali ya Challenge baada ya kuwatoa waliokuwa mabingwa watetezi Uganda ‘The Cranes’ kwa penalti 3-2 kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90, kipa huyo akicheza mikwaju miwili.
Ivo alisema kwamba ameamua kusaini timu hiyo yenye makao makuu Mtaa wa Msimbazi baada ya kuridhishwa na maslahi aliyopewa.
Ivo alisema kwamba Simba SC ni timu kubwa na anaamini atafanya vizuri. Ivo pia amewahi kuidakia Yanga SC.
Ivo Philip Mapunda alizaliwa Novemba 14, mwaka 1979 na kisoka aliibukia katika klabu ya Tukuyu Stars kabla ya kuhama Prisons zote za Mbeya, baadaye Moro United mwaka 2005 kabla ya kuichezea Yanga msimu uliofuata, 2006.
Aliidakia Yanga hadi 2009 akahamia St George ya Ethiopia alikofanya kazi msimu mmoja, akarejea nyumbani kuidakia African Lyon 2011 kabla ya 2012 kuhamia Bandari ya Mombasa, Kenya ambako alifanya kazi kwa miezi sita akasajiliwa na Gor Mahia.
Ivo anamaliza Mkataba wake Gor Mahia Desemba 16, mwaka huu na ataidakia kwa mara ya mwisho klabu hiyo katika mechi ya Kombe la DSTV Desemba 14 dhidi ya Tusker FC na baada ya hapo atapakia kila kilicho chake na kuja kuanza maisha mapya Msimbazi.
Kipa Ivo Mapunda na beki Donald Musoti, wote wamesaini rasmi kuichezea Simba kwa miaka miwili.
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako