A

A

USIWE MTU WA KUOMBA OMBA USHAURI


KATIKA maisha ya kimapenzi, amani ni jambo la msingi na linalopaswa kupiganiwa kwa nguvu zote na pande zote mbili. Ni kwa uwepo wa amani, ndipo tunapoweza kustawisha uhusiano wetu na hatimaye familia.

Na amani haipatikani sehemu ambayo imekosa masikilizano. Ni lazima kila mmoja awe tayari kupokea na kukubali maneno ya upande wa pili, hata kama hayatampendeza. Kusikia na kutekeleza ni vitu viwili tofauti. Wengi wetu tunashindwa kuligundua hili kwa makusudi au kwa kutofahamu.

Wapo wanaodhani kwamba kumsikiliza mwenza wako akiongea, maana yake ni kuridhia anachokisema, hapana. Moja ya makosa ambayo huyafanya kila mara ni kutotaka kumsikiliza mwenzio kwa kuwa tu mmetofautiana.

Ni hivi, lazima tujenge tabia ya kusikilizana, kwa nafasi. Kama mimi nitakuwa na la kusema kwa mwenza wangu, ni vizuri kama atakaa kimya na kunisikiliza maana anaweza akanielewa na tofauti zetu tukazimaliza kirahisi au kama hatanielewa, basi atapata nafasi nzuri ya kujibu nitakachosema kwa sababu atakuwa amenielewa vizuri sana.

Tatizo huwa watu wanachanganya mambo. Wanadhani kumsikiliza mwenzako ni kukubaliana naye. Hapana, msikilize, ndipo utakapoweza kumwelewa. Unapotoa nafasi ya kumsikiliza mwenzako, unampa deni la yeye kukusikiliza utakapohitaji masikio yake. Watu wasiosikilizana ndiyo wale ambao kila mara unasikia makelele ndani ya nyumba yao.

Mmoja au wote wawili wanadhani kupaza sauti ndiyo kumshinda mwenzake. Wanaamini katika kuongea kwa sauti kali badala ya kauli zenye busara kwa sauti ya upole. Binadamu tumeumbwa kwa namna ya ajabu sana, hata tuwe wakatili kiasi gani, mtu mwenye nia njema hutambulika kupitia kauli yake.

Badala ya kusema kwa ukali “Sikia nikuambie mjinga wewe…, mtu akasema kwa upole “Mama nanihii, lakini mbona hutaki kunisikiliza, hebu sikia..”
Namna mtu anavyocheza na sauti ndivyo anavyotuma ujumbe. Ujumbe unaotumwa unaonyesha dhamira ya mtumaji, kama ana shari au hekima. Ni nadra sana kutokea na inapotokea basi ni lazima upande huo uwe na matatizo, kwamba mtu anaongea kwa sauti ndogo, yenye kusihi, lakini ikajibiwa kwa ukali na matusi!

Hata hivyo, inapotokea mkashindwa kupata suluhisho ndani ya nyumba yenu, ni jambo la msingi sana kukaa kimya na kutafakari badala ya kukimbilia kwa majirani, ndugu na jamaa kwa ajili ya kuomba ushauri.

Hili linatokea mara nyingi sana, baadhi ya watu wamejikuta wakitoa siri zao nyingi nje, kwa sababu ya kutafuta ushauri kuhusu kinachoendelea katika uhusiano wao. Utakuta kuna tatizo limetokea, ambalo kama wangekaa chini na kusikilizana lingeisha mapema, lakini wao wanatumia muda mwingi kuwasimulia mashoga zao, na wakati huohuo wakitegemea kupata ushauri.

Watu ambao hukimbilia kwa majirani, marafiki au ndugu kwa ajili ya kuomba ushauri, wana kosa kubwa wanalolifanya. Tunaweza kudhani kuwa tuna lengo la kuimarisha ndoa au uhusiano wetu, lakini ukweli ni kwamba kinachofanyika, ni kutangaza ubaya wa uhusiano wetu kwa watu.

Hatujui tu, lakini huenda kila wanapotuona, wanaulizana “Vipi, leo hakuna muvu mpya?” kwa sababu wamezoea kukuona kila mara ukiwafuata na kuwasimulia kuhusu mambo mnayopishana wewe na mwenza wako.

Ni vyema kama kuanzia leo tukajifunza kwamba mlinzi mkubwa wa siri zetu ndani ya nyumba zetu ni sisi wenyewe. Ikiwa tutakuwa watu wa kupenda kutoa mambo yetu nje, tunawaruhusu watu kutuhoji. “Vipi, siku hizi shemeji ametulia?” swali kama hili unaweza kukutana nalo kama utakaa siku nyingi bila kwenda kuwahadithia mambo yanavyokwenda ovyo katika uhusiano wako.

GPL

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako