Na Saleh
Ally
Sakata la
kamati ya utendaji limeendelea kuchukua sura mpya kila kukicha na jana
mwenyekiti aliyesimamishwa, Ismail Aden Rage amejitangaza upya kuendelea na
nafasi yake.
Lakini
wajumbe wa kamati ya utendaji wameendelea kushikilia msimamo wao kutokana na
kikao walichokaa kwamba wao wamemsimamisha mwenyekiti huyo.
Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF) lililomtaka Rage kuitisha mkutano ndani ya siku 14 na
yeye jana akatangaza kukaidi, limesema litasubiri barua yake halafu liifikishe
kwenye kamati ya utendaji.
Kwa kifupi,
Simba bado hakujatulia na Rahma Al Kharusi ambaye alikuwa mjumbe wa kamati ya
utendaji na kuamua kujondoa anasema amekubali kuitumikia nafasi yake mpya
aliyoteuliwa.
Lakini
anasisitiza iwapo hali ya migongano isiyokwisha ndani ya klabu hiyo itaendelea,
basi yeye atajiondoa kabisa.
“Niko mbali
na ninabanwa na kazi zangu za kibiashara, lakini nimekuwa nikikerwa sana
kutokana na mambo yanayotokea ndani ya Simba.
“Mambo haya
ya migogoro si kitu cha kuendelea kukipa nafasi halafu tukaona ni mambo ya
kawaida, badala yake tuyakemee.
“Mimi
niliamua kujiondoa Simba kabisa, nilifanya hivyo kwa kuwa ninaona kama
tunapoteza muda na ugomvi na malumbano yanachukua nafasi yetu ya maendeleo.
Niliamua kujiondoa lakini nimezungumza na Rage kwa mara nyingine kaniomba tena
nibaki na kuisaidia Simba.
“Nabaki kwa
kuwa nina mapenzi na klabu na watu wake, sasa nimeteuliwa kuwa mjumbe wa bodi
ya wadhamini. Hii itanisaidia kutoingia katika mikutano mingi na badala yake
zaidi nitafanya kazi ya kulinda maslahi na mali za Simba.
“Lakini
kama bado migogoro itaendelea, kweli nitaondoka mara moja na kuendelea na
biashara zangu kwa kuwa hata zenyewe bado zinahitaji muda wangu,” anasema
milionea huyo mwanamke ambaye ni mmiliki wa makampuni ya RPB Group.
Alipoulizwa
kama anaunga mkono upande upi kati ya ule wa Rage na kamati ya utendaji, Malkia
wa Nyuki anasema:
“Mimi
nabaki kuwa kiongozi wa Simba nisiyekuwa na upande, siwezi kujua hata tatizo
hasa ni nini kwa kuwa niko mbali kama nilivyokueleza. Lakini jambo la muhimu ni
kuangalia maendeleo ya klabu.
“Yoyote
anayetaka maendeleo ya klabu ndiye tunafanya naye kazi, angalia suala la
Sunderland tumelishughulikia na limefikia pazuri, lakini inaonekana halipewi
kipaumbele kwa kuwa halina maslahi binafsi.
“Wako
wanaoangalia maslahi yao binafsi na si klabu, hawa wanakosea na lazima tukubali
Simba ni ya watu wengi na tunaopewa nafasi ya kuongoza ni dhamana tu. Lazima
tuitumikie klabu na kuwasaidia Wanasimba badala ya kuiangamiza.
“Kweli
naipenda Simba, lakini nasisitiza malumbano yasiyokuwa na msingi yakiendelea,
mara moja nitaondoka kwa kuwa hakuna faida ya kubaki hapo,” anasema Malkia wa Nyuki.
Mwanamama
huyo aliwahi kumwaga zaidi ya Sh milioni 80 kuisaidia Simba kuweka kambi nchini
Oman kwa siku 15, baada ya hapo akatoa zaidi ya Sh milioni 36 kuisaidia Simba
kulipa deni la Kocha Milovan Cirkovic ambaye uongozi wa Rage ulikuwa umeshindwa
kumlipa.
Kama hiyo
haitoshi, alilipa deni la Simba iliyokuwa inadaiwa mjini Arusha. Malkia wa Nyuki
alitoa Sh milioni 15 kwa mmiliki wa hoteli ambaye alikuwa amezuia basi la
Simba.
Halafu siku
hiyohiyo akatoa zaidi ya Sh milioni 15 na kupunguza deni kwa wachezaji
waliokuwa wanaidai klabu hiyo chini ya uongozi wa Rage.
Lakini siku
chache baadaye aliamua kukaa kimya hadi alipofanya mahojiano, jana na Championi
Jumatatu akisisitiza suala hilo la migogoro kumalizwa, la sivyo atajiondoa
zake.
CREDIT TO SALEHEJEMBE
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako