A

A

Kesi Ya Babu Tale Yaahirishwa, Arudishwa Mahabusu

Mkurugenzi wa Kampuni ya Tip Top Connection ya jijini Dar es Salaam, Hamis Taletale maarufu Babu Tale, leo Mei 23, 2018 saa 6 mchana amefikishwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kusikiliza kesi inayomkabili, akiwa chini ya ulinzi wa polisi.

Babu Tale, ambaye pia ni meneja wa mwanamuziki maarufu wa 'Bongo Fleva' Diamond Platnumz, alikamatwa kufuatia amri iliyotolewa Februari 16, 2018 na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda Maalum, Wilbard Mashauri iliyoelekeza kukamatwa mtuhumiwa huyo na ndugu yake, Idd Taletale.
Amri hiyo pia, ilielekeza watakapokamatwa wapelekwe Gereza la Ukonga wakiwa wafungwa wa kesi ya madai, hadi hapo mahakama hiyo itakapotoa maelekezo mengine.


Hata hivyo, Babu Tale hakuweza kupatikana na ndipo mahakama hiyo ikatoa amri nyingine kama hiyo Aprili 4 mwaka huu. Tangu hapo wamekuwa wakitafutwa bila mafanikio hadi jana alipokamatwa.
Mahakama hiyo iliwaamuru kumlipa Mhadhiri wa Dini ya Kiislamu, Sheikh Hashim Mbonde kiasi cha Sh250 milioni, baada ya kupatikana na makosa ya ukiukwaji wa haki za hakimiliki kwa kutumia masomo yake kibiashara bila ridhaa yake kinyume cha Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki.

Leo baada ya kufika mahakamani mbele ya Naibu Msajili, Ruth Massam, amewapa muda wa dakika 10 pande zote wajadiliane namna ya kulimaliza suala hilo.

Baada ya majadiliano hayo pande zote zilirudisha majibu kwamba hazikufikia maelewano yoyote.   Hivyo Naibu Msajili, Ruth Massam alichukua uamuzi wa kuiahirisha tena kesi hiyo na Babu Tale kurudishwa mahabusu Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam.

Katika kesi ya msingi, Sheikh Mbonde alikuwa akidai kuwa aliingia mkataba na kampuni ya kina Babu Tale (Tiptop Connection) ili wamrekodi mahubiri yake kisha wayauze na kugawana mapato.

Hata hivyo baada ya kurekodi masomo saba, walimkatia mawasiliano na alipowatafuta na kukutana nao wakamweleza kuwa wameamua kuachana na mpango huo.

Sheikh Mbonde alidai kuwa akiwa kwenye mahubiri Dodoma ndipo akakutana na mikanda ya video katika mfumo wa DVD yenye mahubiri yake huku kukiwa na namba za simu za viongozi hao wa Tiptop.

Sheikh Mbonde alidai baada ya kufanya uchunguzi alibaini kuwa DVD hizo zilikuwa zikiuzwa katika mikoa mbalimbali, ndipo akawafungulia kesi ya madai ya fidia kutokana ukiukwaji wa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki.

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako