Credit to Millardayo.com
MWANANCHI
Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa amesema anawatakia kila la heri wanaobeza nguvu ya umma.
Kutokana na umati wa watu waliojitokeza jana kumlaki kuanzia Uwanja wa Ndege wa Mwanza alikowasili saa saba mchana, iliuchukua zaidi ya saa mbili msafara wake kuingia Viwanja vya Furahisha saa tisa alasiri, ambako ni takriban kilomita nane.
Katika hotuba yake iliyochukua dakika 14 kuanzia saa 11.53 hadi 12.07 jioni, Lowassa alisema anawasikitikia wanaobeza nguvu hiyo ya umma.
“Haya siyo mapenzi, haya ni mahaba. Wanaobeza nguvu hii ya umma nawatakia kila la heri,” alisema Lowassa huku akishangiliwa na umati huo.
Akizungumzia idadi hiyo ya wananchi, mke wa mgombea huyo, Regina Lowassa alisema haijawahi kutokea maeneo yote waliyotembelea Dar es Salaam, Mbeya na Arusha.
“Mwanza nimewapenda, nafikiri baba (Lowassa) akitoka hapa atalala usingizi mzuri mzito,” alisema Regina.
Lowassa aliwataka polisi kutoingilia mchakato wa uchaguzi na kutumiwa na CCM kupambana na wapinzani na kwamba, wakiendelea watakuwa wanajitafutia tiketi ya kupelekwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), mjini The Hegue.
“Nimesikitishwa sana kuwa watu wamepigwa mabomu asubuhi. Mkiendelea na mchezo huu tukimaliza uchaguzi tutawapeleka The Hague mkakipate cha mtoto na huko hamtarudi tena,” alisema.
Polisi mkoani hapa jana walilazimika kutumia mabomu ya machozi, kuwatawanya wafuasi wa vyama vinavyounda Ukawa ambao walifurika Uwanja vya Ndege wa Mwanza kumpokea Lowassa.
Lowassa aliwasili akiwa ameambatana na mgombea mwenza, Juma Duni Haji, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, Kaimu Mwenyekiti wa CUF, Twaha Taslima na Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi.
Mabomu ya machozi yalianza kurindima saa tano asubuhi, baada ya baadhi ya wafuasi wa Ukawa kutaka kuingia kwenye lango la uwanja wa ndege, huku wengine wakijaribu kuwatunishia misuli polisi kwa kuwatupia mawe.
Hekaheka za mapokezi ya Lowassa zilianza saa mbili asubuhi, baada ya maelfu ya wafuasi wa Ukawa wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali ikiwamo: “Oil chafu ni kiboko ya mchwa” kutanda kwenye barabara inayoelekea uwanja wa ndege.
Msafara wa Lowassa kutoka uwanja vya ndege uliongozwa na pikipiki ambazo zilikuwa zinapeperusha bendera za vyama vya CUF, Chadema ,NCCR Mageuzi na NLD, huku viongozi hao wakiwa kwenye magari ya wazi.
Lowassa alisema ziara yake hiyo inahusu kujitambulisha na asingependa kuwapa nafasi wapinzani wake kumtafsiri kuwa hajui sheria, lakini kero za Mwanza anazifahamu hivyo akaahidi kurejea na mikakati ya kuzitatua.
Aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Mbunge wa Nyamagana, Lawrence Masha alisema: “Ndugu zangu nimerudi nyumbani, naomba niwaambie Watanzania wote kwa ujumla hapa tulipo tupo kwenye harakati za kuikomboa nchi yetu.
Leo nasimama hapa kama mwana Mwanza, lengo ni kuhakikisha tunapambana na kuikomboa Tanzania, naomba Oktoba 25 tufanye kazi moja tu ya kuchagua viongozi wa Ukawa.”
MWANANCHI
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku amesema Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeulea mtandao wa watu wasiopungua 10 ambao unaendelea kukitesa ndani na nje.
Butiku alisema hayo jana kwenye mdahalo wa maadili katika kuimarisha amani, umoja na haki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 ulioandaliwa na MNF na kubainisha kuwa mtandao huo usio na imani na CCM upo tangu kabla ya mwaka 1990.
“Wanasema ndani ya chama kuna mizengwe, hawataki utaratibu, hawataki waulizwe maswali, wanataka mambo yaendeshwe kiholela… wanasema tunachelewa kutajirika, sasa kama walikuwa wanajua hilo kwa nini hawakutoka tangu mwaka 1992,” alihoji Butiku na kushangiliwa.
Alisema Mwalimu Julius Nyerere aliwaruhusu mapema kuondoka CCM lakini walitega na wameendelea kukaa ndani ya chama huku wakivuruga kwa kutumia agenda ya vijana tangu miaka ya 1990.
“Hata Rais alipochaguliwa (Jakaya Kikwete) alisimamishwa na vijana Morogoro wakamwambia tumechoka. Sasa ndiyo maisha bora, sasa kuna maisha bora?” alisema Butiku na kuwataka wananchi watazame masilahi yao.
Butiku alimwambia Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula aliyehudhuria mdahalo huo chama hicho kilifanya makosa kutoudhibiti mtandao huo tangu awali na kwamba kimeuvumilia na sasa unakisumbua.
Kwa upande wake, Mangula alisema CCM siku zote inasimama kwenye misingi ya kanuni na taratibu na yeyote anayekiuka anashughulikiwa, akitolea mfano chama kilivyowafungia makada wake sita kwa miezi 12 baada kuanza kampeni za urais mapema.
NIPASHE
Miezi kadhaa baada ya kada wa Chama Cha Mapinduzi na Kamanda wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Kingunge Ngombale Mwiru, kuonyesha wazi kumuunga mkono aliyekuwa Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, katika mbio zake za kuusaka urais sasa ameanza kushughulikiwa ndani ya Chama.
Mzee Kingunge sasa amevuliwa wadhifa wake wa ulezi wa UVCCM, hatua inayothibitisha kuwa ni adhabu kutokana na kauli zake dhidi ya Chama kabla na baada ya Lowassa kukatwa jina lake na kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kugombea urais kwa niaba ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Akizungumza na Nipashe jana Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda, alisema kwa jinsi walivyompima Kingunge wameona hafai tena kuwa kamanda wa UVCCM kutokana na kauli zake na wanakiomba chama kumfuatilia kwa karibu.
Kushughulikiwa kwa Kingunge kumeanza kwa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM, kuazimia kumtema kwa nafasi ya ukamanda mkuu wa UVCCM kuanzia Agosti 15, mwaka huu, kwa kile wanachoeleza ni tabia na mwenendo wake wa hivi karibuni kwenda tofauti na maadili na taratibu za chama hicho.
Kingunge ni mwanasiasa mkongwe ambaye bila kumumunya maneno alikishutumu chama chake na kukitaadharisha juu ya rafu mbalimbali zinazochezwa kuwa zinaweza kukiangamiza chama hicho na kukichimbia shimo.
Bila woga alijitokeza jijini Arusha wakati Lowassa akitangaza nia na wakati wa mikutano ya kusaka wadhamini wa kuomba kuteueliwa na CCM kupeperusha bendera ya chama hicho, na kueleza kuwa ni lazima chama kisome alama za nyakati ikiwa ni pamoja na kumweka kada anayekubalika ndani na nje ya chama, kulelewa ndani ya chama kama ilivyo kwa Lowassa na kinahitaji mtu wa namna hiyo ili kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Baada ya Lowassa kukatwa alijitokeza hadharani na kueleza kuwa kitendo cha kumkata kimeacha kasoro kubwa ndani ya CCM.
Kingunge amekuwa mjumbe wa Kamati Kuu (CC), Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM, kipindi cha awamu zote kuanzia ya Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete sambamba na kuwa waziri.
Amewahi kuwa mkuu wa mikoa kadhaa na Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba.
Kingunge ambaye alikuwa Naibu Kamanda alipewa nafasi ya Ukamanda mwaka 2008 baada ya kufariki Mzee Rashidi Kawawa.
Mapunda alisema maamuzi hayo yalitolewa kutokana na tabia na mwenendo wake wa hivi karibuni kwenda tofauti na maadili na taratibu za CCM.
“Kikao kimetoa mapendekezo kwa vikao vya CCM kuuangalia upya uanachama wake na kuchukua hatua zaidi,” ilisema taarifa hiyo.
Alipoulizwa kuhusiana na maamuzi hayo ya UVCCM, Kingunge alisema kwa kifupi:“Aah wamefanya hivyo! sina taarifa hadi sasa, ndiyo nasikia kutoka kwako.”
NIPASHE
Waliokuwa wagombea ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika jimbo la Busega mkoani Simuyu, wamepinga matokeo ya marudio ya kura za maoni, katika uchaguzi uliorudiwa Agosti 13 mwaka huu yanayoonyesha kuwa Dk. Raphael Chegeni alishinda akifuatiwa na Dk. Titus Kamani.
Wagombea hao waliopinga matokeo hayo ni Nyangi Msemakweli, Robart Nyanda, Josephat Nkwabi, Desian Sweya na Igo Shing’oma kati ya wagombea nane walioshiriki kinyanganyiro hicho.
Walisema kuwa matokeo ya awali ambayo yalinyesha kuwa Dk. Kamani aliongoza kwa kura 12,896 dhidi ya Dk. Chegeni ambaye alipata kura 12,745, waliridhika nayo na walisaini, lakini walishangazwa na maamuzi yaliyotolewa na Chama ngazi ya Taifa kuwa warudie uchaguzi.
“Ni kweli tuliridhika kabisa na matokeo hayo ya awali, lakini hatukuelewa sababu za kurudia matokeo na tuliporudia makosa mengi yalijitokeza likiwamo suala la rushwa na upendeleo wa wazi kati ya viongozi wa wilaya dhidi ya Dk. Chegeni,” Sweya.
Shing’oma alidai kuwa wanayoyatambua ni matokeo ambayo waliyakusanya wenyewe kwenye vituo ambayo yanayoonyesha Dk. Kamani aliongoza kwa kura 12,852 dhidi ya Dk. Chegeni aliyepata kura 12, 664 kabla ya yale yaliyotangazwa na Katibu wa CCM wilaya.
“Hatukubaliani na matokeo haya ambayo yalichakachuliwa na viongozi wa wilaya, imani yangu Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, atatenda haki kwani tumeshampelekea malalamiko yetu,” alisema Shing’oma.
Hata hivyo, wagombea hao walitangaza msimamo wao juu ya kutokihama chama hicho kwa sababu mbalimbali na kudai kuwa ni chama pekee kinachoweza kuivusha nchi.
Mwishoni mwa wiki, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alikaririwa na vyombo vya habari akielezea kuwa malalamiko yote katika majimbo ambayo uchaguzi ulirudiwa Agosti 13 yanafanyiwa kazi kwa kuzingatia ngazi husika hadi Taifa kabla ya kutangazwa matokeo rasmi.
Nape alibainisha kuwa, Kamati kuu inatarajia kutangaza wagombea ubunge wa majimbo yaliyorudiwa uchaguzi huo leo.
NIPASHE
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema kuwa imeunda timu ya ushindi ya kuhakikisha matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu yanatangazwa kwa wakati, ya kweli na haki kwa pande zote.
Mkurugenzi wa Nec, Ramadhani Kailima, alisema timu hiyo itakuwa na wajibu mkubwa na hakuna kulala hadi matokeo yote yawe wazi.
“Tutakuwa na timu ya ushindi kutangaza matokeo yote mapema, hakuna kulala hadi tutoe matokeo kwa wakati, ya haki na kweli na yanayoaminika kwa wapigakura,” alisema.
Alisema malalamiko ya kupendelewa kwa chama chochote hayana msingi wowote kwa kuwa Tume haina chama na haitapendelea chama zaidi ya kuweka wazi matokeo yote itakayoyapata kwa wakati kwa kuwa watakuwa wanafanya kazi kisasa zaidi.
Alipoulizwa juu ya uzoefu wa Tume miaka ya nyuma kuhusiana na kuchelewesha matokeo hata ya maeneo ya mijini kunakofikika kirahisi, Kailima alisema kama kutakuwa na ucheleweshaji sababu zitawekwa wazi na wapigakura watatangaziwa bila kificho.
“Ya 2010, yasizungumziwe sasa kwa kuwa tunafanya kazi kisasa kuhakikisha matokeo yanakuwa wazi na kila hatua wananchi watatangaziwa,” alisema na kuongeza:
“Tunawaomba wananchi mara baada ya kupiga kura wakae mbali na ikiwezekana waende nyumbani kwa kuwa kila kituo cha kupigia kura kutakuwa na mawakala kama kuna tatizo lolote la kufanya matokeo yasitangazwe kwa wakati, watajulishwa mapema.”
Kailima alisema Nec iko huru na inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kanuni na haiingiliwi kokote kwani katika kugawa majimbo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kinadaiwa kubebwa na Tume, kimelalamika na kama wangekuwa wanapendelewa, ni wazi kuwa malalamiko yao yangesikilizwa, lakini Tume imeamua kufanya kazi zake kwa uhuru.
“Uhuru wetu siyo jina, bali ni kutekeleza majukumu ya kikatiba na sheria bila kuingiliwa, kiwe chama au mtu hawaruhusiwi kutangaza matokeo ya uchaguzi, bali msimamizi wa uchaguzi wa kata atatangaza ya kata, ubunge yatatangazwa na Mkurugenzi wa Manispaa, mji au halmashauri na Tume itatangaza matokeo ya urais,” alisema.
Alisema watumishi wote wa Tume kabla ya kufanya kazi huapishwa kujiondoa au kukana itikadi ya chama chake na kuanza kutekeleza majukumu yake ili kusiwe na upendeleo kutokana na itikadi.
Alipoulizwa kuhusu matukio kadhaa yaliyotokea katika uchanguzi mkuu wa mwaka 2010 ikiwamo wasimamizi wa baadhi ya majimbo mfano, Shinyanga mjini kutoroka baada ya kutangaza matokeo yenye utata yaliyompa ushindi mgombea wa CCM na kuzua vurugu, Kailima alisema:
“Tuko 2015, tumejipanga kikamilifu, ndiyo maana tuna timu ya ushindi kuhakikisha hakuna ucheleweshwaji wa matokeo. Itakuwa Tume tofauti na ya miaka mingine.”
HABARILEO
Mabasi maalumu kwa ajili ya kutoa huduma chini ya mradi wa mabasi yaendayo haraka yameingia nchini tayari kwa kuanza huduma.
Kampuni ya ubia ya UDART kwa kushirikiana na wakala wa mabasi yaendayo haraka (DART) inaanza leo kuendesha mafunzo kwa madereva kabla ya huduma ya usafiri kuanza rasmi Oktoba.
Mabasi mawili yaliyoingizwa nchini ndiyo yatatumiwa katika mafunzo hayo.
Jana mabasi hayo yenye uwezo wa kubeba abiria wapatao 190 na jingine la abiria 100, yalipitishwa kwenye njia yake kuanzia Kivukoni hadi Ubungo na umma kutambulishwa juu ya mafunzo hayo leo.
“Kesho (leo) tunazindua mabasi mawili kwa mafunzo. Wakufunzi wametoka China…huduma kamili inaanza Oktoba,” Alisema Meneja wa Udart, Sabri Mabruk katika mkutano na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari.
Ujio wa mabasi hayo na kuanza kwa huduma za BRT, kwa mujibu wa Mabruk, ndiyo mwisho wa daladala za kawaida kati ya Kimara na Kivukoni.
Alisema kutakuwa na utaratibu wa kulipa gharama za usumbufu kwa wenye mabasi na kisha kuwapangia njia nyingine.
Idadi ya mabasi yanayotarajiwa kutoa huduma chini ya mradi, ni 76.
Mabruk alisema mwezi ujao ndio watajua ni mabasi mangapi mengine yataletwa. Baada ya mafunzo ya wiki mbili kwa madereva, mabasi yaliyoko yatatoa huduma kupitia vituo 10 pekee kabla ya Septemba ambayo idadi ya mabasi itakuwa imekamilika.
Mabasi hayo yanayotarajiwa kutumia dakika 20 kutoka Kimara hadi Kivukoni eneo la Magogoni, ndani yana viti kwa ajili ya wazee, wajawazito na wenye ulemavu.
Pia yana mikanda maalumu ya kushika kwa abiria wanaosimama. Vile vile ilielezwa hayatakuwa na makondakta wala wapiga debe kutokana na mfumo wake wa kisasa wa ukusanyaji nauli.
HABARILEO
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam jana kimetangaza majina ya wagombea udiwani katika majimbo 10 ya uchaguzi huku ikiwaengua, Yussuf Manji na Diwani wa Kata ya Jangwani Abuu Jumaa.
Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Simba alitangaza wagombea wa udiwani kwa tiketi ya CCM wa kata 91 huku kata moja ya Mianzini katika Jimbo la Mbagala uchaguzi wake utafanyika baadaye baada ya ule wa wali kuvurugika.
“ Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa ndiyo yenye dhamana ya kupitisha majina ya wagombea wa nafasi ya udiwani, baada ya kupokea majina na baadaye kupitia na kuhakiki malalamiko yote,” alisema Simba.
Katika kata ya Mbagala Kuu ambayo Mwenyekiti wa Yanga, Manji aliongoza katika kura hizo alikatwa na Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam kutokana na kukosa sifa na nafasi kuchukuliwa na mgombea aliyeshika nafasi ya pili Abubakari Othuman.
Kwa upande wa kata ya Jangwani ambayo wananchi walilalamika Diwani wa kata hiyo, Jumaa kwa kuongoza tangu enzi za utawala wa awamu ya kwanza, jina lake limekatwa na kupitishwa la mgombea aliyeshika nafasi ya pili Abdul Faraji.
Aidha, akizungumza malalamiko ya wanachama wa CCM kata ya Mbagala Kuu ambao walifika ofisini hapo kwa basi maalumu kupinga kuenguliwa, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida alisema Manji amendolewa kutokana na kukosa sifa.
“ Manji hakutokea kuchukua fomu wala kurudisha fomu, lakini hilo sio tatizo, wakati wa kampeni tuliweka utaratibu wa wagombea kutumia usafiri mmoja kwenye kuomba kura kwenye matawi, Manji hakushiriki. “
Hata wakati wa vikao vya mchujo vya Sekretarieti na kamati ya usalama na maadili ngazi ya kata na wilaya, Manji hakutokea na alipopigiwa simu alijibu amelala.
Alisema kutokana na kutofuata taratibu hizo Manji anakosa sifa za kuwania nafasi ya udiwani, kuwa kura alizopata amezipata kwa hila hivyo sio halali.
HABARILEO
Mmoja wa makada wa CCM aliyewania kuteuliwa na chama hicho kuwania Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Dk John Nchimbi, ameibuka na kudai kuwa, hana kinyongo na yaliyotokea Dodoma huku akionesha kuwashangaa wanaoendelea kunung’unika, akisema watu wa aina hiyo hawakuwa pamoja na chama.
Aidha, Nchimbi, mmoja wa makada vijana waliokulia katika mfumo wa kisiasa ndani ya CCM alikoshika nyadhifa mbalimbali zikiwemo Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Mkuu wa Wilaya, Mbunge na Waziri, amesema sasa si wakati wa kuendelea kuwa na makundi, bali kujenga umoja kwa lengo la kukipa chama ushindi.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la UVCCM jijini Dar es Salaam.
Nchimbi ambaye tangu baada ya uteuzi wa mgombea wa urais wa CCM amekuwa kimya, ikiwa pamoja na kutojitokeza kuwania ubunge katika jimbo lake la Songea Mjini na hata kuhusishwa na mpango wa kukihama chama, amesisitiza hana kinyongo, bali anaunganisha nguvu zake na WanaCCM wengine kuhakikisha ushindi wa Dk John Magufuli, Waziri wa Ujenzi aliyepewa jukumu la kupeperusha bendera ya CCM katika urais.
Alisema ndani ya UVCCM, umoja huo umekubaliana kumaliza makundi na kwamba hivi sasa wapo kitu kimoja kwa ajili ya ushindi wa CCM. Kikwete na Magufuli Naye Rais Jakaya Kikwete, akizungumza katika baraza hilo, alisema chama hakikukosea kumteua Dk Magufuli kwani ni mtu mzuri na anayejiamini.
“Chama kimepata mtu ndiye, sina wasiwasi naye ni kiongozi anayejiamini,”Rais Kikwete.
Aliwataka wanachama wa umoja huo wajenge umoja wao na waachane na mchakato wa urais kwani umemalizika.
“Ukiendelea kubaki kwenye mchakato, basi wewe akili yako mbaya kwani mchakato wa kumpata urais ndani ya chama umeisha na hauwezi kurudiwa,”Rais Kikwete.
Alisema kuna watu waliamini chama kingegawika vipande baada ya mchakato wa kura za urais, lakini haikutokea kwa sababu CCM ni chama kikubwa.
Rais Kikwete alisema waliotoka kwenye chama wanatoka wenyewe, lakini wote walikuwemo kwenye Mkutano Mkuu walikubaliana wote.
Alisema chama kina wagombea wazuri kwa nafasi ya urais, ubunge, uwakilishi na udiwani na kwamba waliwachagua viongozi hao kwa umakini mkubwa.
“Sisi hatuhangaiki nao, tumejipanga namna ya kuwashinda na hatuna sababu ya kushindwa,” alisema Rais Kikwete ambaye baada ya Dk Magufuli kuchukua fomu ya uteuzi kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, alieleza kuwa CCM si chama cha mchezo na wanaodhani hivyo watakiona cha mtema kuni.
Hata hivyo, Rais Kikwete aliwataka viongozi wa umoja huo kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuhakikisha chama kinapata ushindi.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM, Sadifa Juma Hamisi, ameendelea kutetea uamuzi wa CCM wa kutompitisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwa mgombea urais kupitia chama hicho, akidai alipoteza sifa ya kuwa Rais tangu enzi za Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Akifungua Baraza Kuu la UVCCM, Dar es Salaam juzi, Sadifa alisema makada wanaohama chama na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), walipoteza sifa za uongozi tangu enzi za Mwalimu Nyerere.
Sadifa alisema Lowassa ambaye ni mgombea urais wa Chadema, alipoteza sifa ya kuwa rais tangu enzi za Mwalimu Nyerere na kwamba dhamira yake hiyo haitafanikiwa milele.
Aliongeza kuwa, umoja huo haushtushwi na wimbi la wanasiasa maslahi wanaohama chama. Sadifa alisema vijana wa CCM wamejipanga kuueleza umma udhaifu wa wanasiasa hao.
“Hatutatishwa na watu wanaotumia fedha zao kusaka madaraka. Tumeamua kuvunja makundi yetu na tutaeleza uchafu wote…,” alisema Sadifa ambaye inaaminika alikuwa akimuunga mkono Lowassa kuwania urais ndani ya CCM.
Alisema umoja huo utashirikiana na chama, kuhakikisha Mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli anapata ushindi mkubwa.
Alisema mwaka huu, umoja huo utawadhihirishia wote wanaodhani chama ni uso wa mtu wakisahau kuwa ni taasisi kwa kukipa ushindi wa kishindo kwenye nafasi zote za uongozi.
Alisema CCM imepata mgombea makini na kwamba hana dosari wala hakuna sababu ya kutafuta sabuni ya kumsafisha.
Sadifa alisema Rais Jakaya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM aliendesha vikao vya Chama kwa umahiri mkubwa.
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako