Kwa ufupi
Mwigulu alitoa kauli hiyo pale alipoingilia kati
mjadala huo, akiponda kitendo cha watumishi wa Serikali kutumia magari
na fedha lukuki katika wiki za kuadhimisha kumbukumbu mbalimbali za
kitaifa.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba juzi
alijikuta akitamka kuwa anakusudia kufuta maadhimisho mbalimbali ya
kitaifa yanayotumika kama kichaka cha kutafuna fedha za Serikali baada
ya wabunge wa upinzani kuitoa jasho Serikali wakati wa kupitisha
Muswada wa Sheria ya Baraza la Vijana wa mwaka 2015.
Mwigulu
alitoa kauli hiyo pale alipoingilia kati mjadala huo, akiponda kitendo
cha watumishi wa Serikali kutumia magari na fedha lukuki katika wiki za
kuadhimisha kumbukumbu mbalimbali za kitaifa.
Kilichoibua mjadala
huo ni suala la uanzishwaji wa Mfuko wa Vijana na maadhimisho ya wiki ya
vijana ambayo imepangwa Oktoba kila mwaka.
“Napendekeza wiki hii
(ya Mfuko wa Vijana) iondolewe mwezi Oktoba kwa sababu ndani ya wiki
hiyo pia kuna maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere na
kuhitimisha mbio za mwenge,” alisema Mbunge wa Ubungo (Chadema), John
Mnyika.
Kauli ya Mnyika iliungwa mkono na Mbunge wa Singida
Mashariki (Chadema), Tundu Lissu aliyesema si jambo la busara kuiweka
siku hiyo sawa na kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere.
“Kila mtu hapa anajua jinsi siku ya kilele cha mwenge yanavyofanyika mambo mabaya. Hatulitaki jambo hili,” alisema Lissu.
Msimamo
huo ulimnyanyua Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,
Juma Nkamia na kusema kuwa hata Mwalimu Nyerere alikuwa kijana wakati
akifanya harakati za kulikomboa Taifa, si vibaya kama Wiki ya Vijana
ikaadhimishwa mwezi huo.
Kwa nyakati tofauti Mawaziri Jenister
Mhagama, Mary Nagu, Dk Fenella Mukangara na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, George Masaju walisimama kuitetea hoja hiyo bila mafanikio.
Wakati
mvutano ukizidi kuwa mkali, alisimama Mwigulu na kusema: “Mimi nina
mawazo tofauti kidogo. Nadhani umefikia wakati wa kufikiri tofauti na
kuachana na hizi kumbukumbu za wiki ya maafa, wiki ya mtoto wa jicho,
wiki ya kichaa cha mbwa, wiki ya maziwa, sijui kunyonyesha… sijui wiki
ya nini. Nikiwa...”(akakatishwa na Mwenyekiti wa Bunge Zungu).
Mwigulu
alisema katika maadhimisho hayo watumishi wa Serikali hutumia mamilioni
ya fedha na magari ya Serikali kushiriki, kuifanya Serikali kutumia
fedha nyingi katika mambo ambayo si ya msingi sana.
“Kuna
maadhimisho Mtwara watendaji kutoka Mwanza wanakwenda. Sijui kuna
shughuli Kigoma watu wanatoka Dar es Salaam. Tufikie wakati tuachane na
hizi wiki na tubaki na maadhimisho ya muhimu,” alisema.
Akifafanua
baadaye jana, Mwigulu alisema, “Nililenga kuonyesha jinsi fedha
zinavyotumika hovyo. Unajua katika maadhimisho haya, watu wanatengeneza
fulana, kofia na mambo mengine mengi. Sidhani kama ni sahihi.” Alisema
kuna mambo mengi ya msingi yanayohitaji kufanyika lakini fedha
zinakosekana, kama maadhimisho ya wiki yakiangaliwa kwa umakini, fedha
nyingi zinaweza kuokolewa.
Alipoulizwa alitaka kusema nini
aliposema niki... alisema kuna kitu alitaka kusema lakini hakumalizia,
ingawa hoja yake ilikuwa kusisitiza kuwa fedha nyingi za Serikali
zinatumika vibaya katika maadhimisho hayo.
Hata hivyo, pamoja na
kauli hiyo, Mwigulu alipohitimisha kauli hiyo bungeni alipondwa na Lissu
na Mnyika wakisema kuwa kauli yake haikutakiwa kutolewa na mtu kama
yeye, kwamba licha ya kuwa ni waziri mdogo, pia anataka kugombea urais
katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Mvutano huo haukufikia
mwafaka na kumlazimisha Zungu kulihoji Bunge kama linakubaliana na hoja
ya wapinzani. Kutokana na wingi wa wabunge wa CCM, hoja ya Serikali ya
kuanzisha mfuko katika baraza hilo iliungwa mkono.
Hata hivyo, baadhi ya watu wametafsiri kuwa Mwingulu aliposita na kutamka nikiwa.. alitaka kusema nikiwa Rais.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako