Hivi karibuni kumezuka taarifa za upotoshwaji zilizotolewa kwenye
mitandao ya kijamii kwamba Serikali ya Tanzania imemteua Bw. Salaah,
Mkurugenzi wa Home Shopping Centre, (pichani ) kuwa Konseli wa Heshima
(Honorary Consul) kwenye mji wa Guangzhou kwenye Jimbo la Guandong.
Watoa taarifa hizo, hawakutoa ushahidi wowote kuthibitisha madai yao
zaidi ya kutoa picha mbalimbali za Bw.Salaah kutoka kwenye mitandao
mingine ya kijamii.
Taarifa hizo sio za kweli.
Kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za mahusiano ya kidiplomasia ya China,
nafasi ya Konseli wa Heshima haitambuliki 'mainland' China. Kwa maneno
mengine hakuna nchi yoyote duniani inayoweza kuteua mtu kuwa Konseli wa
Heshima katika eneo lolote la China isipokuwa Hong Kong ambako kuna
mamlaka huru za utawala zinazofuata sheria zake.
Kwa faida ya umma, ni vema kufafanua kwamba Nchi ya China inakubali nchi
za Nje kufungua Ubalozi kamili (Embassy) ambao makao yake yanatakiwa
kuwepo katika mji Mkuu wa China- Beijing na Konseli Kuu ama kwa lugha
iliyozoeleka Ubalozi Mdogo (General Consulate) ambao unaweza kufunguliwa
kwenye makao Makuu ya mji wowote ule katika Majimbo ya China.
Watu wengi wamekuwa wakichanganya Ubalozi Mdogo au Konseli Kuu (General
Consulate) na Konseli (Ubalozi) wa Heshima (Honorary Consulate).
Konseli Kuu (General Consulate) ni sehemu ya Ubalozi (ndio maana wengi
huuita Ubalozi Mdogo) ambapo kiongozi wake na maafisa wake wote ni
watumishi wa Serikali kutokea Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa. Masharti ya kuwa Mkuu wa Konseli 'General Consulate' lazima
uwe Afisa Mwandamizi wa Mambo ya Nje mwenye uzoefu usiopungua miaka 10
ya Utumishi katika Wizara ya Mambo ya Nje.
Kwa muktadha huo, taarifa kwamba Bw.Salaah ameteuliwa kuwa Balozi wa
Heshima wa Tanzania huko Guangzhou sio kweli kwasababu Sheria za China
haziruhusu uwepo wa nafasi hiyo. Aidha, Bw Salaah hawezi kuwa Balozi
Mdogo (Consul General) kwa kuwa yeye sio mwajiriwa wa Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Hivyo habari zinazosambazwa kwenye
mitandao ya kijamii sio za kweli na zinalenga kuupotosha umma.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
WIZARA YA MAMBO YA
NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
OCTOBER 30, 2014
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako