A

A

Lundenga na Miss Tanzania wajikoroga


Miss Tanznia 2014, Sitti Mtemvu akifafanua kuhusu utata wa umri wake jana jijini Dar es Salaam. Picha na Said Khamis. 
Kwa ufupi
Sitti alijikuta kwenye wakati mgumu alipotakiwa kueleza mahali kilipo cheti chake cha awali cha kuzaliwa baada ya kile alichopeleka kwenye kamati ya Miss Tanzania kuonyesha kimetolewa, Septemba 9, 2014.

Dar es Salaam. Utata umezidi kutanda kuhusu
Miss Tanzania 2014, Sitti Mtemvu ambaye amejikoroga katika juhudi zake za kujitetea kwenye kashfa inayohusu umri wake.
Sitti alijikuta kwenye wakati mgumu alipotakiwa kueleza mahali kilipo cheti chake cha awali cha kuzaliwa baada ya kile alichopeleka kwenye kamati ya Miss Tanzania kuonyesha kimetolewa, Septemba 9, 2014.
“Cheti changu cha awali kilipotea, hiki ni kipya nimekitengeneza,” alisema Sitti ambaye alipotakiwa kueleza ni kituo gani cha polisi alikoenda kuripoti baada ya cheti chake cha awali kupotea, alijibu kuwa hakikumbuki kwani hakujiandaa kuulizwa maswali hayo.
Sitti aliingia kwenye tuhuma ya kudaiwa kudanganya umri siku chache baada ya kutwaa taji hilo kwa kuwabwaga wenzake 29 katika fainali iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam .
Pasipoti na leseni ya udereva, zenye picha za mrembo huyo zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha alizaliwa 1989 na siyo 1991 kama alivyosema alipoingia kwenye kambi ya Miss Tanzania.
“Nimekuwa nikisakamwa baada ya kutwaa taji, lakini ukweli ni kwamba nilizaliwa Mei 31, 1991, Temeke Dar es Salaam, kuna mambo yanazungumzwa, mengine ya uongo mengine ya ukweli, lakini vitambulisho vinavyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, watu wanayafanya hayo ili kunipakazia,” alisema mrembo huyo ambaye hakuwa tayari kuzungumzia madai mengine yanayomkabili.
Hata hivyo, mwenyekiti wa kamati ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga alimkingia kifua kwa kusema mrembo huyo hatavuliwa taji kutokana na cheti alichopeleka kwao kuonyesha alizaliwa Mei 31, 1991 na siyo 1989 kama inavyodaiwa.
Lundenga, alisema kanuni za mashindano hayo zinamtaka mshiriki asiwe na umri chini ya miaka 18, wala asizidi miaka 24.
Umri mkubwa
Lundenga alisema, wanachokiamini wao ni cheti cha kuzaliwa cha mrembo huyo kilichotolewa na Wakala wa Serikali wa Vizazi, Vifo na Ufilisi (Rita) na si vinginevyo.
“Mrembo kuwa na miaka 25 siyo hoja, kwenye mashindano ya dunia (Miss World) wapo warembo wa nchi nyingine waliowahi kushiriki na miaka 25 ijapokuwa sisi hatujawahi kupeleka mrembo mwenye umri huo.”

No comments:

Post a Comment

Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako