Hekalu la Freemasons lililopo katika Mtaa wa Sokine jijini Dar es Salaam
Wamekuwa wakitajwa kwenye kila aina ya minong’ono. Tumeona
matangazo yakialika watu kujiunga nao kama wanataka kupata utajiri na
kuwa watu wenye nguvu. Lakini bado Freemason, imebaki kuwa kitendawili
miongoni mwa Watanzania wengi.
Leo tunakuletea habari kuhusu Mtanzania maarufu
aliyefungua kinywa na kueleza namna alivyojiunga na Freemasons, kundi
lililo kongwe duniani.
Tayari watu mbalimbali watu wenye hamu ya kupata
utajiri wamekuwa wakitoa ushuhuda kuhusu kundi hilo na kusikika kwenye
vyombo vya habari, hasa baada ya kifo cha mwingizaji nyota, Stephen
Kanumba, mwaka 2012.
Siyo hivyo tu, bali kumeibuka pia matangazo yenye
namba za simu yanayoshuhudiwa kwenye nguzo za simu mitaani hadi
vichochoroni yakiwataka watu wanaotaka kujiunga na Freemason kupiga simu
ili wapewe utaratibu wa namna ya kujiunga kwenye ‘kisima hicho cha
mafanikio’.
Baadhi ya watu tayari wameshanaswa na mtego huo,
huku wengine wakiendelea kujaribu bahati yao kujipatia utajiri kwa njia
ya ‘nguvu za giza’.
Hata hivyo Jayantilal Keshavji Chande, maarufu
zaidi nchini kwa jina Sir Andy Chande, aliyejiunga na Freemason Oktoba
25, 1954 baada ya kupita kwenye usaili mzito, anaeleza namna alivyoibuka
kutoka familia ya kawaida hadi kuwa kiongozi wa Freemason Afrika
Mashariki.
Sir Andy Chande, ambaye amekuwa mwanachama wa
kundi hili kwa karibu miongo sita sasa, anaeleza namna alivyosajiliwa na
kufikia hatua ya juu ndani ya kundi hilo.
Chande alizaliwa Mombasa Kenya, Mei 7, 1928,
ingawa wazazi wake walikuwa wakiishi Bukene mjini, mkoani Tabora,
magharibi mwa Tanzania.
Katika kufafanua utaratibu mzima wa Freemason,
Chande ameandika kitabu alichokiita; ‘A night in Africa-a journey from
Bukene’ (Usiku wa Afrika-Safari kutoka Bukene), pengine akitaka kuweka
sawa dhana na kuondoa tofauti ili misingi inayoendesha Freemason
ifahamike.
Imani ya kimaadili na thamani ya kundi hilo
ilianza wakati wa mazungumzo yake na Messrs Campbell Ritchie na McLean
mwanzoni mwa miaka ya 1950.
“Katika kipindi kile nilianza kutambua kuwa
Freemason ipo katika msingi wake. Ni sayansi ya maisha ambayo malengo
yake ni kumbadilisha mtu kiimani na kumfanya awe anavyopaswa kuwa. Ni
mabadiliko ya mtu binafsi,” Sir Andy Chande ameandika katika kitabu
chake chenye kurasa 207.
Anasema kuwa malengo ya Freemason yamefunikwa na
mafumbo, ambayo pengine ndiyo yanayoeleza utamaduni uliojificha katika
utendaji kazi wake.
Chande anabainisha kuwa kanuni kubwa tatu za Freemason
ziliandikwa kwenye kitabu kimoja nchini Canada, kilichochapishwa na
Kampuni ya Penumbra Press.
Anaandika: “Kwa hiyo, ukiwa kwenye ngazi ya kwanza
(first degree), kanuni inayoongoza, inamtaka mtu awe mkweli na mwenye
maadili ambayo hasa Freemason inalenga kuyaweka kwenye akili, ili
mwanachama awe mzuri.
Ngazi ya pili ya utaratibu inatilia mkazo kwenye
vipaji na akili kupitia sanaa na sayansi, ili kutoa mchango mzuri
iwezekanavyo kwenye maisha.”
Anafafanua kuwa ngazi ya tatu inampa mtu nafasi ya
kutafakari uwepo wake kwa kina na kwamba kanuni zote tatu zinafahamika
kama upendo wa kindugu, kujiweka huru na ukweli.
“Kwa njia hizi inamaanisha, unafundishwa namna ya
kuyafurahia maisha kwa kiwango chake cha juu. Kwa kufuata hizo kanuni
tatu za upendo wa kindugu, kujiweka huru na ukweli, wakati huohuo
ukijitambua na kuanza kujiandaa na kutokwepeka kwa kifo,” anaandika
Chande.
Anaongeza kuwa, wakati kanuni hizo tatu
zinapoondolewa kwenye alama ya sanaa inayofunika imani ya Freemason,
ambazo zilimpa udadisi wa kupata taarifa kuhusu utaratibu huo wa kale.
Sir Andy Chande ni Kiongozi wa Freemason Afrika Mashariki.
Kanuni za Freemason zinafundisha nini?
Katika ratiba ya Freemason, anaandika Chande
akieleza kuwa, kanuni ya upendo wa kindugu inawafundisha ndugu wote
kuwachukulia wanadamu wote kama familia moja iliyoumbwa na nafsi moja
kuu.
“Kujiweka huru, vilevile, inaleta ujumbe
nilioupata kutoka kwa baba yangu, aliyesema ni kuwekwa huru kwa mtu
mwenye msongo. Kama ni kuwekwa huru kutoka kwenye umaskini, matatizo au
akili isiyo na furaha,” anaandika Chande katika kitabu hicho.
Anafafanua kuwa ngazi ya tatu ambayo ni ukweli na pengine ndiyo muhimu zaidi ni mchango wa kimungu kwa mwanachama wa Freemason.
Anabainisha kuwa kipindi hicho ndicho
kinachoheshimika kama njia ya matazamio na marekebisho na kama
inawezekana, kurudiwa kwa kanuni hizo kama msingi wa kuelekea kanuni kuu
nne alizozitaja kuwa ni; udhibiti binafsi, nguvu, umakini na haki
Chande anaeleza kuwa Freemason siyo kifaa cha dini, pia siyo
mpinzani wa dini, lakini inakaribisha watu wote bila kujali dini zao na
haijaribu kubadilisha imani zao au kushawishi kuabudu kwao.
“Inajaribu tu kuwafanya watu kuwa wema,” anaandika Sir Chande akifafanua:
“Hii ndiyo dunia niliyoingizwa mwaka 1954, imekuwa
na mchango mkubwa katika maisha yangu tangu wakati huo…: Roho yangu,
akili yangu na nafsi yangu, vimetajirishwa na kushiriki kwangu
Freemason.
Chanzo;Mwananchi
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako