Suruali ya mtuhumiwa huyo ikiwa imezungushiwa Cocaine. (picha: Francis Dande) |
Baadhi ya dawa alizokuwa amemeza mtuhumiwa huyo. |
DAR ES SALAAM, Tanzania - KIKOSI cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini kinamshikilia Andres Filipe Ballesteros Uribe (28) raia wa Colombia kwa tuhuma za kuingiza dawa hizo nchini kinyume cha sheria.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo, Mkuu wa kikosi hicho, Kamanda Godfrey Nzowa alisema mtuhumiwa huyo aliingia nchini saa nane usiku kwa ndege ya shirika la Ethiopian akitokea Adisi Ababa.
Alisema mtuhumiwa huyo alikutwa na Cocaine iliyofungwa kwenye pakiti sita tofauti na kuiweka sehemu za siri, kiunoni kama mkanda na nyingine tumboni.
Kamanda Nzowa alisema mtuhumiwa huyo mwenye pasi ya kusafiria namba AP816263 iliyotolewa Julai 3,2014 nchini Columbia, alitoka Columbia kupitia Adis Ababa kuja Tanzania huku akibainisha kwamba hiyo ni njia mpya ya usafirishaji wa dawa hizo haramu.
“Hawa jamaa wanajaribu kubuni mbinu mpya kama huyu kijana alikuwa amefunga unga wa cocaine kama zilivyokuwa zikifungwa pipi na akazimeza… mpaka sasa ameshatoa pipi 13 kwa njia ya haja kubwa na anaendelea kutoa.
“…Sio rahisi kujua idadi ya mzigo aliokuwa nao mpaka atakapomaliza kuzitoa zote za tumboni ndiyo tunaweza kusema uzito wa dawa hizo na thamani yake,” alisema kamanda Nzowa.
Alisisitiza kwamba taarifa sasa wanazopeana kwenye mtandao wao unawezesha kukamatwa kwa watuhumiwa huku akibainisha kuwa lengo ni kudhibiti usafirishaji kwa njia yoyote.
Kamanda Nzowa alisema mafanikio yanaonekana kwa vile kuanzia Juni 24 mwaka huu hadi Agosti 10 hakuna mtu aliyekamatwa akiingiza huku akibainisha kwamba umadhubuti wa mtandao wao umefanikisha hilo.
“Asiyeamini kwamba tumefanikiwa atujaribu aone… naamini tunakokwenda dawa za kulevya hasa cocaine na heroine zitakuwa hazipiti wala kuingia Tanzania,” alisema na kuongeza kwamba wanadhibiti pia ulimaji wa bangi.
Kwa mujibu wa kamanda huyo lengo la mtandao wao ni kudhibiti sio kukamata wala kuteketeza.
Hati ya kusafiria ya mtuhumiwa huyo yenye namba AP816263 iliyotolewa Julai 3,2014 nchini Columbia. (picha: Francis Dande) |
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako