MWIGULU NCHEMBA
ACHOMOZA URAIS 2015
..Wasomi, diaspora, wakulima, wafugaji wajitokeza kumhitaji
Na Mwandishi Wetu
ACHOMOZA URAIS 2015
..Wasomi, diaspora, wakulima, wafugaji wajitokeza kumhitaji
Na Mwandishi Wetu
Mwigulu ambaye pia ni Naibu Katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) (bara), ameombwa na baadhi ya viongozi wa dini, wakulima, Wafugaji, Walimu, vijana wa vyuo vikuu na Watanzania waishio Marekani na Uingereza, pamoja na mitandao ya kijamii.
Makundi hayo yamewasilisha maombi yao kwake hivi karibuni kupitia matamko na kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu kadhaa vya habari, hatua hiyo ya kumuomba Mwigulu atangaze kugombea urais 2015, imekuja baada ya kuonekana kuwa ni kijana mwenye elimu ya kutosha, ari na uwezo wa kupeperusha bendera ya chama chake katika kinyang’anyiro hicho.
Habari zaidi zinasema kuwa watanzania masikini, wafugaji, wakulima, vijana kote nchini tayari wametangaza dhamira yao kusimama na kuhakikisha Mwigulu anachukua fomu ya kugombea urais 2015.
Hata hivyo , baadhi ya makundi hayo wamesema kuwa endapo hatochukua fomu watachukua wao, kumjazia na kuitembeza nchi nzima ili apate udhamini aweze kuwa mkombozi wao kwa miaka 10 ijayo.
Hatua ya watu hao imefikiwa pia kwa kutambua na kuthamini jitihada za kiongozi huyo za kupigania maslahi ya watanzania wote hususani maskini.
Kwa mujibu wa habari hizo, mwenendo wa Mwigulu Nchemba alimaarufu mtoto wa mfugaji tangu aingie kwenye siasa umewagusa watanzania wengi wa tabaka la chini walioonekana kukata tamaa kufuatana na kile walichokiita kusahaulika kwao.
Mwigulu anayefananishwa na aliyepata kuwa Waziri Mkuu, Marehemu Edward Sokoine kwa msimamo wake mkali juu ya wakwepa kodi na wenye matumizi mabaya ya fedha za wavuja jasho, ambao wakati wa Sokoine wakiitwa wahujumu uchumi, amejipambanua kwa ujasiri na uzalendo wake kwa vitendo.
Hivi karibuni Mzee Aloyce Kimaro, Mbunge wa zamani wa Jimbo la Vunjo aliwahi kumsifu Mwigulu akisema kuwa ni kijana anayestahili kuongoza nchi.
“Huyu kijana anastahili kuongoza hii nchi, maana ana ujasiri sana. Haogopi kumkemea mtu yeyote. Alipomkemea Mbowe (Freeman) nilidhani ni uchama, sasa alipopewa wizara ya fedha amefanya mengi yenye ujasiri, aliwambia waziwazi wabunge wa bunge la katiba wakiwemo wa CCM kuwa anayeona laki tatu kwa siku haitoshi achukue begi lake aende zake,” Kimaro alisema.
Kwa mujibu wa Kimaro, vyombo vya habari viliripoti kuwa timu ya wataalamu walipanga kila mbunge apewe shilingi laki 8, kwa siku na kiinua mgongo cha shilingi milion 5, kwa kila mbunge.
Aliongeza kuwa Mwigulu alipoteuliwa alikataa kuwalipa viwango hivyo vya fedha na kubaki na laki tatu huku akisema kuwa hawa ni watanzania na katiba ni ya Tanzania, hatujakodisha wataalamu kutoka Kenya, Uganda au Marekani kuja kutengeneza katiba yetu.
“Tumesikia pia jinsi alivyowakoromea Wizara ya Fedha na Benki kuu kuhusu mabilioni ya escrow akiwauliza zilitokaje? Zililipiwa kodi?” alisema Kimaro.
Naye Mhe. Lekule Laizer alisema anamfananisha Mwigulu na Sokoine kwani kuna wakati alikwenda naye Loliondo wakati wafugaji waliponyang'anywa sehemu za malisho, ambapo alisema mbele ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwa wafugaji warudishiwe sehemu ya malisho yao.
Naye Ndugu K. Mrashani, Mwenyekiti wa wafugaji Kanda ya Ziwa, alisema anamuona Mwigulu kama vile Nyerere amefufuka.
“Kumbe kisima cha Nyerere bado hakijakauka. Huyu kijana anayajua maisha halisi ya watanzania masikini, wafugaji , wakulima, watoto wa masikini wanaokosa mikopo na wale wasio na ajira,” alisema mwenyekiti huyo.
Mrashani alisema kuwa endapo Mwigulu atachukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama chake kuwania urais, wao (wafugaji) watauza ng'ombe ili wampatie fedha za kufanyia kampeni.
Habari kutoka Chama cha Wakulima, Ruvuma, kupitia kwa mwenyekiti wao ndugu Mhagama, zinasema Mwigulu aliposema wakulima wasizuiwe tena kuuza mazao yao nje ya nchi, wengi walitokwa machozi.
“ Aliposema kuwa kuwazuia wakulima kuuza mazao nje ni kuwatia umasikini ni kweli. Mazao yetu magunia kwa magunia yalinyeshewa mvua. Yaani Mungu amemwinua kijana huyu tokea tabaka la masikini ili atusaidie maana kuna viongozi hawajui mateso ya watu masikini hapa,"alisema Mzee Mhagama.
Kwa upande wa vijana hususani Vijana wa CCM kumekuwepo na shinikizo kubwa wakitaka Mwigulu achukue fomu ya Urais Mwaka 2015.
Kwa mfano shirikisho la vyuo Morogoro, Ruvuma, Mbeya, Iringa, Singida, Mwanza, Dodoma, Kilimanjaro na Arusha kwa nyakati tofauti wametoa matamko kuwa watazunguka nchi nzima kumpigia kampeni Mwigulu awe Rais kwani ndiye mtu aliyeonesha kuguswa na kero zinazo wahusu vijana na kuja na mapendekezo ya namna ya kutatua.
Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) na wale vyama vingine kwenye Mitandao ya Kijamii wamekuwa wakimjadili Mwigulu kama tegemeo lao kwenye utatuzi wa mambo mbalimbali ya taifa hili kwa sababu ana uthubutu wa kuchukua hatua.
Wengi wameona namna alivyofanya kazi kubwa ya kung'oa vigogo waliokuwa wananufaika na misamaha ya kodi ilihali kuna vijana hawana mikopo vyuoni, na viwanda havijajengwa kwa sababu fedha zinaishia kwa watu wachache.
Kuhusu mikopo ya elimu ya juu, habari zinasema kuwa Mwigulu alikuja na hoja ya mfuko na serikali ikachukua, sasa migomo imepungua. Sasa anapigania kila mtoto masikini apate mkopo kwa asilimia 100.
“Alipeleka hoja binafsi ya ajira, sasa analeta sera ya ajira kulinda ajira za wazawa. Mungu atupe nini? Wengi tulikuwa hatumwelewi huyu jamaa kwa ajili ya msimamo wake mkali ni kutokuogopa mtu yeyote. He is the right person,” aliandika mmoja wa wachangiaji wa Mtandao wa Kijamii wa Jamii Forum.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari , wakati wa kikao cha Bunge la Bajeti kulikuwa na fununu za kwenda Dodoma kwa baadhi ya matajiri waliokuwa na lengo la kutaka kumshawishi Mwigulu asifute misamaha ya Kodi.
Lakini habari zaidi zinasema kuwa Mwigulu aliwakatalia akisema kuwa kuwasamehe matajiri na kuwatoza kodi masikini ni kusababisha masikini waendelee kuwa masikini na matajiri waendelee kuwa matajiri.
“ Hii inaonesha jamaa haingiliki, hata hivyo, katika kuonesha umwamba, Mwigulu alimvaa spika kuwa misamaha ya kodi kwa matajiri lazima ifutwe. Bunge zima likazizima. Hakika Jamaa anatuwakilisha vizuri vijana,” alisema kijana mmoja wa aliyeongea na mwandishi wetu wiki iliyopita jijini, Dar es Salaam.
Wakati hayo yakiendelea nchini Tanzania, duru za kimataifa kutoka Jumuiya ya watanzania waishio nchini Marekani (Diaspora) zinaripoti kuwa, Watanzania waliopo Marekani wameamka sana katika kufuatilia na kutoa maoni yao kuhusu mustakabali wa siasa za Tanzania hususani kuelekea 2015.
Chanzo chetu cha habari kilichopo Washington kinadokeza kuwa mbali na watu kadhaa waliokuwa wanasikika kwenye medani za Urais 2015, Mwigulu Nchemba anabeba taswira tofauti kabisa kwa Watanzania walipo huko Marekani.
Kama ilivyo kwa wafugaji hapa nchini, Watanzania waishio Marekani wao wamesema kuwa wako tayari kumchangia fedha za kampeni Mwigulu endapo atajitokeza na kupitishwa na chama chake kuwania nafasi hiyo.
Taarifa toka kwa afisa mmoja wa Ubalozi wa Tanzania, huko New York zinasema watanzania hao wapatao 93 wakiwakilisha states mbalimbali walifanya kikao Julai 4, 2014 katika Hoteli ya Marriott, mjini Houston walikokwenda kuhudhuria harusi ya Mtanzania mwenzao aliyefahamika kwa jina moja la ndugu Mtafungwa.
Watanzania hao kwa kauli mmoja walikubaliana kwanza kumshawishi Mwigulu akubali maombi ya watanzania walio wengi ambao wamekuwa wakimuomba achukue fomu ya Urais 2015.
Aidha, afisa huyo wa ubalozi amesema kuwa watanzania hao walikubaliana kuwa wataungana na wenzao wa Uingereza, wafugaji wa Tanzania na wakulima ambao tayari walishatoa tamko kuwa watachangishana fedha ili wamsaidie kijana huyo apate fedha za kampeni.
“Kwa upande wao watanzania waishio Marekani na Uingereza wamemkubali Mwigulu na kumtaja kuwa ni jasiri, mkweli na mtu mwenye maadili na uzalendo kwa taifa lake asiyeogopa kufichua uovu, anayetenda mambo anayoyasema”, alisema afisa huyo.
“Mwigulu anasema na kutenda anachokiamini, mzalendo wa kweli, ni mtu mwenye maono, ni kweli ni mtu tunayemhitaji, he is the man we need (ni mtu tunayemhitaji). Hapindishi maneno, haogopi mtu yeyote inapofikia kuambizana ukweli.
Tutamchangia fedha za kampeni na tutarudi Tanzania kuungana na vijana, wafugaji na wakulima kumtafutia kura”, alisema afisa huyo.
Habari zaidi kutoka kwa afisa ubalozi huyo zinasema kuwa watanzania hao waliunda kamati ya watu 8 wa kutoka Calfornia, Houston, Chicago, DMV, Boston, North Carolina, Ohio na New York walimfuata Mwigulu katika ofisi za Umoja wa Mataifa alipokwenda kuhudhuria mkutano wa kupanga agenda baada MDG8 kufikia ukomo kumweleza maazimio ya kikao cha watanzania waliowatuma baada ya kikao cha Julai 4, mwaka huu.
Aidha, habari zinasema kuwa wajumbe wa kamati hiyo walipotoka kumuona Mwigulu walikuwa na nyuso za furaha zilizoashiria kuwa huenda kiongozi huyo aliwakubalia ombi lao.
Katika kipindi ambacho viongozi ndani ya CCM wamekuwa wakitangaza nia za kuwania Urais 2015, kumekwepo na wito, ushauri na kiu kutoka kwa watanzania wengi wakitaka Mwigulu Nchemba agombee Urais na kwamba ni aina ya kiongozi anayetakiwa kuongoza Tanzania kwa sasa hasa kutokana na msimamo wake usioyumbishwa kuhusu maslahi ya taifa, ujasiri wake wa kuwakemea waovu, wezi na wakwepa kodi bila kuogopa, maono yake ya namna ya kuwainua kiuchumi watanzania masikini hasa wakulima, wafugaji na watoto wa masikini wanaokosa mikopo.
Akiongea na mwandishi wetu hivi karibuni akiwa nchini Afrika Kusini, Mwigulu alisema hawezi kuzungumzia jambo hilo kwa sasa ila amewataka waliomuomba agombee urais wawe wavumilivu kidogo.
Alisema kuwa chama chake kina utaratibu mzuri kwa makada wake wanaotaka kuwania nafasi mbali mbali za uongozi, hivyo si busara kwake kupingana na utaratibu huo.
“Ni kweli nimefuatwa na makundi ya watanzania wakiniomba nami nitangaze nia ya kuwania nafasi ya urais.
“Hawakufanya vibaya kwakuwa sifa ya mtu binafsi kutaka urais haitoshi bali watu wengine kumpima kwa kutumia vigezo na kujiridhisha kuwa anafaa kuwa kiongozi wa kuwatumikia.
“Nina kazi kubwa katika wizara yangu lakini ninachotaka niwaombe ni kwamba wawe wavumilifu,” alisema Mwigulu.
Hata hivyo, Mwigulu amesema kuwa kiu yake kwa sasa ni kufanya mabadiliko ili fedha ziweze kwenda kwenye miradi iliyokusudiwa.
“Nina jukumu kubwa la kufanya mabadiliko ili kuongeza makusanyo ya fedha, kudhibiti mianya ya ukwepaji wa kodi, kufuta misamaha ya kodi inayotolewa kwa matajiri na kuwabebesha mzigo maskini, kusimamia fedha zitumike kwenye matumizi yenye manufaa kwa watanzania, kama vile barabara, umeme na maji.
“hapa ninamaanisha kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kusimamia fedha zilizopelekwa kwenye miradi ya maendeleo zitumike kwa uadilifu,” alisema Mwigulu.
Kuombwa kwa Mwigulu aweze kutangaza nia ya kuwania urais, kumekuja huku kukiwa na makada kadhaa wa chama hicho ambao tayari wameonyesha nia ya kuitaka nafasi hiyo ya juu kabisa ya uongozi wa
nchi.
Mmoja wa makada hao ni Mbunge wa Rungwe Mashariki na Waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya.
Kiongozi huyo , hivi karibuni alisema kuwa ana nia ya kuwania urais mwaka 2015.
Mwandosya, ambaye aliwahi kuwania nafasi ya kuteuliwa na chama kugombea urais mwaka 2005, akichuana na Rais Jakaya Kikwete, alisema kuwa itakuwa heshima kwake kama chama kitaweza kumfikiria na hatimaye kumteua kugombea urais mwaka 2015.
Mwingine aliyekwisha kutangaza nia yake wiki chache zilizopita, ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Akitangaza nia yake hiyo akiwa Uingereza alikokuwa akihudhuria mkutano wa sekta ya mawasiliano baada ya kuhojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza, Makamba alisema kuwa huu ni wakati wa kupisha fikra mpya kuongoza dola.
Makamba, mmoja wa makada wa CCM iwapo atapitishwa na chama hicho, ataelekeza nguvu kwenye vipaumbele vyake vinne ambavyo ni ajira, huduma za jamii, uchumi imara na utawala bora.
Mbunge huyo wa Bumbuli alisema hayo
“Ni wakati wa fikra mpya kushika dola na mimi ninaona kwamba wazee wakae kando. Mfano awamu moja inapoondoka na wazee walioko katika mfumo wakae kando ili kupisha fikra mpya kuongoza dola,” alisema Makamba ambaye ana umri wa miaka 40.
Kada mwingne wa CCM ambaye tayari ameonyesha nia ya kutaka kuwania urais 2015 ni Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye.
Akitangaza nia yake alisema kuwa yeye ni tumaini la Watanzania na mpambanaji wa vita dhidi ya maovu.
Kauli hiyo aliitoa jijini Mwanza , katika hotuba yake ya uzinduzi wa taasisi ya Vijana ya Tanzania Youth (TYDC).
Februari 18, mwaka huu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu katika kikao chake ilipendekeza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa makada wake sita ambao wameanza kampeni ya kuwania urais wa mwaka 2015.
Makada waliopewa adhabu ya mwaka mmoja kwa tuhuma za kuanza kampeni za kuwania urais kabla ya wakati ni January Makamba, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu) Steven Wassira pamoja na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Katika adhabu hiyo, makada hao walizuiwa kujihusisha na masuala ya kisiasa ndani ya chama hicho kwa miezi 12, huku mwenendo wao wa kisiasa ukifuatiliwa chini ya uangalizi mkali katika kipindi chote cha kutumikia adhabu hiyo.
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako