Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, ameteleza ulimi tena na mara
hii amejikuta akimuita Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila
(NCCR-Mageuzi) tumbili.
Kabla
ya kutoa kauli hiyo, Werema alikuwa akitoa ufafanuzi wa mwongozo
ulioombwa na Kafulila, kuhusu fedha zilizokuwa katika akaunti ya Escrow
iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambazo zimelipwa kwa kampuni ya
PAP, inayomiliki mitambo ya kampuni ya umeme ya Independent Power
Tanzania Limited(IPTL).
Werema alisema fedha hizo si za Serikali, kama inavyodaiwa na Kafulila, kwa kuwa fedha za Serikali, hazikai katika akaunti hiyo.
Alifafanua
kuwa taarifa zinazotolewa, zinapotosha umma kuwa serikali imetoa fedha
kuilipa IPTL, wakati ukweli ni kuwa fedha hizo ziliwekwa katika akaunti
hiyo, kutokana na misuguano baina ya wanahisa wawili, waliokuwa wamiliki
wa IPTL.
Werema
alibainisha kuwa mmoja wa wanahisa hao, alikuwa akitaka IPTL ifilisiwe,
huku mwingine akipinga jambo hilo mpaka walipouza hisa zao na kumaliza
mgogoro huo, ambapo Mahakama iliruhusu mali za kampuni hizo, apewe
mwanahisa mpya, PAP.
Werema
alisema kuna watu walileta bungeni vipeperushi, wakidai ni ushahidi
kuhusu utoaji wa fedha hizo za akaunti ya Escrow na kuhusisha na rushwa.
"Kafulila
ni miongoni mwa wanaoeneza taarifa potofu…kama ni tuhuma au kuna
rushwa, itakuja kujulikana, tusubiri uchunguzi wa vyombo husika,” alisema.
Wakati
akizungumza, Werema alitumia mfano wa kabila la Wanyankole, aliosema
kuwa wana usemi unaosema kwamba 'Tumbili hawezi kuamua kesi ya msituni'.
Kabla
ya kufafanua maana ya msemo huo, Kafulila bila kuwasha kipaza sauti,
alikuwa akipiga kelele kumuita Werema kuwa ni mtuhumiwa, hivyo atangaze
maslahi yake.
“Naomba nisikilize, hata kama ni mtuhumiwa, nina fursa ya kusikilizwa …nisikilize wewe tumbili,” alijikuta akisema Werema.
Baada ya kusema hivyo, Kafulila hakukubali ;na yeye bila kuwasha kipaza sauti, alisema: “Wewe (Werema) ni mwizi tu.”
Kutokana
na hali hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azan 'Zungu' alimuomba Jaji
Werema, kukaa chini ili atoe ufafanuzi, huku Mbunge wa Ubungo, John
Mnyika (Chadema) na Kafulila wakitaka kuzungumza.
Zungu
alisema kwa kuwa Bunge, lilishaamua kuwa suala hilo, lipelekwe Taasisi
ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG), ni vyema kama Kafulila ana ushahidi
wowote, apeleke huko.
Baada
ya kutoa mwongozo huo, ambao ulisitisha malumbano, Mwenyekiti Zungu
alisitisha shughuli za Bunge mpaka jioni na kuondoka, huku akisindikizwa
na makatibu wa Bunge na wapambe kama kawaida.
Hatua
ya Mwenyekiti wa Bunge kuondoka katika ukumbi, baada ya kusitisha
shughuli za Bunge, ilimpa fursa Jaji Werema kuweka sawa makabrasha yake
na kutoka katika kiti chake, ambapo alionekana kama vile anakwenda
kumkabili Kafulila.
Wakati hilo likitokea, Mbunge wa Maswa Mashariki, Sylvester
Kasulumbayi (Chadema), alihama katika kiti chake na kukimbilia alipokuwa amekaa Kafulila.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, baadhi ya mawaziri walimzunguka Jaji Werema, kabla hajamfikia Kafulila na Kasulumbayi.
Mawaziri
hao ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira, Waziri wa Sheria na
Katiba, Dk Asha Rose Migiro na Naibu Waziri wa Afrika Mashariki, Dk
Abdullah Juma Abdullah Saadalla.
Nje
ya Bunge, Kafulila na Mnyika waliitisha mkutano na waandishi wa habari,
ambapo walidai kuwa na ushahidi wa kutuhumu baadhi ya mawaziri, kusema
uongo bungeni kuhusu fedha hizo za Escrow.
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako