A

A

WENGER, RODGERS WAGOMBEA KUMSAJILI MCHEZAJI MKENYA


KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger na kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers wameingia katika vita ya kumuwania mtoto wa staa wa zamani wa timu ya taifa ya Kenya, Mike Okoth Origi, Divock Origi anayekipiga klabu ya Lille ya Ufaransa.

Origi alizaliwa nchini Ubelgiji katika mji wa Ostend nchini Ubelgiji ambako baba yake alikuwa akicheza soka la kulipwa katika klabu mbalimbali za Oostende KV, KRC Harelbeke na Racing Genk.

Katika msimu huu, Origi, 18 amefunga mabao matano katika mechi za Ligi Kuu ya Ufaransa na tayari ameanzisha mgogoro miongoni mwa timu kubwa za England huku Liverpool na Arsenal zikianza kimbelembele.


Aweka rekodi Ufaransa

Akiwa na umri wa miaka 17 na miezi tisa tu, Divork aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa pili mdogo zaidi kufunga bao msimu huu wa Ligi Kuu Ufaransa huku wa kwanza akiwa kinda Neal Maupey, 16, wa klabu ya Nice.

Lakini kabla ya hapo, katika msimu wake wa kwanza Origi alifunga bao katika mechi ya kwanza dhidi ya Troyes katika sare ya 1-1. Kutokana na bao hilo, Origi alisifiwa vilivyo na kocha wake pamoja na wachezaji wenzake kutokana na kiwango kizuri alichoonyesha.

Kocha wake, Rudi Garcia, alimwelezea Origi kama muunganiko mzuri katika timu na tishio kubwa mbele ya lango, lakini alimtaka asivimbe kichwa kutokana na mwanzo huo mzuri. Garcia alisema kwamba ana kazi kubwa ya kufanya katika masuala ya mbinu.

“Amefanya mazoezi na sisi mara kadhaa. Ana nguvu na ni mzuri mbele ya lango, lakini lazima afanye kazi kubwa. Kuna kazi kubwa mbele yake sana sana katika suala la mbinu. Njia bado ndefu kwake.”

Kabla ya kutua Ufaransa, Origi alikuwa akikipiga katika klabu ya Racing Genk ya Ubelgiji ambayo baba yake pia aliwahi kuchezea. Mpaka sasa bado hajaamua timu ya taifa ya kuichezea lakini tayari ni staa wa timu ya vijana ya Ubelgiji chini ya umri wa miaka 19.

Amewahi kukipiga katika timu ya taifa ya Ubelgiji chini ya umri wa miaka 15, 16 na 17. Lakini mpaka sasa amefunga mabao manne katiak mechi tisa za timu ya chini ya umri wa miaka 19 ambako ana nafasi ya kudumu kikosini.

Harambee Stars yaanza kumtolea macho

Wakati Wabelgiji wakimtaka aichezee timu ya wakubwa ya nchi hiyo kwa kumuunganisha na mastaa wengine kama Eden Hazard, Marouane Fellaini, Romelu Lukaku, Christian Benteke na wengineo, Wakenya wanamuhitaji katika timu yao ya taifa kwa ajili ya kuimarisha safu yao ya ushambuliaji