A

A

RAIS KIKWETE AMLILIA MAALIM GURUMO, ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara kufuatia kifo cha mwanamuziki maarufu na wa siku nyingi, Muhidini Maalim Gurumo kilichotokea tarehe 14 Aprili, 2014 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya ugonjwa wa moyo uliomsumbua kwa muda mrefu.
“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa na taarifa za kifo cha Muhidini Maalim Gurumo ambaye alikuwa mmoja wa wasanii wa muziki wa dansi nchini waliolitumikia Taifa hili kwa bidii tangu miaka ya sitini kupitia sanaa ya muziki katika bendi mbalimbali za muziki wa dansi kuanzia Bendi ya NUTA Jazz, Mlimani Park Orchestra, Orchestra Safari Sound (OSS) na Msondo Ngoma ambayo ameitumikia hadi alipostaafu mwaka 2013”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake.
 
Rais Kikwete amesema mchango wa Marehemu Muhidini Maalim Gurumo kwa Taifa letu ni mkubwa na wa kupigiwa mfano kupitia kipaji alichojaaliwa na Mwenyezi Mungu ambacho alikitumia kikamilifu kwa manufaa ya wananchi wa nchi yetu na Taifa kwa ujumla.

Rais Kikwete amemuomba Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kumfikishia Salamu zake za Rambirambi na pole nyingi kwa familia ya Marehemu Muhidini Maalim Gurumo kwa kumpoteza kiongozi na mhimili wa familia yao.  Amesema binafsi anaungana na familia ya marehemu kuomboleza msiba huu mkubwa kwa kutambua kuwa msiba wao ni wa wote, na anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza mahala pema peponi Roho ya Marehemu, Amina.

Aidha Rais Kikwete amewaomba wanafamilia ya marehemu kuwa na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza msiba wa mpendwa wao kwa kutambua kwamba yote ni mapenzi yake Mola.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

14 Aprili, 2014