A

A

Ndege ya Malaysia ilibadili mkondo ‘Maksudi’


Marubani wawili waliokuwa wanaendesha ndege ya Malaysia
********
Mtambo wa mawasiliano wa ndege ya Malaysia iliyotoweka wiki moja iliopita, ulizimwa kwa maksudi.
Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya waziri mkuu wa Malaysia Najib Razak.
Alisema kuwa ndege hiyo ilibadili mkondo na kuendelea kuruka kwa saa saba zaidi ya muda uliotakiwa kulingana na mawasiliano yaliyorushwa kwa Satelite na mtambo wa Radar.

Bwana Razak aliongeza kwamba hatua za ndege hiyo zinaambatana na matakwa ya mtu binafsi ambaye alikuwa akiielekeza.
Ngege hiyo ilitoweka wiki jana ikiwa imewabeba abiria 239.
Nusura bwana Razak aseme kuwa ndege hiyo ilitekwa nyara ingawa alisisitiza kwamba uchunguzi ungali unaendelea kubaini ilikokwenda ndege hiyo.
Dhana kwamba ndege hiyo ilitekwa nyara ilipingwa vikali awali lakini sasa inaonekana imerejea kuwa mojawapo ya sababu za kutoweka kwake.

Juhudi za kuitafuta ndege ya Malaysia bado zinaendelea
Mtambo wa mawasiliano wa ndege hiyo ulizimwa kwa maksudi na huenda marubani walifanya hivyo kwa hiari au kwa kulazimishwa.
Darubini sasa inawalenga watu waliokuwa wameabiri ndege hiyo na wafanyakazi wa ndege.
Wapelelezi watataka kujua ikiwa kumekuwa na tukio lolote la matatizo ya kiakili, changamoto za kifamilia na shinikizo la mawazo kwa yeyote aliyekuwa katika ndege hiyo, hasa marubani.
Ni wiki nne tu zimepita tangu rubani wa ndege ya Ethiopia kuiteka nyara ndege akitaka kupata hifadhi nchini Switzerland.
Marubani wa ndege hiyo ya Malaysia walikuwa na rekodi nzuri tu ya kikazi ingawa polisi bado wamefanya msako nyumbani kwao.
CHANZO: BBCSWAHILI