PAC imeanza uchunguzi kuhusu ukwepaji kodi unaofanywa na makampuni ya Kimataifa
PAC imeanza uchunguzi kuhusu ukwepaji kodi unaofanywa na makampuni ya kimataifa.
Leo tarehe 30 Machi 2014, kamati ya BUNGE ya PAC imeanza rasmi
uchunguzi kuhusu ukubwa wa tatizo la ukwepaji kodi na utoroshwaji wa
fedha unaofanywa na makampuni ya kimataifa ( multinational
corporations). Uchunguzi huu unatokana azimio la umoja wa kamati za PAC
za nchi za SADCOPAC lilioamuliwa Arusha, Tanzania mwezi Septemba mwaka
2013 ( Azimio lilisomeka – PACs should initiate investigations on the
extent of tax avoidance/evasion and illicit money transfer in their
jurisdiction).
Leo PAC imekutana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Benki Kuu ya
Tanzania (BOT), Kitengo cha Fedha Haramu ( FIU) na Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa ajili ya majadiliano ya awali
kuhusu uchunguzi huo.
Kamati imeelezwa kuwa tatizo la
ukwepaji kodi ni kubwa sana na
linagusa sekta zote. TRA imeieleza kamati mifano mbalimbali kwa kila
sekta namna gani Taifa linapoteza kodi. Njia zinazotumika ni pamoja na
udanganyifu katika mikopo, udanganyifu katika bei za mauzo ya bidhaa
zinazouzwa nje na mikataba ya biashara miongoni mwa makampuni
yanayohusiana. Uchunguzi uliofanywa na TRA kwa kampuni mojawapo wa
uchimbaji madini unaonyesha kuwa kampuni hiyo iliyotangaza hasara mwaka
2011 iligundulika kuwa kumbe ilipata faida ya dola za kimarekani 327
milioni.
Sekta ya Utalii na mahoteli inaonyesha kugubikwa kiasi kikubwa na
ukwepaji kodi kwa kampuni katika sekta hiyo kutumia mikataba na
makampuni yanayohusiana yaliyokwenye Tax Havens ambayo inahamisha mapato
mengi kwenda offshore (profit shifting and base erosion).
Kamati imeelezwa na BoT kuwa hivi sasa kuna uchunguzi maalumu unaoendelea kuhusu ‘illicit financial transfer’ kutoka Tanzania.
Kamati imeelezwa na BoT kuwa hivi sasa kuna uchunguzi maalumu unaoendelea kuhusu ‘illicit financial transfer’ kutoka Tanzania.
Pia ameeleza kwamba hatua zimeanza kuchukuliwa kufunga akaunti za
makampuni ya madini yaliyopo offshore kwani sababu za makampuni hayo
kuwa akaunti nje hazina msingi tena. Hata hivyo changamoto kubwa ni
mikataba waliyoingia na Serikali ambayo inawaruhusu kufungua akaunti
offshore na kuweka mapato yao yote ya mauzo ya madini huko.
Utoroshaji wa fedha kutoka Tanzania ni changamoto kubwa sana ya
maendeleo ya Tanzania katika kupambana na umasikini. Utoroshwaji umekuwa
ukikua mwaka hadi mwaka. Taarifa ya benki ya maendeleo Afrika
inaonyesha kuwa mwaka 2010 peke yake Tanzania zilitoroshwa jumla ya dola
za kimarekani bilioni 1.3 ambazo zilikuwa sawa na asilimia 5 ya Pato la
Taifa (GDP) na zaidi ya asilimia 20 ya mapato ya ndani ya TRA.
Kamati ya PAC itaendesha uchunguzi na kuandaa taarifa
itakayowasilishwa bungeni kwa hatua zaidi. Hii itakuwa ni mara ya kwanza
kwa BUNGE la Tanzania kuendesha uchunguzi wa aina hii. Pia Tanzania
imekuwa nchi ya kwanza katika eneo la SADC kutekeleza azimio hili.
Nchini Uingereza kamati ya PAC ya BUNGE la uingereza iliendesha
uchunguzi kama huu na makampuni makubwa kama google, Amazon na Starbucks
waligunduliwa kukwepa kodi nchini humo. Kwa nchi za Afrika sekta yenye
kutorosha fedha na kukwepa kodi kwa wingi ni sekta ya madini, mafuta na
gesi. Mwaka 2013 mwezi Desemba kamati ya PAC Tanzania ilikutana na PAC –
UK ili kupata uzoefu wa namna ya kuendesha uchunguzi wa aina hii.
Zitto Kabwe, MB
Mwenyekiti, PAC
Dodoma
30-03-2014
Mwenyekiti, PAC
Dodoma
30-03-2014