HAPA NDIPO JK ALIPOMMALIZA WARIOBA NA TAKWIMU ZAKE
"Lakini wapo
wanaodai kuwa takwimu za Tume hazionyeshi ukweli huo. Wanasema kuwa
taarifa ya Tume imeonesha kuwa Watanzania waliotoa maoni yao kwa Tume
kwa mdomo na maandishi walikuwa 351,664. Kati yao ni wananchi 47,820 au
sawa na asilimia 13.6 ndiyo waliokerwa na muundo wa Muungano hivyo
wakauzungumzia. Wananchi 303,844 au sawa na asilimia 86.4 muundo wa
Muungano kwao halikuwa tatizo, ndiyo maana hawakuuzungumzia kabisa. Wanahoji kuwa iweje leo asilimia 13.6 ya Watanzania wote waliotoa maoni wageuke kuwa ndiyo Watanzania walio wengi! "
Wanasema pia, kwamba mbona Taarifa ya
Tume yenyewe, kuhusu takwimu (uk.
66 na 67), inaonesha kwamba kati ya hao watu 47,820 waliotoa maoni
kuhusu Muungano, ni watu 17,280 tu ambao ni sawa na asilimia 37.2 ndiyo
waliotaka muundo wa Serikali tatu, asilimia 29.8 walitaka Serikali
mbili, asilimia 25.3walipendekeza Serikali ya Mkataba na asilimia 7.7
walipendekeza Serikali moja. Hii hoja ya Watanzania wengi kutaka
Serikali tatu msingi wake upi?
Takwimu za Tume (uk. 57)
zinaonyesha, vilevile kuwa Tume ilipokea maoni 772,211. Kati ya hayo
asilimia 10.4 tu ndiyo yaliyozungumzia muundo wa Muungano na asilimia
88.6 hayakuzungumzia Muungano bali mambo mengine. Hivyo basi wanahoji
pia kwamba kama muundo wa Muungano ungekuwa ni jambo linalowakera
Watanzania wengi, lingedhihirika kwenye idadi ya watu waliotoa maoni na
kwenye idadi ya maoni yaliyotolewa. Yote hayo hayakujitokeza.
Waliouzungumzia Muungano walikuwa asilimia 13.6 tu ya watu wote waliotoa
maoni na maoni yanayohusu Muungano yalikuwa asilimia 10.4 ya maoni
yote. Hivyo basi, wanauliza “usahihi wa hoja ya Watanzania wengi kutaka
Serikali tatu uko wapi?”