"Ndugu zangu, Uchaguzi
mkuu wa TFF ulifanyika tarehe 27 Oktoba, 2013 na kukamilika alfajiri ya
tarehe 28 Oktoba, 2013 ambapo Kamati ya Utendaji ya TFF ilitangazwa
rasmi na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa TFF Ndugu Hamidu
Mbwezeleni.
Katika
kuelekea uchaguzi mkuu huo niliitisha mkutano na waandishi wa habari
ambapo nilitangaza ilani yangu ya uchaguzi. Lengo la ilani ilikuwa ni
kuwaeleza wadau na wapenzi wa mpira wa miguu Tanzania dira ambayo
ingeongoza mpira wetu iwapo ningechaguliwa kuwa Rais wa TFF. Aidha
niliahidi iwapo ningechaguliwa tungekutana katika chumba hiki hiki
baada ya siku 100. Ninapenda nichukue fursa hii kuwashukuru na
kuwapongeza wajumbe wote wa Mkutano Mkuu wa TFF, walionipa kura na ambao
hawakunipa kura, kwa kukamilisha vyema zoezi la uchaguzi huo. Uchaguzi
umekamilika kazi iliyobakia mbele yetu ni kutekeleza majukumu yetu kama
viongozi wa mpira miguu Tanzania.
Ilani na Utekelezaji wake
Ilani
yangu ya uchaguzi iliainisha maeneo kadhaa ya kupewa vipaumbele.
Nitakumbushia maeneo haya na kueleza hatua tulizofikia katika
utekelezaji wake:
1. Idara ya Ufundi
1.1 Kikao
cha Kamati ya Utendaji kilichokaa tarehe 23 Novemba, 2013 pamoja na
mambo mengine kilipitisha muundo mpya wa Sekretariati ya TFF. Muundo
huo unaelezwa katika chati hii hapa chini:
Katika muundo huu Idara ya Ufundi imepanuliwa kwa kuundwa vitengo vya Ufundi,Elimu na Maendeleo ya mpira.
Aidha
katika kutekeleza azma ya kuboresha usimamizi wa mpira wa vijana (Youth
Football) Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania limeamua kuajiri Desk
Officer wa vijana yaani msimamizi maalum wa mpira wa vijana na tayari
ameajiriwa.
Zoezi la kuimarisha Idara ya Ufundi kwa kuajiri Mkurugenzi wa Ufundi pamoja na Wakurugenzi wake Wasaidizi linaendelea.
1.2 Ujenzi wa Kituo cha Mpira (Football Centre of Excellency)
Limekuwa
ni jambo la kufurahisha na kutia moyo kuwa mara baada ya kuingia
madarakani Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo ilitufahamisha juu ya uamuzi wa Serikali, kwa kushirikiana na
Kampuni ya SYMBION ya Marekani na Klabu ya Mpira ya SUNDERLAND ya
Uingereza, wa kujenga kituo cha michezo (Sports Centre) Kidongo Chekundu
, Ilala na kujenga kituo cha kulea na kukuza vipaji vya vijana (Elite
Academy) Wilayani Kinondoni. Wizara ilinikutanisha na Uongozi wa
SYMBION na mazungumzo yanaendela kuona ni jinsi gani mradi huu
utashirikisha Serikali, Mshirika wetu SYMBION, Klabu ya SUNDERLAND na
TFF ambao kwa mujibu wa katiba yetu ndio waratibu na wasimamizi wa
maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania. Vikao kadhaa vimefanyika na
mwelekeo ni mzuri sana. Tunaamini mradi huu utatoa mchango mkubwa sana
katika kuendeleza mpira wa vijana (Youth Football).
Aidha
kamati ya utendaji ya TFF imeviagiza vyama vyote vya mpira vya mikoa
kuomba kumilikishwa viwanja vikubwa katika maeneo mapya yanayopimwa,
TFF italipia malipo yote yatakayotakiwa. Mkoa wa Tanga tayari
wametekeleza agizo hili na hati imekwisha toka.Msanifu tayari anaanda
michoro ya awali kwa ajili ya kujenga kituo cha michezo katika ardhi
hii. Mfano wa mchoro wa kituo hiki ndio utakaotumika nchi nzima iwapo
utapitishwa na kamati ya utendaji.
1.3 Timu Kupanda Daraja
TFF
tayari imeunda Kamati ya dharura (Adhoc) ya kuangalia mapungufu
yaliyopo katika utaratibu wa sasa wa kuwa na timu 14 za Ligi Kuu na 24
za Ligi Daraja la Kwanza ili tuone ni kwa jinsi gani tutaweza kuboresha
Ligi yetu. Ripoti ya Kamati ikikamilika italetwa mbele ya Kamati ya
Utendaji kwa ajili ya maamuzi ya mwisho.
1.4 Kuanzisha Mashindano Mapya na Kufufua ya Zamani
Juhudi
zinaendelea kuhakikisha mashindano ya Kombe la Taifa yanafufuliwa.
Aidha taratibu za kuanzisha upya Kombe la Shirikisho (Federation Cup)
ambalo litakuwa ni la mtoano nchi nzima zimefikia hatua nzuri na muda
si mrefu taratibu zake zitatangazwa pindi mshirika wetu atakapokuwa
amemaliza maandalizi upande wake.
1.5 Mpira wa Wanawake
1.5.1 Katika
kuhakikisha mpira wa wanawake unatengenezwa mkakati maalum wa maendeleo
matayarisho ya mpango wa maendeleo ya mpira wa wanawake (women football
development plan) yamekamilika na yatawasilishwa katika kikao kijacho
cha Kamati ya Utendaji kwa ajili ya maamuzi ya mwisho. Mpango huu
utatoa dira ya maendeleo ya mpira wa miguu kwa miaka mitano ijayo na
utakuwa ni sehemu ya mpango kazi wa TFF wa miaka mitano.
1.5.2 TFF
inayo furaha pia kuufahamisha umma wa wapenda mpira wa Tanzania kuwa
shula ya kukuza na kuendeleza vipaji ya Alliance Mwanza kwa kutambua
mapungufu yaliyopo katika kuendeleza mpira wa wanawake kuanzia mwaka huu
imeanzisha mafunzo maalum ya mpira wa watoto wa kike umri chini ya
miaka 10. Matunda yake tutayaona baadaye. Hawa watakuzwa na kulelewa
pamoja.
1.5.3 Jitihada
zinafanyika kuanza mashindano ya kitaifa ya wanawake na muda si mrefu
utaratibu wake utatangazwa baada ya mshirika wetu kumaliza maandalizi
yake.
1.5.4 TFF
kwa kushirikiana na Wizara ya Wanawake na Jinsia ipo katika kuandaa
mpango kazi wa kushirikiana na vyuo 55 vya Ustawi wa Jamii Tanzania
katika kuanzisha masomo maalum kwa wasichana katika vyuo nchini, masomo
ambayo yatahusisha ufundishaji wa mpira wa wanawake, urefa, ukocha na
utawala wa mpira. Lengo ni kutoa fursa kwa wasichana kujifunza stadi
hizi kama sehemu ya masomo yao katika vyuo vya maendeleo ya jamii.
Utaratibu wa mpango huu unasimamiwa na chama cha mpira wa migu wa
wanawake (TWFA) na taasisi nyingine husika.
1.5.5 Pamoja
na ufinyu wa bajeti tulionao na timu zetu za wanawake kutokuwa na
udhamini TFF bado inahakikisha timu zetu za wanawake zinashiriki
michuano yote ya kimataifa.Wiki iliyopita timu yetu ya Taifa ya wanawake
imesajiliwa kushiriki mtoano wa kushiriki fainali za All Africa games
Congo Brazzavile 2015.
1.6 Maandalizi ya Vijana (Grassroot Football)
Mpango
kazi wa maendeleo ya mpira wa miguu wa vijana Tanzania (Tanzania youth
development plan) maandalizi yake yamekamilika na utazinduliwa muda si
mrefu. Vipaumbele vikuu vya mpango huu ni pamoja na:
1.6.1 Kuhakikisha
shule zote za msingi 16,000 za Tanzania zinakuwa na viwanja vya
kuchezea mpira, mwalimu mmoja wa mpira na zinapata kwa mwaka angalau
mipira 10 ya size 3 na 4 pamoja na jozi angalau 30 za viatu.
TFF
tayari inawasiliana na Mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali ili
yatukusanyie vifaa vya mpira vilivyotumika (has viatu) ili viweze
kuletwa na kugawiwa kwa watoto wetu kwenye shule za msingi na
academies. Kwa sasa tayari kontena mbili za vifaa hivi zimekwisha
kusanywa nchini Uingereza na utaratibu wa kuzileta unafanyika. Lengo ni
kuingiza nchini jozi za viatu 500,000 kwa mwaka na mipira 160,000 ya
size 3 na 4 kwa mwaka. TFF inaomba ushirikiano wa Serikalini, Taasisi
za Umma, Makampuni Binafsi na Taasisi zisizo za kiserikali katika
kuhitimisha azma hii.
1.6.2 TFF
ilipata fursa ya kukutana na Balozi wa Uholanzi hapa nchini na kufanya
naye mazungumzo. Nia na lengo ilikuwa ni kuangalia ni kwa jinsi gani
Uholanzi inaweza kutusaidia kufundisha walimu wa walimu (trainer of
trainers). Matumaini yetu ni kuwa walimu hawa wakishafuzu watakuwa na
jukumu la kuwafundisha walimu wa michezo wa shule za msingi kwa
kushirikisha vyuo vya walimu vinavyotoa taaluma hii kama Malya,
Murutunguru na Butimba.
1.6.3 TFF
kwa kushirikiana na taasisi isiyo ya kiserikali inaangalia uwezekano wa
kujenga vituo vya michezo 169 katika Wilaya zote 169 Tanzania. Vituo
hivi pamoja na kufundisha mpira vitakuwa pia ni vituo maalum vya
kuwafundisha vijana juu ya athari za matumizi ya dawa za kulevya.
1.6.4 TFF
kupitia Idara yake ya Ufundi na Kamati ya Vijana iko mbioni kufanya
sensa ya vituo vya kukuza na kulea vipaji vya vijana (Academies) pamoja
na vituo vya mpira (Sports Centres) nchini kote Tanzania. Utaratibu
unafanywa wa kuweka vigezo vya kutambuliwa vituo hivi na TFF itaanzisha
utaratibu wa kusajili na kutoa vyeti vya usajili kwa vituo
vitakavyokidhi vigezo. Lengo ni kuweka utaratibu nchini wa kusimamia na
kuendeleza vituo hivi kitaifa.
1.6.5 Mpango
wa muda mfupi wa TFF ni kuandaa timu ya Taifa ya vijana itakayoshiriki
mashindano ya Fainali za Afrika umri chini ya miaka 17 mwaka 2019.
Tanzania tumeomba uenyeji wa Fainali hizi. Mwaka huu wa 2014 TFF
itafanya mashindano maalum ya vijana chini ya umri wa miaka 12 ili
kuunda timu ya Taifa ya kuanzia ya U12, timu ambayo itakua pamoja
kuelekea 2019. Malengo ni kuiboresha timu hii kila mwaka kwa kuongeza
vijana U13 mwaka 2015, U14 mwaka 2016, U15 mwaka 2017 na mwishowe U16
mwaka 2018.TFF imekwisha pata mshirika wa mpango huu na akimaliza
maandalizi yake atatangazwa rasmi.
1.6.6 Ili
Tanzania ifundishe mpira unaofanana nchini kote, utaratibu unafanyika
wa kuandaa mtaala wa kufundisha mpira (National football curricullum).
Mtaala huu unaandaliwa na Idara ya Ufundi ya TFF kwa kusaidiana na
Mtaalam wa mpira toka Uholanzi. Mtaala huu ukikamilika utakuwa nyenzo
muhimu ya kufundishia mpira mashuleni na kwenye Academies.
1.7 Tiba, Waalimu na Makocha
TFF
imeandaa mpango wa kukutana na wenyeviti wa vyama vya Tiba, Waamuzi na
Makocha ili kupanga nao mikakati ya maendeleo ya kitaaluma. Mikakati
hii ikiwa tayari itajumuishwa katika mpango mama wa maendeleo wa TFF
(TFF National Business Plan), mpango ambao maandalizi yake yatakamilika
ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa.
1.8 Utawala
TFF
imeanza kwa kuboresha mazingara ya utendaji wa kazi. Vyama shiriki
TAFCA, FRAT, TASMA, TWFA na SPUTANZA tayari vimepatiwa ofisi za kisasa
katika eneo la Ilala. Ofisi kuu za TFF nazo ziko mbioni kuhamia katika
jengo la kisasa la PPF Tower,nia ikiwa ni kuiwekea sekretariet ya TFF
mazingira ya kisasa ya kufanyia kazi na pia kupisha ujenzi wa kitega
uchumi eneo letu la Uwanja wa Karume.
Aidha
TFF imeunda kamati maalum (Adhoc) ya kupitia Muundo wa Bodi ya Ligi
lengo likiwa ni kutekeleza maagizo ya Mkutano Mkuu wa TFF ulioagiza Bodi
ya Ligi iundwe ikiwa ni ya mpito kuelekea uundwaji wa Kampuni ya
kuendesha Ligi Kuu ya mpira wa miguu.
1.9 Mahusiano na Zanzibar
Mahusiano
kati ya TFF na Chama cha mpira Zanzibar (ZFA) yamezidi kuimarishwa
kufuatia ziara kadhaa ambazo tumezifanya kati ya maeneo yetu mawili.
Mipango ya kuimarisha timu zetu za Taifa za wakubwa, za vijana na za
wanawake inafanywa kwa pamoja. Juhudi za kuhakikisha Zanzibar inajiunga
na FIFA pia zinaendelea kupitia mazungumzo na wahusika.
1.10 Vilabu vya Mpira
Mara baada ya kuingia madarakani Uongozi wa TFF ulikutana na viongozi
wa vilabu vyote vya Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza. Kikao hiki
kilifanyika kama sehemu ya kuangalia ni maboresho gani yafanyike ili
kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa Ligi zetu. Utekelezaji wa
maazimio ya kikao hicho unaendelea kupitia wahusika mbalimbali.
1.11 Wachezaji
SPUTANZA wameleta TFF mapendekezo yao ya jinsi ya kuboresha maslahi ya
wachezaji wa mpira wawapo mpirani na baada ya kustaafu kucheza soka.
TFF inayafanyia kazi mapendekezo hayo. Lakini kubwa litakuwa ni
kuanzisha Mfuko Maalum (Trust Fund) utakaochangiwa na wachezaji wakiwa
bado wanacheza pamoja na TFF na taasisi nyingine ili mfuko huu uwasaidie
pindi wakistaafu.
1.12 Masoko na Uwekezaji
Kama nilivyoeleza hapo juu TFF iko mbioni kuwekeza katika Kiwanja cha
Karume, lakni pia njia nyingine za kuiongezea TFF mapato ziko mbioni
kuanzishwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha utaratibu maalum wa kuuza jezi
za Timu ya Taifa (replica shirts).
1.13 Kitengo cha Habari
TFF imeandaa utaratibu wa kuboresha kitengo hiki kwa kukiongezea nguvu
kazi ili upashanaji wa habari uwe ni wa haraka zaidi ikiwa ni pamoja na
TFF kuanzisha Blog yake,kuboresha Tovuti yake, na kuwa na kurasa kwenye
mitandao ya kijamii kama Instagram, Facebook, Twitter, n.k. Press
officer ataajiriwa punde ili kuimarisha kitengo hiki.
1.14 Viwanja
Wakati tunaingia madarakani FIFA kupitia mpango wake wa maendeleo
ilikuwa imekwisha tenga pesa kwa ajili ya kuweza nyasi bandia uwanja wa
kihistora wa Nyamagana jijini Mwanza. Uongozi wetu kwa kushirikiana
na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Meya wa Manispaa ya Mwanza tulifuatilia kwa
karibu na kufanikiwa kuondoa dosari zilizokuwa zimekwamisha mradi huu.
Utandazaji wa nyasi bandia utaanza mara moja kuanzia sasa.
Kwa mafanikio haya Tanzania tuna viwanja vyenye/ vitakavyokuwa na nyasi
bandia baadae ambavyo ni Gombani Pemba, Amani Zanzibar,Uwanja wa Uhuru,
Uwanja wa Karume, Uwanja wa Azam Chamazi na Uwanja wa Nyamagana.
TFF iko mbioni kuanza mazungumzo na baadhi ya vyama vya siasa ambavyo
ni wamiliki wa viwanja kadhaa vya mpira ili kuangalia uwezekano wa
kuingia ubia kwa nia ya kuviendeleza.
1.15 Timu ya Taifa (Taifa Stars)
Ili kuandaa mkakati maalum wa kuboresha timu ya Taifa TFF iliitisha
kikao maalum cha walimu wa mpira waandamizi. Kikao hiki kilifanyika
Zanzibar kati ya tarehe 06-07 Desemba, 2013 na kilitoka na maamuzi
kadhaa. Tarehe 18-19 Januari, 2014 TFF iliitisha kikao kingine maalum
cha Makatibu 30 wa vyama vya mpira vya mikoa yote ya Tanzania Bara na
Zanzibar ajenda ikiwa ni uboreshaji wa Timu ya Taifa (Taifa Stars).
Matunda ya vikao hivi ni mpango kazi maalum ulioandaliwa wa kuboresha
timu ya Taifa kwa kushirikiana na washirika wetu Tanzania Breweries ltd
kupitia bia yao ya Kilimanjaro Lager. Mpango huu utatangazwa rasmi wiki
ya pili ya mwezi February 2014.
CHANGAMOTO:
Uongozi mpya tangia umeingia madarakani umekutana na changamoto kadhaa. Baadhi yake ni kama hizi zifuatazo:
1.Tiketi za Elektronik.
Uongozi
mpya ulipoingia madarakani ulikuta awamu iliyopita ilikwisha saini
mkataba wa mradi huu.Jukumu la uongozi wangu ni kutekeleza masharti ya
mkataba. Changamoto nyingi zimejitokeza ikiwa ni pamoja na mitambo
kuzima mara kwa mara,mitambo kufanya kazi kwa spidi ndogo , mageti
yaliyofungwa mashine hizi kuwa machache (mfano Mkwakwani yamefungwa
mitambo miwili katika uwanja unaoingiza watu zaidi ya elfu kumi,uwanja
wa Taifa mitambo 48 wakati unaingiza watu 60,000,linganisha na uwanja wa
Emirates London unaoingiza watu 60,000 mitambo imefungwa 125,karibia
mara tatu ya uwanja wetu wa Taifa). Pia uelewa mdogo wa wadau kuhusu
taratibu za utumiaji tiketi hizi nao ni tatizo na mkataba wa TFF na CRDB
unaitaka TFF ibebe jukumu la kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi ya
tiketi hizi na bajeti yake haipungui shilingi milioni 500 ikijumuisha
gharama za matangazo kwenye
radio,magazeti,televisheni,roadshows,mabango,vipeperushi n.k. Matokeo
yake yalikuwa ni vurugu katika baadhi ya viwanja, vurugu ambazo kama si
busara za TFF zingeweza kusababisha maafa.Mazungumzo yanaendelea kati ya
TFF na mzabuni CRDB ili kutafuta namna ya kuboresha utaratibu wa mfumo
wa tiketi za elektronik,lakini pia ni kuangalia ni kwa jinsi gani
tiketi hizi hazigeuki kuwa mzigo kwa mlaji maana licha ya watazamaji
kulipia gharama ya tiketi yenyewe lakini bado kuna asilimia inakatwa
kama kamisheni ya uwakala jambo ambalo pia ni mzigo kwa vilabu.TFF ina
nia thabiti ya kutumia utaratibu huu,ni mzuri iwapo utatekelezwa kwa
taratibu stahili.
- Ufinyu wa bajeti
TFF
katika kutimiza majukumu yake inahitaji pesa nyingi hasa kuendeleza
mpira wa vijana, kukidhi gharama za kuendesha ofisi, kuvipa nguvu vyama
wanachama na kusimamia timu zake nane za Taifa (Za wakubwa mbili
wanawake/wanaume,U17 mbili,U20 mbili na za olimpiki mbili).Eneo lenye
ufadhili mkubwa ni timu ya Taifa ya wanaume tu.Hivyo ni dhahiri mahitaji
ya fedha TFF ni makubwa sana na vyanzo havikidhi.Jitihada zinafanyika
kuhakikisha tunaongeza vyanzo mbadala wa mapato.
- Madeni
Madeni
ambayo uongozi mpya ulipoingia madarakani uliyakuta ni makubwa na
yamelielemea shirikisho. Juhudi za kuongea na wanaotudai ili aidha
watupunguzie madai yao au tuyalipe kwa masharti nafuu yanaendelea.Wale
wote wanaotudai ambao wametuelewa katika hili tunawashukuru sana. Kwa
sasa kesi zote za madai dhidi ya TFF zilizokuwa mahakamani zimeondolewa
baada ya mapatano.
- Nidhamu
Nidhamu
bado ni tatizo si kwa wachezaji bali hata kwa viongozi wetu.Yupo
mchezaji amediriki kupigana na walinzi wa raia na wengine wakadiriki
kumpiga mwamuzi,hili halikubaliki na hatua kali zitakuwa zinatolewa
dhidi ya watovu wa nidhamu bila kujali wao ni kina nani kwenye mpira wa
nchi hii.
- Maadili
Wizi
mdogo mdogo hasa wa mapato ya milangoni umeendelea.TFF tumekuta kesi za
wizi wa aina hii zaidi ya hamsini zilizoripotiwa polisi Chang’ombe na
watuhumiwa hawakuwahi kupelekwa mahakamani kwa kuwa mlalamikaji (TFF)
hakujitokeza kuandika taarifa (statement). Uongozi wangu umeamua utakuwa
unafuatilia kwa karibu kesi hizi ili kukomesha tabia iliyozoeleka ya
udokozi.Pesa ya mpira itumike kwenye mpira.
- Maamuzi uwanjani (Refeering)
Wapo
waamuzi wanaokosea kwa makosa ya kibanadamu, hao tunawaelewa.Lakini
zinapotokea tetesi au tuhuma za haki kutotendeka kiwanjani kwa sababu
nyingine zaidi ya hii shirikisho linashtuka sana na kamwe halitakubali
lidhalilike kwa tuhuma kama hizi.Shirikisho kwa sasa linafuatilia kwa
karibu kinachoendelea uwanjani ili kuhakikisha haki inatendeka kwa timu
zote. Tayari mitihani imekwisha fanyika kupandisha madaraja waamuzi
mbali mbali ili kuongeza uwigo wa kupata waamuzi.Kozi za waamuzi
zitaendelea kutolewa ili kuzidi kunoa uwezo wao.
Aidha
vituo vya kuendeleza waamuzi vijana vya kambi ya Jenerali Twalipo na
Alliance academy Mwanza viko mbioni kuimarishwa ili viwe na nguvu
zaidi ya kufundisha waamuzi vijana.
HITIMISHO
Ndugu zangu nihitimishe kwa kutoa wito kwa wadau wote wa Mpira wa Miguu Tanzania wakiongozwa na
Serikali, CAF, FIFA, CECAFA, vyombo vya habari, Mashirika ya Umma,
Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Makampuni na watu binafsi wote kwa
pamoja tushikamane kwa pamoja tukiwa na nia moja tu, kuinua kiwango cha
mpira Tanzania na kuzifanya timu zetu za mpira ziwe za wakubwa, za
wanawake na za vijana ziwike, sio tu barani Afrika, bali duniani pote. Kwa pamoja tunaweza.
Tukijaliwa
tutakutana tena ndani ya chumba hiki hiki baada ya siku 365 tangia
nimechaguliwa kuongoza TFF ili tufanye tathmini ya mwaka mmoja wa
uongozi wangu.
Mungu ibariki TFF, Mungu Ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika,"
Jamal Malinzi, Rais wa TFF, 07 Januari, 2014.

No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako