RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya
Kikwete ameeleza mshituko na masikitiko yake kufuatia kifo cha Mkuu wa
Chuo Kikuu cha Dar Es salaam (UDSM), Balozi Fulgence Kazaura
kilichotokea nchini India usiku wa jana, Jumamosi, Februari 22, 2014.
Katika salamu zake za rambirambi kwa
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Rais Kikwete amesema:
“Nimepokea kwa mshituko, masikitiko na huzuni taarifa ya kifo cha Mkuu
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Balozi Flugence Kazaura, ambacho
nimejulishwa kuwa kimetokea katika Kituo cha Matibabu ya Kansa katika
mji wa Chennai, nchini India.”
“Kwa hakika, kifo cha Mzee Kazaura siyo kwamba kimekipokonya Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam kiongozi hodari na mwenye visheni kubwa, lakini
kifo hicho kimeondolea Tanzania mmoja wa watumishi hodari wa umma. Mzee
Kazaura pia alikuwa mtumishi mwaminifu na mwadilifu kwa nchi yake na
sote tunaendelea kwa kumkumbuka kwa sifa hizo na mchango wake mkubwa
katika utumishi wa umma,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Alithibitisha sifa hizo katika nafasi zote alizozishikilia katika
maisha yake tokea alipokuwa Katibu Mkuu katika wizara mbali, hadi
alipokuwa Balozi wa Tanzania Makao Makuu ya Umoja wa Ulaya (EU) na
nchini Ubelgiji, hadi alipoteuliwa Mshauri Maalum wa Uchumi wa Rais,
hadi alipokuwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuia ya Afrika Mashairiki (EAC)
katika uongozi mbali mbali za Bodi za mashirika ya umma na binafsi na
hata kwenye nafasi yake ya Ukuu wa Chuo Kikuu cha Dar Es salaam kwa
miaka tisa. Tutaendelea kumkumbuka.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Nakutumia wewe Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Dkt. Shukuru Kawambwa salamu zangu za rambirambi kufuatia msiba
huu mkubwa. Aidha, kupitia kwako naitumia jumuia nzima ya Chuo Kikuu
cha Dar Es Salaam pole nyingi kwa kuondokewa na kiongozi wao.”
“Nakuomba pia unifikisshie salamu zangu za pole nyingi kwa familia ya
Mzee Kazaura. Wajulishe kuwa naungana nao katika kuomboleza kifo cha
Mzee wetu huyu na kwamba msiba wao ni msiba wangu pia. Pia naomba wajue
kuwa naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema,
aiweke mahali pema peponi roho ya Marehemu Fulgence Kazaura. Amina.”
No comments:
Post a Comment
Toa maoni yako lakini angalia kuchafua hali ya hewa na usimuumize mwenzako